Habari za Punde

ZSTC yanunua tani 3,101 za karafuu Unguja, Pemba


HABIBA ZARALI, PEMBA              

TANI 3,101 za karafuu kavu zenye thamani ya shilingi bilioni 43.4 kutoka kwa wakulima wa Unguja na Pemba, zimeshanunuliwa na Shirika la Biashara la Taifa ZSTC tokea kuanza kwa msimu mwezi Julai mwaka huu.

Katika kisiwa cha Pemba pekee, Shirika hilo limeshanunuwa tani 3,072 zenye thamani ya shilingi bilioni 43, na kisiwa cha Unguja limenunuwa tani 28.2 zenye thamani ya shilingi milioni 400.

Akizugumza katika ziara yake ya ukaguzi wa ununuzi wa zao la karafuu Mkoani kisiwani Pemba, Mkurugenzi Muendeshaji wa shirika hilo Said Seif Mzee, alisema shirika la hilo, bado lina uwezo wa kununuwa karafuu ambazo zitapelekwa kuuzwa.

Alisema ZSTC ipo kwa ajili ya wananchi, hivyo ni vyema wakaitumia kuuzia zao hilo, ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

“Wananchi wasiwe na wasiwasi kuhusu shirika hili, waendelee kuleta karafuu zao na kuziuza bila ya hofu, na zitanunuliwa zote”,alisema.

Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa, wakati wa kuzipeleka karafuu zao kwa ajili ya kuziuza, wahakikishe zimekauka vizuri na wameziondowa uchafu, zikiwemo takataka, ili ziweze kununuliwa kwa sifa na kuondokana na hasara isiyo ya lazima.

Akizungumzia kuhusu elimu iliyotolewa kwa ajili ya wakulima wa zao hilo, imefahamika kutokana na wananchi waliowengi huzipeleka karafuu zikiwa katika hali nzuri.

“Karafuu zinapoletwa ZSTC zikiwa kavu na safi, zinarahisisha kazi kwa Shirika na kwa muuzaji pia kwani hakumbani na tatizo lolote ikiwemo la kurejeshwa kuanikwa na kuzidondowa takaka mara mbili.

 Wakati huohuo, aliwashauri wananchi kuacha tabia ya kuzichuma karafuu zikiwa changa kwani zinakuwa nyepesi na hupelekea kukosa faida kwa mkulima.

Kwa upande wake mkulima wa zao hilo kutoka kangani Ali 
Nassor Khamis, alilishauri Shirika hilo, kuwaongezea mezani ya kupimia katika kituo kilichopo Mkoani, kwani hulazimika kukaa foleni kubwa hasa katika siku ya Jumatatu na Ijumaa kwa vile watu wengi wanakwenda kuuza karafuu zao.

“Pamoja na kuweko kwa vituo katika vijiji vyetu lakini mzigo ukiwa mwingi ndo tunaona tuje huku kuondokana na usumbufu wa kupima kidogo kidogo,alisema.

Nae mkulima Jide Said Rashid kutoka Tironi Mkoani alisema changamoto inayowakabili katika kufikisha zao hilo ZSTC ni kutokuwa na usafiri katika kijiji chao, jambo ambalo linawapa ugumu wanapotaka kuuza zao lao.

“Sisi katika kijiji chetu cha Tironi, hatuna usafiri wa kuzileta karafuu zetu ZSCT kwani tuna ubovu wa barabara na karafuu ziko nyingi hufika pahala tukashindwa hatuna la kufanya”,alisema.

Alifahamisha hadi sasa mezani ya kupimia ni nzuri na  haina  tatizo lolote na kuwashauri wakulima wenzake, wazipeleke karafuu zao katika shirika hilo kwa ajili ya mauzo.

Mdhamini wa shirika hilo Pemba Abdalla Ali Ussi alitowa maelekezo kwa wakulima ambao wako vjiji vya ndani ambako ni vigumu kupata usafiri wa kuzipeleka karafuu zao ZSTC wajikusanye pamoja na kutowa taarifa kwa kwa ajili kupewa usafiri.

“Lakini ni vyema wakajikusanya kwa pamoja ili tukizichukuwa zikawa nyingi tusije tukawapelekea usafiri ikawa ni hasara baada ya faida”alifahamisha.

Hivyo aliwashukuru wakulima wanaoendelea kupeleka karafuu zao katika shirika hilo, na kuwataka wengine kufanya hivyo, ili kuweza kuunga mkono na kutimiza lengo lililokusudiwa

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.