Habari za Punde

ZAC yalia na wasiotaka kubadili tabia

Na.Haji. Nassor - Pemba.
Tume ya Ukimwi Zanzibar ZAC, ofisi ya Pemba imesema kazi kubwa wanayoifanya ya kuihamasisha jamii ili kudhibiti maambukizi mapya ya VUU na unyanyapaa kwa watu wanaoishi na Ukimwi, haitofanikiwa iwapo watu hawatobadili tabia zao.
Tume hiyo, imesema inaamini jamii ya wazanzibar kwa asilimia 99, wameshafikiwa na elimu ya Ukimwi kwa kupitia njia mbali mbali, na sasa kazi iliopo mbele yao na watu hao kubadili tabia, ili kufikia malengo ya kutokuwa na mgonjwa wowote mpya mwenye VVU.
Kauli hiyo imetolewa na Mratbu wa Tume hiyo, kisiwani Pemba, Nassor Ali Abdalla, wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mjini Chakechake kuelekea maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani.
Alisema kazi ya mtu kubadili tabia ni yake binafsi, na wao kama Tume, hiyo ndio mipaka yao, hivyo kilichobaki ni kuwabembeleza, ili wabadili tabia ya kufikia malengo ya Tume na ya jamii kwa ujumla.
Alisema ingawa takwimu za maambukizi ya VVU yameshuka hasa kwa kisiwani Pemba, kutoka kila watu 1000 kuwa sita (6) wana VVU hadi kufikia idadi kama hiyo, kwa watu watatu (3), lakini hilo isiwe sababu kuacha kubadili tabia.
Alieleza kuwa, Tume ya Ukimwi kazi yake kubwa ni kupanga mikakati, kutoa mbinu, kuelimisha na kuhakikisha inayafikia makundi yote ndani ya jamii, kisha watu wenyewe ndio wafuate miongozo yao.
“Hivi sasa, sisi ndani ya Tume tunajivunia kuwa, kazi tulioifanya kwa kushirikiana na wadau wetu kama vijana, viongozi wa dini vyombo vya habari, viongozi wa serikali na sekta binafsi, imezaa matunda, lakini jamii ibadili tabia ili tufikie malengo” ,alieleza.
Katika hatua nyengine Mratibu huyo wa Tume ya Ukimwi Zanzibar ofisi ya Pemba, Nassor Ali Abdalla, alisema bao Ukimwi upo na kuwatahadharisha wananchi kuwa, wilaya ya Chakechake inaendelea kuwa tishio.
Alisema hilo, linatokana na tafiti mbali mbali zilizofanywa na, kuonyesha maambukizi bado yako juu, hasa kutokana na mchanganyiko mkubwa wa wageni uliopo.
“Sehemu kuu za starehe kwa Pemba ziko wilaya ya Chakechake, wageni wote wanaanzia Chakechake, nyumba za kulala wageni na hoteli nzao zinapatikana hapa, ambapo hivyo na vyengine vinachangia kuibuka kwa watu wapya wenye VVU”,alibainisha.
Hata hivyo, alisema wanakusudia hadi ifikapo mwaka 2020, iwe tayari kila wazanzibar 1000, basi 99 wawe wameshapima na kujua afya zao.
Kuhusu matayarisho ya kuadhimisha siku ya Ukimwi duniani, alisema wao kwa Zanzibar watatangulia kwa siku moja kabla ya Disemba mosi, kutokana na siku yenyewe kuwa ni ndogo kiimani.
Hata hivyo, alisema kwenye maadhimisho hayo, pamoja na hutuba ya mgeni rasmi, watu wanaoishi na VVU watakuwa na maonyesho ya biashara zao mbali mbali, watatoa ushuhuda pamoja na shamra shamra nyengine.
Omar Hassan Abeid, wa Chakechake alisema, elimu ya Ukimwi bado inahitajika ndani ya jamii, hasa kutokana na dira ya ZAC ya kutaka kuondoa wagonjwa wapya wa VVU.
Othaman Yahya Iddi, anaesihi na VVU mwaka wa nne sasa, alisema mpango wa ZAC wa kutegemea wafadhili hata kupita kwenye mabaa na migahawa kutoa elimu, basi wasitarajie kuwa kuna siku hakutakuwa na wagonjwa wapya.
Kwa upande wake, Khadija Ali Waziri wa Madungu, alisema suala la kubadili tabia, ni vyema viongozi wa dini wakawaelimsha wafuasi wao, kila wanapokutana kwenye nyumba zao za ibada.

Tokea kugundulika kwa mgonjwa wa kwanza Zanzibar mwenye VVU mwaka 1986, kisiwani Pemba wapo wananchi wastani wa 1,200 wanaoishi na virusi vya Ukiwmi, ambapi kati ya hao zaidi ya 300, wamekubali kujitangaaza na kujiunga kwenye Jumuia ya watu wanaoshi na VVU.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.