Habari za Punde

Watendaji Wizara Tisa Zanzibar wafuja fedha za umma

MAMLAKA ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Wahujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA), imesema wizara tisa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) pamoja na watendaji wake wamebainika kufanya vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma.

Ofisa uchunguzi katika taasisi hiyo, Khamis Bakari alisema Sh bilioni 1.6 zimebainika kupotea katika wizara hizo pamoja na taasisi za vikosi vya ulinzi vya SMZ. Bakari alisema kazi inayofanywa kwa sasa ni kukamilisha uchunguzi na kuwasilisha majalada ya kesi kwa Mkurugenzi wa Mashtaka na Makosa ya Jinai Zanzibar (DPP). “Tumemaliza uchunguzi katika hatua ya mwisho na sasa tunakusudia kuwasilisha majalada ya kesi katika Ofisi DPP kwa hatua nyingine zaidi,” alisema.

Alizitaja wizara ambazo watendaji wake katika Idara ya uhasibu kuhusika na tuhuma hizo ni Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Afya, Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko pamoja na Wizara ya Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo.


Aidha alisema katika ubadhirifu huo vipo vikosi vya Idara ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambavyo ni KMKM, JKU pamoja na Chuo cha Mafunzo Zanzibar. Mwishoni mwa wiki Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Khalid Salum Mohamed akizungumza na wandishi wa habari alikiri kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha huku watendaji 21 wakihusishwa na shutuma hizo. Alisema madai yote ya ubadhirifu wa mali ya umma kwa watumishi wa serikali yamepelekwa kwa mamlaka ya rushwa na sasa yapo katika hatua za mwisho kufikishwa Mahakamani kwa ajili ya kufunguliwa kesi.

Chanzo: Habari Leo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.