Habari za Punde

Balozi Seif: Serikali haitomuonea huruma mtu yeyote akijenga sehemu bila ruhusa

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akitembelea Majengo ya Mradi wa Chuo cha Marekebisho ya Watu walioathirika na Dawa za Kulevya yaliyopo Kidimni Wilaya ya Kati

Kulia ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga  na  Kushoto ya Balozi ni Katibu Mkuu Ofisi hiyo Dr. Idriss Muslim Hijja na Mshauri Muelekezi wa MrADI HUO Nd. Mbwana Bakari Juma.
  Mshauri Muelekezi wa Ujenzi wa Mradi wa Chuo cha Marekebisho ya Watu walioathirika na Dawa za Kulevya Kidimni Nd. Mbwana Bakari Juma aliyesisima akimuonyesha Ramani ya MAJENGO Balozi Seif aliyefika kukagua hatua iliyofikiwa.

 Mkurugenzi Utumishi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Bibi Halima Ramadhan Toufiq  akitoa ufafanuzi ya gharama za Ujenzi wa Mradi huo kwa Balozi Seif.

Mkurugenzi Tiba Wizara ya Afya Dr. Mohamed Dahoma aliyeshika kipaza sauti akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyefika Binguni kuangalia eneo linalotarajiwa kujengwa Hoispitali Kubwa ya Rufaa Zanzibar.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis , OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameonya na  kusisitiza kwamba  Serikali haitomuonea  huruma Mtu ye yote atakayeamua kujenga Nyumba au jengo lolote katika eneo lisilopata ridhaa ya Taasisi inayohusika na masuala ya Ujenzi, Ardhi, Mipango Miji na Vijiji.

Alisema hivi sasa ipo tabia ya muhali inayoonekana kuendelea kufanywa na baadhi ya Viongozi wanaopewa jukumu la kusimamia Sheria na Taratibu za Serikali kiasi kwamba watu huamua kuchukuwa sheria mikononi mwao.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo wakati alipofanya ziara ya kukagua eneo ambalo Serikali kuu inatarajia kujenga Hospitali Kubwa ya Rufaa katika Kijiji cha Binguni Wilaya ya Kati Mkoa Kusini Unguja.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshaamua kudhibiti wimbi la ujenzi holela katika maeneo mbali mbali hasa yale yaliyotengwa kwa ajili ya Kilimo na Miradi mengine ya Maendeleo.

Balozi Seif  aliuagiza Uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar kuhakikisha kwamba eneo hilo lililotengwa na Serikali kwa ajili ya Ujenzi wa Mradi Mkubwa wa Hospitali linakuwa katika udhibiti unaostahiki.

Akitoa maelezo ya eneo hilo Mkurugenzi Idara ya Tiba Dr. Mohamed Dahoma alisema eneo hilo lenye ukubwa wa Hekta 83 hivi sasa liko kwenye udhibiti wa Wizara ya Afya kwa ajili ya mpango wa baadae wa Ujenzi wa Hospitali Kubwa ya Rufaa.

Dr. Dahoma alimueleza Balozi Seif  kwamba Wizara ya Afya kupitia wataalamu wa uchambuzi yakinifu inaendelea na uhakiki wa eneo hilo kwa lengo la kufanya michoro itakayotoa muelekeo mzima wa uendelezaji wa mradi huo utakavyokuwa.

Alisema Mradi huo mkubwa utakaokwenda kwa Awamu Tatu umepangwa kuwa na Kitengo cha Mafunzo, Hospitali ya kulazwa Wagonjwa baina  ya Mia Mbili na Mia Tatu, Nyumba za Wafanyakazi pamoja na Majengo ya Utawala.

Mkurugenzi Tiba wa Wizara ya Afya alifafanua kwamba Majengo yaliyokuwemo ndani ya Eneo hilo hapo awali  yalikuwa ya Taasisi ya African Muslim Agency kwa ajili ya ujenzi wa Skuli lakini Serikali iliamua kulichukuwa eneo hilo kwa ajili ya Mradi mkubwa zaidi wa Kijamii Nchini.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitembelea Majengo ya kitakachokuwa Chuo cha Marekebisho ya Watu walioathirika na Dawa ya Kulevya { Sober House } liliopo katika Kiji cha Kidimni Wilaya ya Kati.

Mshauri Muelekezi wa Mradi huo Nd.  Mbwana Bakar Juma alimueleza Balozi Seif  kwamba mradi huo tayari umeshakamilika katika Awamu ya kwanza kwa uwepo wa Ofisi, Jiko pamoja na Bweni la kulala Waathirika hao.

 Bwana Bakar alisema Mkandarasi wa Ujenzi huo Kampuni ya Kizalendo ya Al – Hilal General Traders licha ya mradi huo tayari  kuukabidhi Serikalini lakini hivi sasa Wahandisi wake wanaendelea kufanya uhakiki wa maeneo ambayo yana hitilafu yoyote ili kuyafanyia marekebisho.

Mshauri Muelekezi huyo alifahamisha kwamba Majengo hayo yatakapokamilika kabisa yatakuwa na sehemu za Kilimo, Karakana ya Mafunzo ya Ujasiri amali, Wafanyakazi pamoja na eneo la michezo kwa Vijana watakaokuwa wakiishi sehemu hiyo.

Naye Mkurugenzi Utumishi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Bibi Halima Ramadhan Toufiq alisema Mradi huo hadi hivi sasa tayari umeshagharimu Jumla ya Shilingi za Kitanzania Milioni Mia 6.9 katika hatua ya Awamu ya Kwanza.

Bibi Halima alisema awamu ya Pili unaotarajiwa kugharimu jumla ya shilingi Bilioni Nne za Kitanzania utaongezwa ghorofa katika Ofisi ya Utawala na Majengo mengine pamoja na kutengenezwa miundombinu ya Maeneo ya kilimo na viwanja vya Michezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.