Habari za Punde

Balozi Seif afungua Kongamano la Taasisi za Kiraia katika Ukumbi wa Mikutano wa Zanzibar Beach Resort

  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akinunua moja ya bidhaa zilizotengenezwa na Wajasiri amali wa Taasisi za Kiraia kwenye maonyesho Maalum yaliyoandaliwa ndani ya Kongamano la Taasisi za Kiraia linalofanyika katika Ukumbi wa Zanzibar Beach Resort  Mazizini.

Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utawala Bora na Utumishi wa Umma Mh. Haroun Ali Suleiman anayekaimupia Wizara ya Fedha na Mipango na Kushoto ya Balozi ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud.
 Balozi Seif akiridhika na kiwango cha utengenezaji wa Mafuta ya kujipaka ya Asili ya Nazi yaliyosarifiwa na wajasiri amali wa Zanzibar wakati akikagua maonyesho ya Taasisi za Kiraia.

 Mmoja wa Wajasiri Amali wa Taasisi za Kiraia akimpatia maelezo Balozi Seif jinsi wanavyotengeneza bidhaa zao kwa kutumia elimu maalum.

   Mazizini Nje kidogo ya Mji Mji wa Zanzibar.
 Balozi Seif katika picha ya pamoja na Viongozi wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Taasisi za Kiraia mara baada ya kulizindua Kongamano hilo.

Balozi Seif katika picha ya pamoja na Viongozi wa Taasisi za Kiraia na zile za Kiserikali mara baada ya kulizindua Kongamano hilo.

Balozi Seif akiagana na Mwenyekiti wa Kongamano la Taasisi za Kiraia mara baada ya kulizindua rasmi hapo katika Ukuimbi wa Mikutano wa Zanzibar Beach Resort Mazizini Nje kidogo ya Mji Mji wa Zanzibar.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapindiuzi ya Zanzibar inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaoendelea kutolewa na Taasisi za Kiraia katika kuisaidia Serikali na Wananchi kukabiliana na tatizo la umaskini Nchini.

Alisema mchango unaotolewa na Taasisi hizo ni mkubwa na wasimamizi wake wanastahiki kuzidi kushiriki kikamilifu katika kuendelea kuungana na Serikali Kuu katika kusukuma gurudumu la Maendeleo ili liwanufaishe vyema Wananchi pamoja na Taifa kwa jumla.

Akilifungua Kongamano la Pili la Siku mbili la Taasisi za Kiraia linalofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort  Mazizini  Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar ni ya Wananchi wote wakiwemo wanajumuiya ya Kiraia ambao nao wana wajibu wa kuijenga.

Hata hivyo Balozi Seif  alizitahadharisha Taasisi  hizo za Kiraia Nchini  kwamba Serikali  haitokuwa tayari kuziona zinafanya  kazi ambazo ziko nje na kinyume  na Katiba pamoja na Taratibu zilizojipangia zenyewe.

Alisema uzoefu wa majukumu ya Taasisi za Kiraia umetoa mafunzo na mambo mengi na kupelekea baadhi ya Taasisi hizo kukiuka madili. Hivyo Serikali haitokuwa tayari kurejea makosa yaliyojitokeza ya kuziacha Taasisi za Kiraia kufanya zitakavyo bila ya kuzingatia sheria za Nchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia washiriki wa Kongamano hilo la Taasisi za Kiraia Nchini kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  itakua tayari kuyapitia mapendekezo yote watakayoyatoa kwa nia ya kuyafanyia kazi.

Alisema mapendekezo ya wanakongamano hao kwa  imani kubwa yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuimaika kwa Utawala Bora sambamba na jamii kupata nguvu za kupambana dhidi ya Umaskini.

Balozi Seif alielezea matumaini yake kwa Wataalamu watakaoendesha  Kongamano hilo kwamba watazichambua mada zitakazowasilishwa kwa undani kabisa ili kila mshiriki  apate uelewa kwa kutosha.

Aliwataka washiriki wa Kongamano hilo la Taasisi za Kiraia waogelee zaidi kwenye michango yao itakayotoa muelekeo wa kufanikisha lengo lililokusudiwa la kuwepo kwa mkusanyiko huo muhimu wa ushirikishwaji wa Wana Taasisi za Kiraia.

Mapema Mwenyekiti wa Kongamano la Taasisi za Kiraia Dr. Mzuri Issa aliiomba Serikali Kuu kuendelea kuratibu Taasisi za Kiraia kwa lengo la kufanya kazi kwa pamoja ili malengo yaliyokusudiwa katika kuanzishwa kwa Taasisi hizi lifikiwe.

Alisema Wana Jumuiya ya Taasisi za Kiraia wanaendelea kufanya utafiti za umuhimu wa huduma za Kijamii ambazo ndio chimbuko la mafanikio yanayoweza kusukuma kwa haraka maendeleo ya Wananchi.

Dr. Mruzi  alieleza kwamba wanakongamano hao watapata fursa ya kupokea na kujadili mada sita muhimu zilizowazunguuka katika utekelezaji wa majuku yao ya kila siku ambazo ni  hali halisi ya Taasisi za Kiraia Zanzibar, Mkakati wa kupunguza Umaskini Zanzibar Awamu ya Tatu pamoja na Kusaidia Biashara zinazojitokeza kwa Wajasiriamali.

Alizitaja Nyengine ni pamoja na Mtazamo wa Makundii yenye mahitaji Maalum, haki za Watoto na Ulemavu, Nishati mbadala kwa Zanzibar  pamoja na ile ya Utafutaji wa Rasilmali kwa Jumuiya zisizo za Kiserikali.

Akimkaribisha Mgeni ulifungua Kongamano hilo Kaimu Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar  Mh. Haroun Ali Suleiman alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya {EU} imeanzisha Mradi Maalum wa kuzizaidia Taasisi za Kiraia Nchini ili zifanye kazi zake kwa ufanisi.

Mh. Haroun alisema Mradi huo wenye kutekelezwa kwa mfumo wa Mkataba uliotengewa takriban fedha Euro Milioni Tatu umekusudiwa kuimarisha sheria pamoja na Utawala Bora kupitia Taasisi hizo.

Waziri Haroun ambae ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utawala Bora na Utumishi wa Umma alisema matarajio ya Mradi huo ni kuimarika kwa Taasisi za Kiraia pamoja na kuibua maeneo mapya.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.