Habari za Punde

Matamu, machungu ukodishaji mashamba ya mikarafuu Pemba haya


Na mwandishi wetu.

MWEZI Julai  mwaka huu, Makamu wa pili wa rasi wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, alifanya uzinduzi wa uchumaji wa zao la karafuu, kwenye kijiji cha Changaweni wilaya ya Mkoani, kisiwani Pemba.

Ni eneo lenye idadi kubwa ya mikarafuu, ambapo mwambao huo, unaelekea Tironi, Manyaga, Fumbani na ukiamua kukosa sana hadi mabonde ya Wambaa kama sio Makombeni.

Kwa ujumla Mkoa wa kusini Pemba, uanounda wilaya za Chakechake na Mkoani, ndio wenye idadi kubwa ya Mikarafuu, kuliko wilaya za Micheweni na Wete, zilizoko Mkoa wa kaskazini Pemba.

Zoezi la uchumaji wa zao hilo, bila shaka kuliashiria pia ukodishwaji wa mashamba yale ya serikali, umaarufu eka tatu tatu, ambazo ukweli ni urithi wa akili ya rais wa kwanza wa Zanzibar, sheikh Abeid Amani Karume.

Eka tatu ni mashamba maalumu yaliokatiwa wananchi wa nchi hii, tokea uhai wake, ambapo wamiliki wa mwanzo wanapofariki, hutakiwa wale wanaotaka kuyaendeleza wayaombe serikalini.

Wapo waliofanya hivyo kwa karne, maana walikuwa wanajua, na wengine wapo waliojichukulia, aidha kwa ujanja ujanja au kwa kujua kuwa, wanalinda na kuienzi mali ya serikali.

Miaka nenda miaka mirudi, serikali hii ya Mapuinduzi ya Zanzibara ya awamu ya saba, inayoongozwa na rais wake mahiri Mhe: dk Ali Mohamed Shein ikionyeshwa kuchoka kuibiwa.

Ndio maana sasa, ndani ya msimu huu au kabla ya kuanza, ikadhamiria kwa nia safi kabisa, kuyasaka, kuyatafuta, kuyazinga, kuyarudisha mashamba yote ya serikali na hasa ambao hata waliomilikishwa wameshafariki.

Hapo zoezi la pata shika nguo chanika kisha shoneka, ikaanza kwa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, kuwa kinara wa zoezi la ukosdishaji na utambuzi.

Matamu ya ukodishaji

Kamati ya ukodishwaji ikaundwa chini ya Mwenyekiti wake Haji Mussa Haji, ambae ni mtendaji ndani ya wizara ya Kilimo, ili kuhakikisha wanapita wilya zote nne kufanya kazi ya ukodishaji.

Kazi ya kuingia msitu hadi msitu, mabonde na milima ikaendelea kwa kuchupa mito, mizizi, kupita vichaka kadhaa vya wilaya zote nne, ili kuhakikisha zoezi linakamilika tena kwa mafanikio.

Kumbe serikali inayoa mashamba kadhaa, ambayo yalikuwa mikononi mwa wachache, wakila, wakinywa, wakivaa na kujitibia kwa mali ya umma.

Maana kamati hiyo ya ukodishwaji na wizara kwa ujumla, ilidhamiria kuhakikisha inayaibua mashamba walau 1,525 kisiwani Pemba pekee.

Na hapo iliona kwa wastani kama yakipatikana na mashamba hayo, na yakikodishwa kisha waliokoadi kuamua kulipa fedha kama ilivyo kwenye mikataba ya zoezi hilol basi serikali hii, ingejipatia shilingi zaidi ya bilioni 2.393.

Lakini kutokana na kazi nzuri, iliofanywa na Kamati ya ukodishwaji mshamba ya serikali, ikiambatana na wakuu wa mikoa na wilaya, basi haikufanya vibaya sana, maana waliyapata mashamba 1,451.

Ingawa hapa fedha ambazo zimeshaingia kwenye accounti ya serikali, kama sio wizara husika ni wastani wa shilingi milioni 900.661.

Walishasema wahenga kuwa, mpango sio matumizi wala, mwenye nacho hamjui mkosaji, na ndio maana inawezekana waliokodishwa wameshachuma, lakini kurejesha wanahitaji mtutu wa bunduki.

Kumbe azma ya serikali ya kuyatafuta kwa udi na uvumba mashamba yake, ni kuona sasa kwa misimu ijayo, wanayatambua mashamba, na kuachana na ule wa mpango wa zamani eti kuvuna milioni 100 pekee kwa ukodishwaji.

Zuri ambalo pia limezingatiwa na kamati hii pamoja na mamlaka nyengine za juu, kama sio sheria husika, ni kuhakikisha mara mnada wa ukodishaji umalizikapo, ni kumsikiliza anae lilea shamba.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Haji Mussa Haji, anasema bei yoyote iliofikiwa iwe kubwa au ndogo, lazima wa kwanza kuulizwa iwapo ana mudu kulikodai shamba ni anaelilea.

Kwa mfano shamba limefikia shilingi milioni 18, basi anaelishughulikia ndio huulizwa iwapo anazo fedha hizo na yuko tayari kulikodi.

Zuri ambalo limo kwenye mikataba ya ukodishaji, ni kuwepo kwa fedha, za anaelishughulikia umaarufu ‘kifuta jasho’ ambacho ni asilimia 40 ya bei iliofikiwa.

Kwa mafano shamba limekodishwa kwa bei ya shilingi milioni moja, basi anaelishughulikia hata kama amelikodi yeye, atajikusanyia shilingi 400,000.

Nakumbuka hadi leo hii, kwenye zoezi la uzinduzi wa ukodishwajia wilaya ya Chakechake, mtendaji wa wizara ya kilimo aliemwakilisha Afisa Mdhamini Kilimo, bwana Said Juma Ali, alitamka mengi mazuri.

 Moja kwamba, mara baada ya bei kufikiwa, ya mtu aliekodi shamba la serikali, hutakiwa kulipa asilimia 25 ndani ya siku mbili na kumaliza asilimia 75 ndani ya wiki mbili kama mkataba unavyotaka.

Tena kabla ya kuanza kwa zoezi hilo, kwanza masharti ya mkataba huo, ulikuwa ukisomwa hadharani, kusudi kila mmoja, asikie yaliomo na kuangalia uwezo wake.

Maana wazee wa zamani walishatuwachia usemi kuwa, kila mwenda mbio hushauri nyonga yake, ni sawa na yule mbeba mzigo mzito hungalia nguvu zake.

Kubwa zaidi ambalo linakuja kuwa ni tamu pindi wale wanaodaiwa shilingi bilion 1.492 wakizilipa na kuingia serikali, ambapo itachapuzi maendeleo ya taifa letu.

Wizara ya Kilimo, ilifanikiwa kuyakodi kimakosa mashamba zaidi ya 75, kisiwani Pemba lakini baada ya wenyewe kuzuka na vielelezo husika, ililazimika kuyarejesha kwa wamiliki halali.

“Zozi hili halipo kwa ajili ya kuwachukulia wananchi haki zao, bali ni kuhakikisha mali ya serikali inarudini mikononi mwa serikali na sio kuliwa na wachache”,alisema Afisa Mdhamini Kilimo Sihaba Haji Vuai.

Mchungu ya ukodishaji.

Walishasema waliotangulia kuwa, hakuna jambo lenye faida likakosa na hasara na hasa kwa yale yote yalioasisiwa au kutengenezwa na binadamu.

Maana moja ya donda ambalo limejitokeza kwenye zoezi hili la ukodishaji wa mashamba ya mikarafuu ya eka tatu tatu ni kuzuka kwa malalamiko kwa wale waliokuwa wakiyalea.

Kombo Abdalla Kombo akiwakilisha wenzake, alilia sana baada ya kupewa taarifa kuwa, shamba analolishughulikia linataka kukodishwa.

Shamba hili lililopo mabonde ya Chonga wilaya ya Chakechake, anasema alichokifikiria kwa vile wizara husika, iliyatekeleza kwa zaidi ya miaka 20 mashamba hayo, wengesubiri msimu huu ukamalizika, ndio wakayatafuta.

Akili yake inampelekea kuhoji iweje zaidi ya miaka 20 analilee shamba hilo, bila ya kuulizwa hadi hapo msimu huu ulionawiri, ndio leo hii aelezwe kuwa linatakiwa.

Uchungu aliokuwa nao zaidi, ni baada ya kupigwa mnada na kufikia shilingi milini 18, kwa kuwepo watu aliowaita madalali, wakipandisha bei ili limshinde.

“Mimi hili shamba nimeshapanda mikarafuu 100 mipya, na mikongwe iliomo haizidi 80, na mazao wa mwaka huu wala haukuwa mkubwa, sasa leo linakodishwa kwa mnada wa hadhara bei hiyo, hee”,aliguna.

Abdalla kama walivyowenzake, yeye aliona ushauri wake ni mashamba ambayo yanalelewa na watu, basi kwanza yengefanyiwa tathmini na wizara husika, kisha kuulizwa iwapo wanauwezo ya kuyakodi, na wakishindwa ndio uitishwe mnada wa hadhara.

Chungu jengine lililoibuka kwenye zoezi hilo, ni kwa wananchi iwe kwa wanaoyalea au wamiliki halali, kutopata taarifa sahihi ya zoezi hilo, wakidai kuwa lilikuwa kama la kushitukia.

Taarifa nyengine mbaya na za kusikitisha, wakati wizara ya kilimo ikionekana kuja juu kuyasaka mashamba hayo na kuwataka masheha, watoe ushirikiano, hali ni tofauti maana watendaji wenyewe wa wizara husika wengine sio wasafi.

Kwa vile ZAECA ilikuwa bega kwa bega kwenye zoezi la ukodishaji na utambuzi wa mashamba ya serikali, yenyewe iliyafichua mashamba 30, ambayo yanadaiwa kufichwa na watendaji wa serikali hii.

Maana Mdhamini wa ZAEC Pemba, Suleiman Ame Juma, anasema, mashamba hayo yamo ndani yake yaliofichwa na masheha, watendaji wa wizara ya kilimo au wananchi wanaoelewa zaidi.

“Hivi sasa tunamshikilia mtendaji wa wizara ya kilimo Pemba, ambae alitengeneza kizuka bandis ili shamba moja lililopo Mizingani wilaya ya Mkoani libakie mikononi mwake”,anasema.

Mdhamini akaenda mbali zaidi kuwa, baada ya maofisa wake kufanya kazi walioajiriwa, walimgundua Hassan Hija Maduhushi, kutengeneza kizuka na kumpa ushauri wa siri kwa lengo la shamba hilo, kuwa mikononi mwake.

Baada ya kumuhoji mtendaji huyo wa wizara ya Kilimo, ZAECA iligundua kuwa, shamba hilo, mtendaji huyo lilikuwa la babayake kabla ya kufikwa na umauti, na kushindwa kulirejesha serikali.

Hapa unagundua kuwa kama mtendaji wa serikali kupitia wizara ya kilimo, analishikilia shamba la serikali kwa njia hiyo, sasa la kujiuliza wengine watafanya nini.

Kwa sasa Maduhushi yuko mikononi mwa ZAECA, akisubiri taratibu za kisheria, ili akumbanae na kifungu cha 37 cha sheria no 1 ya mwaka 2012 ya Kuzuia rushwa na uhujumu wa uchumi Zanzibar.

Ingawa ZAECA inamshikilia mtendaji huyo, hata wizara yenyewe inakusudia kuwakabidhiwa, wananchi wanaodaiwa zaidi ya shilingi bilioni 1.492 zinazotokana na ukodishwaji wa mikarafuu, ambao hawajalipa fedha hizo.

Ni kauli ilitolewa na Afisa Mdhamini wa wizara hiyo, kisiwani humo Sihaba Haji Vuai, wakati alipokuwa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, juu ya mwenendo wa ukodishaji na namna ya wananchi waliokodi walivyolipa fedha hizo.

Yeye alisema tayari mashamba 1,451 yameshakodishwa kwa wananchi mbali mbali kisiwani Pemba, ambapo kama ingekuwa wameshalipa, serikali ingepata zaidi ya shilingi bilioni 2.393, ingawa hadi sasa, ni zaidi ya shilingi milioni 900.661 zilizokwishalipwa .

Sasa baada ya kuona, hili linaelekea ndivyo sivyo, hatua inayofuata wakaona, ni kuwakabidhi kwa ZEACA, ili hatua za kisheria sasa zichukuliwe dhidi yao.

Lakini ZAECA, imesema inaendelea kuyatafuta mashamba mengine, iwapo yamefichwa au laa, na wakibaini hilo na wanaamini watayapata, basi ni kuwafungulia mashiataka wahusika.


Ingawa ZAECA wanasema suala la kukodishana mitu na kuwepo kwa mkataba, ni suala la madai hivyo, na wao wanashughulikia zaidi jinai, ingawa wanavipitia vifungu kuona wanawashika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.