Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ashiriki Katika Uzinduzi wa Usafi Ikiwa Shmrashamra za Sherehe za Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akishiriki usafi wa mazingira katika mwanzo wa shamrashamra za sherehe za Maadhimisho ya kutimia Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwa mgeni rasmi hapo Hospitali ya Chake chake Pemba.
Wananchi pamoja na Wanavikundi vya Mazoezi Mjini Chake Chake Pemba wakishiriki zoezi la usafi wa Mazingira katika mwanzo wa shamra shamra za sherehe za Maadhimisho ya kutimia Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar mgeni rasmi akiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.(Picha na OMPR)


Na. Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umewadia kwa Wananchi kulazimika kujizatiti kikamilifu kwa kushirikiana na Viongozi wa Serikali, Taasisi za Umma na zile za Kijamii katika kupiga vita vitendo vya Udhalilishaji.


Alisema  wimbi la udhalilishaji linaloonekana kuongezeka kila kukicha hivi sasa tayari limeshaathiri jamii na kulitia aibu Taifa ovu ambalo linapaswa kupiga vita na kudhibitiwa kwa nguvu zote.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo mara baada ya kushiriki zoezi la usafi wa Mazingira ikiwa ni mwanzo wa Kumi la  shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia Miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 lililofanyika katika Majengo ya Hospitali ya
Chake chake Kisiwani Pemba.

Alisema wapo watu waliojitoa mshipa wa fahamu wa kuendeleza vitendo vya udhalilishaji vikiwaathiri zaidi watoto Wadogo pamoja na baadhi ya Wazee wenye umri mkubwa mambo yaliyo kinyuume cha ubinaadamu na hata vitabu vya Dini.

Balozi Seif alisema inasikitisha kuona Mtu na nguvu na akili yake anafikia hatua ya kufanya vitendo viovu na vya kinyama wakati akili aliyonayo anaweza kuitumia katika mambo ya msingi ya kuisaidia Jamii iliyomzunguuka.

Aliwalaumu baadhi ya Wazazi kujitumbukiza katika makosa kwa kuendelea kuficha uovu unaofanywa na baadhi ya Jamaa zao kwa hofu ya kujiepusha na migogoro inayoweza kuibuka ndani ya Familia ikihusisha Watu waliomo  ndani ya kundi hilo.

Hata hivyo aliwakumbusha Wazazi wenye tabia ya kuwaozesha mapema Watoto wao na wawaache wasome mpaka ukomo wa uwezo wao kwani kinyume na hivyo watawakosesha haki yao ya kupata Elimu Watoto hao.

Alisema tabia hiyo inayoonekana kubebewa bango na baadhi ya Wazee hasa Vijijni imewaathiri watoto wengi wa Kike ambao wengine wana uwezo wa kupata elimu hadi vyuo vikuu.

Akizungumzia Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 ambapo Taifa hivi sasa linaadhimisha Miaka 54 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema wapo baadhi ya Watu hadi sasa hawajaelewa thamani ya Zanzibar kufanya Mapinduzi.

Balozi Seif  alisema haki za msingi zilizopaswa kuwafikia Wananchi wa daraja zote zilizkuwa zikitolewa kwa Watu maalum wenye uwezo na hadhi ya kiutawala huku Wananchi wa kawaida walikuwa wakiendelea kubaguliwa na kuzikosa huduma za kimsingi za Kibinaadamu.

Alisema haki ya elimu, Afya, Ardhi pamoja na huduma za Maji ilikuwa Wananchi Wazalendo walioongozwa na Jemedari Mzee Abeid Aman Karume walilazimika kufanya Mapinduzi Mwaka 1964 kuondoa ukandamizaji huo wa kinyama.

Balozi Seif  alielezea faraja yake kuona Wananchi waliowengi ndani ya Visiwa vya Zanzibar na Ukanda wa Mwambao wa Tanzania wanaendelea kufaidi Matunda ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

“ Zanzibar ndio pekee inayotoa huduma za Afya bure ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki ”. Alisema Balozi Seif. “ Jamii ilikuwa inatafunana kwa sababu ya Ardhi wakati wa enzi za
Kikoloni, lakini hivi sasa Ardhi hiyo imekombolewa kupitia Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 ”. Alisisitiza Balozi Sdeif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Wazanzibari wote kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza Sera zake za Ardhi kuwa Mali ya Serikali, Elimu na Afya bila ya malipo kwa lengo la kuwafaidisha  Wananchi licha ya gharama kubwa za kuendesha sekta hizo.

Akigusia usafi wa mazingira Balozi Seif alisema wakati umefika kwa Taifa kwa kushirikiana na Wananchi wake kutafuta siku maalum ya kufanya usafi wa mazingira baina ya siku moja katika Wiki au mwezi kwa vile ni jambo msingi lenye kusaidia mapambano dhidi ya maradhi mbali mbali.

Alisema zipo Nchi nyingi Duniani zikiwemo zile za Bara la Afrika zilizopiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kuimarisha usafi wa mazingira uliowapelekea kuongeza matapo yao kutokana na wawekezaji wengi walioshawishika na tabia hiyo ya usafi wa Miji yao.

Mapema Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah alisema sherehe za Mwaka huu za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ni za aina yake kutokana na mfumo wa ushirikishwaji wa Wananchi katika hatua ya awali ya sherehe hizo.

Mhe. Hemed alisema Wananchi wameshuhudia mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya kipindi cha Miaka 54 ya Mapinduzi hayo ambayo kwa sasa wanaweza kuendesha mambo yao wenyewe.

Alisema dhana ya Mapinduzi ni ya Wazanzibari wenyewe iliyowawezesha kujiongoza katika kila nyanja bila ya usimamizi uliokuwa ukifanywa na kuendeshwa na Wakoloni.

Akigusia kasi ya udhalilishaji ulioenea kila pembe ya Visiwa vya Unguja na Pemba Mkuu huyo wa Mkoa wa Kusini Pemba alionya na kuweka wazi kwamba Uongozi wa Mkoa huo hautamuonea haya Mtuj yeyote atakayebainika kuhusika na Vitendo vya udhalilishaji.

Alisema Mkoa huo umejipanga kupiga vita vitendo vya udhalilishaji kwa nguvu zote na kuwaomba Wananchi wote Mkoani humo kutoa ushirikiano utakaosaidia kukabiliana na wimbi hilo hatari kwa Jamii ya watu wa Zanzibar.

Aliipongeza na kuishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa uamuzi wake wa kutoa baraka  za kupiga vita athari za Dawa za Kulevya na vitendo vya Udhalilishaji wa kijinsia unaowaathiri zaidi akina Mama na Watoto wadogo.

Usafi huo wa mazingira uliolenga katika majengo yote ya Hospitali ya Chake chake Pemba umeshirikisha Viongozi wa Serikali, Vikosi vya Ulinzi wa Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar,Vikundi vya Mazoezi pamoja na Wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.