Habari za Punde

Mgeni Rasmin Mahafali ya 12 Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalim Nyerere Mkurugenzi Idara ya Elimu Mbadala na Watu wazima Zanzibar.

Mkurugenzi Idara ya Elimu mbadala na watu wazima Zanzibar Bi Mashavu Ahmada Fakih amewataka wahitimu wa chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kujiandaa kisaikolojia na kutumia stadi walizozipata Chuoni hapo katika kuboresha maisha yao.

Bi Mashavu aliyasema hayo leo Mjini  Dar-es-Saalam  wakati alipofunga mahafali ya kumi na mbili ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kuwapongeza wahitimu wote waliohitimu masomo yao na kusema wana kila sababu ya kusherehekea siku yao hiyo.

Pia aliwaomba wahitimu hao kufanyia kazi kwa uweledi mkubwa mafunzo waliyoyapata ili kudumisha maadili mema ya utendaji kazi na kujiepusha na vitendo vya kutoa au kupokea rushwa, vitendo vya ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma ili kuunga mkono juhudi za Serikali yetu ya awamu ya tano ya kuhakikisha Tanzania inafikia uchumi wa kati wa viwanda.

 Aidha alimshukuru Mkuu wa Chuo pamoja na uongozi mzima wa Chuo kwa heshima aliyopewa ya kuwa Mgeni Rasmi katika mahafali hayo hata hivyo hakusita kuupongeza uongozi huo, wanataaluma na watumishi waendeshaji wa Chuo na wanafunzi kwa ujumla kwa kazi nzuri waliyoifanya na wanayoendelea kuifanya katika kutekeleza majukumu yao, hasa ya utoaji wa taaluma bora inayokwenda sambamba na Sera ya Elimu ya mwaka 2014 pamoja na kuboresha mazingira na miundombinu ya Chuo hicho. 

Aliongeza kwa kusema Elimu  ndiyo  msingi wa maendeleo kwa binadamu yoyote yule. Aidha Elimu ndiyo inayofungua  milango  ya aina ya maisha tunayoyataka.  Elimu ndiyo inayojenga taswira ya Mwanadamu anavyoonekana mbele ya jamii anayoishi, na elimu hiyo hiyo ndiyo inamfanya Mtu aonekane mstaarabu, atimize majukumu yake kwa ufanisi, na pia kurekebisha mwenendo na matendo yake kwa ujumla. 

Aidha, alichukua fursa ya kuwaasa Wahitimu kujiepusha na tabia hatarishi zinazoweza kuwaharibia maisha yao, kwani tabia hizo ni pamoja na kuendekeza vitendo vya uasharati vinavyosababisha magonjwa ya kuambukiza kama ukimwi na utumiaji wa madawa ya kulevya.

Pia aliwaomba wananchi wote kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano  kwa kuhakikisha watoto wote waliofikia umri wa kwenda shule basi wakawaandikishe ili waweze kupata haki yao ya msingi kabisa ya elimu, kwani elimu ni mfano wa Shamba ambalo unapanda mbegu bora na unavuna mavuno bora.

Hata hivyo aliipongeza taarifa iliyosomwa mapema na Mkuu wa Chuo hicho, inaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi imeongezeka sana hadi kufikia 4132 sawa na asilimia 85 ukilinganisha na wanafunzi 1570 katika mwaka 2015. Aidha, katika kampasi ya Zanzibar, idadi imeongezeka hadi kufikia 1075 ukilinganisha na wanafunzi 22 katika mwaka 2015. Hali hii ni dalili njema kwa Chuo kwani inaonyesha ni jinsi gani wazazi na wanafunzi walivyo na imani ya ubora wa mafunzo na huduma zinazotolewa na Chuo hiki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.