Habari za Punde

Balozi Seif Afungua Mkutano wa Wajasiriamali Kuhusiana na Fursa Kwa Vijana.

Baadhi ya Vijana washiriki wa Semina ya  Mafunzo ya kuwajenge uwezo Vijana wa kupata fursa za ajira wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo hapo Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni jijini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifungua Semina ya Mafunzo ya Fursa kwa Vijana Wajasiriamali yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Kiraia ya Fursa Tanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifungua Semina ya Mafunzo ya Fursa kwa Vijana Wajasiriamali yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Kiraia ya Fursa Tanzania.
Muanzilishi ambae pia ni msimamizi wa programu ya mafunzo ya Jumuiya Fursa Tanzania Bwana Ruge Mutahaba  akitoa darsa kwa Vijana walioshiriki wa Semina ya Mafunzo ya Fursa kwa Vijana Wajasiriamali Zanzibar.
Muwakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa { UN} yanayofanyakazi Nchini Tanzania  Bwana Alvaro Rudge akitoa salamu katika hafla ya ufunguzi wa Semina ya Mafunzo ya Fursa kwa Vijana Wajasiriamali Zanzibar.
Baadhi ya Vijana Washiriki wa Semina ya Mafunzo ya Fursa kwa Vijana Wajasiriamali Zanzibar  byaliyofanyika katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni jinni Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia moja ya Nembo za Jumuiya ya Fursa Tanzania inayotoa ujumbe wa         { Nipo Tayari } katika Kampeni ya Kitaifa ya usafi wa Mazingira.Kulia ya Balozi Seif ni Muwakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa { UN} yanayofanyakazi Nchini Tanzania  Bwana Alvaro Rudge, Mbunge wa Jimbo la Mpendae Mh. Salum Turky na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud.
Picha na - OMPR - ZNZ.
Na. Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Tanzania imebarikiwa kuwa na idadi kuwa ya Wajasiriamali, lakini ni asilimia ndogo tu ya Wajasiriamali hao wenye ujuzi wa usimamizi wa Biashara, Taarifa na Maarifa  ya kiufundi  yanayohitajika ili kukuza biashara na kuwa na ushindani kwenye soko husika.
Alisema ukosefu wa Taaluma hizo hupelekea Biashara nyingi kufa kutokana na kushindwa kuendana na na mahitaji halisi sambamba na kushindwa kufikia ushindani wa soko.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akifungua Semina ya Mafunzo ya Fursa kwa Vijana Wajasiriamali yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Kiraia ya Fursa Tanzania yaliyofanyika katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakishi Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Alisema Serikali iko tayari kushirikiana na Jumuiya ya Fursa katika kutengeneza na kutekeleza Miakati ya makusudi ili kujenga mazingira bora na wezeshi ya Kibiashara ikiwemo miundombinu katika kusaidia maendeleo ya Wajasiriamali na Vijana Nchini.
Balozi Seif alisema Taifa la Tanzania hivi sasa limo katika ujenzi na uimarishaji wa Uchumi wa Viwanda azma ambayo katika kufikia hilo, kundi la wajasiriamali lazima lizalishwe kwa wingi ili kuanzisha, kukuza na kuendeleza Viwanda hivyo na kutengeneza ajira, kuchochea uvumbuzi na kuhamasisha ushindani wa soko.
Alielezea faraja yake kutokana na juhudi  kubwa zinazochukuliwa na Jumuiya ya Fursa iliyoanzishwa Miaka Mitano iliyopita ya kufanya kazi na Vijana, Serikali Jamii na Washirika wengine wa Maendeleo katika kutatua changamoto zinazowakabili Vijana ikiwemo kuondoa umaskini hasa kwa Vijana wa Vijijini.
“ Fursa imekuwa ikizunguuka Nchi nzima Tanzania ili kuzungumza na Vijana ambapo tayari Mikoa 13 ya Tanzania imeshapata Semina zinazoandaliwa na Taasisi hiyo ya Kiraia”. Alifafanua Balozi Seif.
Mapema akitoa Taarifa ya Jumuiya ya Fursa Tanzania Muanzilishi wa Taasisi hiyo ambae pia ni msimamizi wa programu ya mafunzo ya iliyolenga kuwakomboa Vijana na Maisha duni Bwana Ruge Mutahaba  alisema  ni vyema kwa Kila Mjasiriamali kubuni kitu kitakachomuhitaji jirani au mwenzake mfumo ambao unaibua ajira na thamani ya kipato.
Bwana Ruge alitahadharisha wazi kwamba wakati umefika kwa jamii hasa Vijana kuondokana na mawazo mgando ambayo yanaviza upeo wa ufikiri wa mabadiliko ya mahitaji yanayotarajiwa ndani ya Jamii katika kueleka kwenye upeo wa maendeleo.
Alisema Vijana wanaomaliza masomo na wale walioko vyuoni kutokana na mabadiliko ya ufinyu wa fursa za ajira Kitaifa na Kimataifa wanalazimika kujitia hasira katika kufikiria njia zitakazowaongoza katika kuendesha maisha yao kwa amani na furaha hapo baadae.
Akifafanua tafsiri ya Ajira Msimamizi huyo wa Program za Mafunzo ya fursa za kujikimu alieleza wazi kwamba fursa za ajira ni kwa Mtu mwenyewe kuanzia kufikiria atafanya nini  mara anapomaliza mafunzo yake skulini.
Alisema ni vyema kwa Wanafunzi wa sekondari na Vyuo kuanza kufikiria namna atakapoingia katika fursa bado akiwa masomoni  ili amalizapa masomo aanze kuendelea na maisha yake bila ya kuyumba na wasi wasi wowote.
Alitahadharisha kwamba wapo wazee waliopata fursa za kufanyakazi katika Taasisi za umma wakiwa na nafasi nzuri lakini hatma yao inakuwa mbovu kutokana na kushindwa kujiwekea misingi imara mapema wakati wa utumishi wake.
Akimkaribisha Mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo hayo ya fursa kwa Vijana Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud aliwakumbusha Vijana kuchangamkia fursa za ajira hasa katika Sekta za Utalii na Uvuvi.
Mh. Ayoub alisema Serikali tayari imeshatekeleza wajibu wake wa kuimarisha miundombinu pamoja na Sera ili kutoa nafasi kwa jamii kuendesha maisha yao katika misingi ya amani na utulivu, kilichobakia kwa watu hasa Vijana kutumia nafasi hizo.
“ Serikali kazi yake kubwa ni kutengeneza mazingira rafiki ili Jamii na Wageni waendeshe maisha yao katika maisha na misingi ya amani na Utulivu ”. Alisema Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mhmoud.
Mkuu huyo wa Mkoa Mjini Magharibi alisisitiza kwamba asilimia 27%  ya Mapato ya Taifa inayotokana na Utalii imezalisha ajira zaidi ya 88,000 ambazo nyingi zimechukuliwa na wageni kutokana na Wazawa kutochangamkia fursa katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa Nchi.
Akitoa salamu za Mashirika ya Umoja wa Mataifa { UN} yanayofanyakazi Nchini Tanzania, Muwakilishi wa Taasisi hizo Bwana Alvaro Rudge alisema Umoja wa Mataifa kupitia Taasisi zake hizo utaendelea kutoa Taaluma kwa Wanawake ili kuwajengea uwezo wa kujiendesha Kimaisha.
Bwana Alvaro alisema hakuna Taifa lolote Duniani linaloweza kupiga hatua za Kiuchumi bila ya mchango wa Maendeleo ya Wanawake ambao wanastahiki kupewa msukumona kujengewa mazingira mazuri  ili kufikia lengo hilo.
Mwakilishi huyo wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa aliahidi kwamba Umoja huo utaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Fursa Tanzania ili kusaidia nguvu zitakazopelekea kupunguza au kuondosha kabisa changamoto zinazowakabili Vijana hasa kundi kubwa la Wanawake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.