Rais wa Zanzibar na Mwnyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akitowa Salamu za Mwaka Mpya kwa Wananchi wa Zanzibar, na kuwatakia Mwaka Mpya wenye Kheri na Baraka na Mafanikio.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesema kuwa juhudi za kuimarisha ukusanyaji wa mapato
zimeiwezesha Serikali anayoiongoza kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa Kampeni
za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ya kupandisha mishahara ya kima cha chini kwa
asilimia mia kutoka TZS 150,000 mpaka TZS 300,00 kwa mwezi kwa watumishi wa
Serikali.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo katika risala yake ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2018 aliyoitoa
kupitia vyombo vya habari, Ikulu mjini Zanzibar na kusisitiza kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kuongeza pesheni kwa wastaafu na kuendelea kutoa
fedha za Pensheni ya Jamii kwa wazee wote wanaostahiki.
Alieleza kuwa tangu
mwezi April, 2017 walengwa wa nyongeza hizo wamekuwa wakifaidika na neema hiyo
ambapo pia, katika mwaka 2017 Serikali imezidi kuimarisha maslahi ya
wafanyakazi wa sekta binafsi wanaopata mshahara wa kima cha chini jambo ambalo
ni faraja kuona waajiri wengi katika sekta hiyo wameshaitikia wito licha ya
kuwepo baadhi waliotaka kurejesha nyuma juhudi hizo za serikali.
Aliongeza kuwa uchumi
wa Zanzibar unaendelea kuimarika na katika robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2017
(Januari-Machi), kasi ya ukuaji uchumi ilifikia asilimia 6.3 ikilinganishwa na
kasi ya ukuaji wa asilimia 5.2 kwa kipindi kama hicho cha robo mwaka ya kwanza
ya mwaka 2016 ambapo katika kipindi cha robo mwaka ya pili (Aprili-Juni) kwa
mwaka 2017 ukuaji wa uchumi nao uliimarika na kufikia asilimia 8.2.
Hivyo, Dk. Shein
alieleza kuwa ni jukumu la kila mmoja katika mwaka huu mpya wa 2018 la kuongeza
juhudi ili kuhakikisha kuwa yanaendelea kutekelezwa vizuri malengo hayo
yaliobainishwa kwenye MKUZA III na mipango mengine ya maendeleo.
Dk. Shein aliendelea
kutoa pongezi kwa wananchi wa Mikoa yote ya Zanzibar kwa juhudi zao kwa
maendeleo ya kutia moyo yaliyopatikana katika sekta mbali mbali za maendeleo kwenye
ziara za Mikoa aliyofanya Unguja na Pemba zikiwemo sekta za kiuchumi na kijamii
ikiwa ni katika kutekeleza Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020,
Dira ya Maendeleo ya 2020, MKUZA 111 na Malengo ya Maendeleo Endelevu
yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa Serikali imepiga hatua kubwa
katika ujenzi wa miundombinu mbali mbali katika sekta ya afya na hivi
sasa juhudi kubwa zimeelekezwa katika kuimarisha huduma pamoja na upatikanaji
wa dawa na vifaa vya utibabu katika hospitali na vituo vya afya.
Aliongeza kuwa katika
mwaka wa fedha uliomalizika 2017/2018, Serikali imetenga jumla ya TZS 7.0
bilioni kwa ununuzi wa dawa na vifaa vya utibabu, sawa na ongezeko la asilimia
42.9 ikilinganishwa na kiwango kilichotengwa kwa mwaka 2016/2017.
Kwa upande wa sekta ya
elimu, Dk. Shein alisema kuwa ikiwa tayari serikali imeshaanza ujenzi wa mradi
wa skuli 9 za ghorofa katika sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba, ili
kuimarisha mazingira ya kusomea kwa wanafunzi hapa nchini ambapo ujenzi wa skuli
hizo utagharimu jumla ya TZS 24.4 bilioni ambazo ni mkopo kutoka Mfuko wa OPEC
dhamira ikiwa ni kumaliza ujenzi wa skuli hizo ifikapo Januari mwaka 2019.
Dk. Shein alieleza
kuwa katika sherehe za Elimu bila ya malipo zilizofanyika tarehe 23 Septemba,
2017 alitangaza rasmi kuondoa michango katika elimu ya Sekondari kuanzia mwezi
wa Julai, 2018 hatua iliyolenga kuendeleza utoaji wa elimu bila ya malipo kwa
skuli zote za msingi na sekondari kwa watoto wote kwa misingi ile ile
iliyoanzishwa na waasisi wa nchi hii.
Alieleza kuwa mwaka
2017 unamalizika ikiwa tayari kazi ya kulishuhulikia tatizo la kupoteza fedha
za mishahara kwa wafanyakazi wanaochukua likizo bila ya malipo, wanaotoroka
kazini, wanaolipwa kinyume na utaratibu (hewa), ambapo taarifa rasmin itatolewa
na Serikali muda mfupi ujao.
Aliongeza kuwa katika
mwaka 2018, Serikali inaendeleza utafiti wa mafuta na gesi kwa kutegemea
taarifa itakayotolewa na wataalamu na kutoa wito kwa wananchi kuwa watulivu na
Serikali itatoa taarifa rasmi ya matokeo ya utafiti huo unaofanywa kwa maslahi
ya Zanzibar.
Aliwataka wananchi
kutosikiliza maneno ya mitaani na kwenye mitandao wakati serikali yao ipo na
kuwataka kuendelea kuunga mkono juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali
katika kuiendeleza sekta yua Mafuta na Gesi Asilia.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alisema kuwa Mpango Maalum wa Kulifufua Zao la Karafuu ulioanzishwa mara
tu baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba kuingia madarakani
mwaka 2010 kwa kupanda mikarafuu mipya limeanza kutoa matokeo mazuri.
Alisema kuwa hadi
tarehe 20 Disemba, 2017 wakulima wa karafuu walikuwa wameshauza karafuu ZSTC
zenye thamani ya TZS 108.8 bilioni ambapo
kiwango hicho cha fedha kimekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha
mzunguko wa fedha na kukuza sekta nyengine za kiuchumi.
Dk. Shein alisema kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wote wanaendelea kuwakumbuka
wakati wote wanajeshi 15 wa Jeshi la Wanachi wa Tanzania waliofariki huko
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako walikuwa katika shughuli za kusimamia
amani chini ya uongozi wa Umoja wa Mataifa.
Alisema kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika kupanga na kutekeleza mikakati mbali mbali ya
kulinda na kudumisha amani nchini, Barani Afrika na duniani kote kwa jumla.
Dk. Shein pia,
aliwasisitiza wananchi wakati wakiupokea mwaka mpya wa 2018, kila mmoja aweke
dhamira ya dhati ya kufanya kazi kwa bidii na maarifa na kuongeza jitihada za
kuongeza kipato na kupambana na umasikini.
Aliwataka wananchi
kushirikiana na Serikali kwa lengo la kuimarisha utawala bora, kukuza uadilifu
na uwajibikaji na kusimama imara kwa vitendo katika mapambano dhidi ya rushwa,
uhujumu wa uchumi na dawa za kulevya, sambamba na kujidhatiti katika
kuvitokomeza vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein aliwataka wananchi kuanza kusherehekea mwaka mpya 2018 kwa kushiriki
kikamilifu katika maadhimisho ya Sherehe za miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar ya tarehe 12 Januari 2018 pamoja na kushiriki katika ufunguzi na
uwekaji wa mawe ya msingi ya miradi mbali mbali ya maendeleo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment