Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein, Azindua ShamraShamra za Sherehe za Mapinduzi Kwa Usafi wa Mazingira Sebleni leo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akimkabidhi Vifaa vya kufanyia Usafi Katibu wa Baraza la Vijana wa Wilaya ya Magharibi B Unguja Farida Juma,wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika eneo la Nyumba za Wazee Sebleni Unguja. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa hakuna mbadala wa usafi hivyo wananchi wote wanapaswa kuwa wasafi wao wenyewe pamoja na mazingira wanayoishi.

Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kushiriki kikamilifu katika uzinduzi wa usafi wa mazingira uliofanyika katika nyumba za wazee Sebleni mjini Zanzibar ikiwa ni mwanzo wa shamrashamra za miaka 54 ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.

Dk. Shein alisema kuwa usafi ukikosekana kuna kila sababu za mwanaadamu ama jamii kupata maradhi na hatimae kupelekea kuathirika na kupata matatizo ya afya ikiwemo kupata maradi ya kipindupindu.

Katika suala zima la usafi, Dk. Shein alisisitiza kuwa mwanaadamu ni usafi hasa katika usafi wa mazingira, sehemu anazoishi, anazokula, kunywa na kuvaa na ndio maana dini zote zinasisitiza suala zima la usafi.

Dk. Shein alieleza haja ya kuendelea kufanya usafi na kusisitiza kuwa usafi huo uwe endelevu na usiwe kwa leo pekee na kwa kila mmoja afanye juhudi katika suala zima la usafi na yule ambaye hawezi kufanya usafi wakiwemo wazee wasaidiwe ili waendelee kuishi maisha bora.

Alisisitiza haja ya wananchi kuungana na Serikali yao ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaenzi na kuwatunza wazee.

Aidha, Dk. Shein alipongeza juhudi za Mkoa wa Mjini Magharibi za kuwapa ajira vijana 3630 ambao watapata nafasi ya kujiongezea kipato chao kupitia fedha zitakazokusanywa kwa huduma za uzoaji taka kutoka nyumba za wananchi na maeneo ya biashara.

Alieleza kufurahishwa na  Mpango Mkakati wa kuimarisha usafi na kupelekea Mkoa wa Mjini Magharibi kuwa safi huku akitilia mkazo kwa wale wote watakaokwenda kinyume  na taratibu zilizowekwa na Mkoa huo ikiwa ni pamoja na adhabu kwa atakaeegesha gari maeneo ya barabarani.

Dk. Shein aliwataka viongozi wa Mkoa kuyashughulikia na kuongeza njia na kutaka Mikoa mengine ije kuiga na kwa vile kila Jumaamosi wameamua kufanya usafi na yeye ametangaza kuwa ameamua kuwa kila Jumaamosi ya mwisho wa mwezi atakutakana na uongozi wa Mkoa wake ili aisikie nini wanafanya katika kila mwezi na kutaka miezi sita wamefanya nini.

Alisikilize utekelezaji waliofikia katika Mpango huo wa kuimarisha usafi na kuendezesha mji  na kumpataka Mkuu wa Mkoa kusimamia yeye na wasaidizi wake kwani sheria na kanuni vyote bvipo na kutaka mpango huo utekelezwe.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwataka wananchi kuwayenzi, kuyaendeleza na kuyapa heshima Mapinduzi ya Januari 12, 1964 kwani ni uhai wa nchi na yameleta Muungano uliopo wa Tanzania kwani hakuna mbadala wake na lazima wawe imara katika kuyatunza na kuyaendeleza ili nchi ipate tija.

Alisema kuwa Zanzibar itajengwa na Wazanzibari wenyewe, na hivi sasa tayari miaka 54 imeshafikiwa huku Zanzibar ikiwa imepiga hatua kubwa sana kutokana na mabadiliko makubwa yaliopatikana ya Maedendleo yanayotokana na Mapinduzi.

Dk. Shein alisisitiza kuwa ni vyema Mapinduzi yatunzwe na yaenziwe na kuendelezwa kwa kuijenga Zanzibar kwa ari na nguvu kubwa ili maendeleo yazidi kupatikana.

Alimpongeza Mkuu wa Mkoa kwa zoezi hilo kufanyika katika eneo la Sebleni lenye historia kubwa huku akieleza maagizo ya Ilani ya ASP yaliotanagzwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ikiwa ni pamoja na afya, elimu sambamba  na kujengwa kwa nyumba za wazee, kwani ilikuwa ni Sera ya ASP iliyowakomboa wananchi wote wa Unguja na Pemba.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza kuwa Serikali ina wajibu wa kuwatendea mema watu wote bila ya ubaguzi kwani Serikali ni ya wote.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mahmoud alieleza kuwa Mpango uliwekwa na Mkoa wake ni mashirikiano ya pamoja kati ya viongozi wa Serikali, Mkoa, Majimbo na Shehia za Mkoa huo.

Nae Katibu Tawala Hamida Mussa Khamis akisoma taarifa ya uzinduzi wa Mpango wa Kuimarisha Usafi na Kupendezesha Mji katika Mkoa wa Mjini Magharibi alisema kuwa Mkoa umepanga kutekeleza Mapngo huo kwa kipindi cha majaribio cha miaka miwili.

Alieleza kuwa lengo ni kuhakikisha mwishoni mwa mwaka 2019 Mkoa wa Mjini Magharibi uwe msafi na wenye mvuto na usiwe hatarishi katika kuchangia kuenea kwa maradhi ya mripuko.

Alieleza matamko yaliyoazimiwa na Mkoa huo ikiwa ni pamoja na kila nyumba italazimika kuchangia fedha za uzoaji wa taka taka ambazo zitachukuliwa kutoka zilizopo na kupelekwa katika eneo lililotengwa kukusanyia taka TZS mia moja kila siku ambazo zitakuwa ni jmla ya TZS elfu 30 kwa mwezi.

Mtu yeyote atakaebainika kutupa taka ovyo, kutema mate na kujisaidia ovyo atawajibika kwa kulipa faini kama zilivyoanishwa katika kanuni za uchafuzi wa mazigira.

Kila mwenye nyumba, ofisi au aneo la bishaara lililopo barabarani analazimika kuweka ‘Interlock’ au bustani ili kuweka haiba nzuri na kila mfanyabiashara anawajibu wa kuweka vyombo maalum vya kutupia taka huku Mkoa ukipanga kuwa kila siku ya Jumaamosi ya kila wiki kuwa ni siku ya usafi kuzia saa 12:00 hadi saa 4:00 asubuhi.

Aliongeza kuwa gari zote zinazolazwa au kuegeshwa katika maeneo ya barabarani hazitaruhusiwa tena na kwamba kuanzia sasa gari zote zitachukuliwa na gari maalum za Manispaa ambapo mhusika atalazimika kulipa fidia ili apewe gari yake.

Hamida aliongeza kuwa Mkoa wa Mjini Magharibi unaweza kuwa Mji wa mfano endapo wananchi wataunga mkono jitihada za Serikali za kuimarisha usafi wa mazingira.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.