RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amesema kuwa ni jambo la kufurahisha sana kwamba mwaka 2017 unaagwa huku Zanzibar
ikiwa imeweza kuirudisha sifa na heshima iliyokuwepo miaka mingi katika mchezo
wa Mpira wa Miguu.
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika
risala yake ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2018 aliyoitoa kupitia vyombo vya
habari, Ikulu mjini Zanzibar na kusisitiza kuwa Timu ya “Zanzibar Heroes”
imeitangaza vyema Zanzibar katika Mashindano ya Kombe la Chalenji la CECAFA kwa mwaka 2017.
Katika risala yake hiyo, Dk. Shein
alisema kuwa Zanzibar imepata nafasi ya pili baada ya kufika fainali na
kushindwa kwa njia ya penalti ambapo wachezaji wameonesha vipaji na uwezo wa
hali ya juu.
“Wachezaji wetu wameonesha vipaji na
uwezo wa hali ya juu na sisi tumeonesha mapenzi, mshikamano na uzalendo mkubwa
kwa vijana wetu....Tumepata heshima kubwa katika mashindano haya”, alisisitiza
Dk. Shein katika risala hiyo.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa mafanikio
hayo yaliopatikana ni ishara kwamba, juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kufufua michezo zimeanza kuzaa matunda
mazuri.
Hivyo, Dk. Shein alitoa wito kwa
wanamichezo na wananchi wote kushikiana katika kufufua na kuendeleza michezo
hapa nchini.
Kwa mara nyengine tena, Dk. Shein alitoa
pongezi maalum kwa wachezaji na viongozi wa Timu ya “Zanzibar Heroes” kwa
mafanikio makubwa iliyoyapata timu hiyo na kupelekea kuiwakilisha na kuitangaza
vyema Zanzibar kitaifa na kimataifa.
Vile vile, Dk. Shein alitumia fursa hiyo
kutoa pongezi kwa vijana wa “Zanzibar Sand Heroes”(Mashujaa wa Mpira wa
Ufukweni) kwa kufika fainali na kuifunga timu ya Malawi magoli matatu kwa
mawili na kuchukua kikombe cha mashindano hayo.
Dk. Shein alisisitiza kuwa nayo timu hiyo
imeiletea sifa kubwa Zanzibar kwa mara ya kwanza kutokana na ushindi wake huo.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwataka
wananchi kujitokeza kwa wingi katika mashindano maalum ya mpira ya kombe la
Mapinduzi (Mapinduzi Cup) pamoja na Michuano ya “ZBC Watoto Mapinduzi Cup”
ambayo yanazishirikisha timu za watoto wa Wilaya zote za Unguja na Pemba.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwahimiza
wananchi kujitokeza kwa wingi katika Tamasha la nne la maonesho ya biashara
litakaloanza rasmi tarehe 7 hadi 16 Januari 2018 kwenye viwanja vya Maisara.
Dk. Shein pia, aliwataka wananchi
wahakikishe kwamba kila mtu anapata fursa ya kuyaona maonesho hayo huku
akiwataka kujitahidi kuhudhuria katika kilele cha Sherehe za Mapinduzi
zitakazofanyika katika uwanja wa Aman tarehe 12 Januari, 2018.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment