RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesema kuwa mazoezi ni kinga na tiba mbadala ya maradhi
mbali mbali yanayoisumbua jamii katika maisha ya kila siku hivyo kufanya
mazoezi kunapunguza uwezekano wa kupata maradhi.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa
katika maadhimisho ya siku ya mazoezi Kitaifa yaliyovishirikisha vikundi
mbali mbali vya mazoezi kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara pamoja na vikosi
vya SMZ yaliyoanzia katika uwanja wa Tumbaku na kuishia katika uwanja wa Amaan
mjini Zanzibar yaliosimamiwa na Chama Cha Mazoezi ya Viungo Zanzibar (ZABESA).
Viongozi mbali mbali walishiriki katika maadhimisho hayo
akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na
viongozi wengine wa Seriali na vyama vya siasa na wananchi ambapo katika
maelezo yake Dk. Shein alisisitiza kuwa kufanya mazoezi kunasaidia kupunguza
uzito wa mwili na kuwataka wananchi kufanya mazoezi na kutosubiri hadi
wakaambiwa na daktari.
Dk. Shein
aliwasisitiza wananchi kuzingatia usemi maarufu wa mabingwa wa lugha ya
kiswahili kwamba “Tahadhari kabla ya athari” na “Kinga ni bora kuliko tiba”,
hivyo alisisitiza ni vyema kila mmoja akajiwekea muda maalum wa kufanya mazoezi
yanayolingana na afya na umri wake.
Pia, Dk. Shein
alitangaza rasmin kuwa maadhimisho hayo ya Siku ya Mazoezi Kitaifa hapo mwakani
yatafanyika Kisiwani Pemba huku akiitaka Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo kukitafutia
ofisi Chama Cha Mazoezi ya Viungo Zanzibar (ZABESA) ili kiweze kufanya kazi
zake kwa ufanisi zaidi.
Aidha, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kwa mara nyengine tena kuipongeza timu ya “Zanzibar Heroes”
kwa kufikia hatua ambayo haijawahi kufikiwa tangu mwaka 1995, ilipopata ubingwa
wa mashindano Kombe la Chalenji la
CECAFA huku akiahidi kuwa mashindano yajayo popote pale
yatakapofanyika timu hiyo itachukua ubingwa.
Pia, alitoa pongezi
kwa vijana wa “Zanzibar Sand Heroes”(Mashujaa wa Mpira wa Ufukweni) kwa kufika
fainali na kuifunga timu ya Malawi magoli matatu kwa mawili na kuchukua kikombe
cha mashindano hayo. Pia, aliyapongeza mashindano ya “ZBC Watoto Mapinduzi Cup”
yanayozishirikisha timu za watoto kutoka Wilaya zote za Unguja na Pemba.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alieleza azma ya Serikali hadi kufikia mwaka 2020 kumaliza viwanja vitano
katika Wilaya za Unguja na Pemba kikiwemo kiwanja cha Kitogani ambacho ujenzi
wake unaendelea huku akieleza hatua nzuri za ujenzi zinazoendelea katika uwanja
wa Mao Tse-Tung.
Akitoa maelezo juu ya
Mashindano ya “Mapinduzi Cup” yanayoendelea, Dk. Shein aliitaka Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na
Michezo kupunguza fedha za viingilio katika mashidnano hayo yanayofanyika
katika uwanja wa Amaan ili wananchi wote wapate kuyaona kwani mashindano hayo
ni ya Serikali na sio ya ZFA bali wao ni wasimamizi tu, hivyo wananchi
wanafursa ya kuyaangalia kwa fedha wanazozimudu.
Dk. Shein alieleza kuwa
mashindano ya “Mapinduzi Cup” hayana
mbadala na kuwaeleza wale wote wanaobeza Mapinduzi wajue kuwa na wao wanabezwa
kwani Mapinduzi yaliwagomboa watu wote na yamemnufaisha kila mtu na yataendelea
kuwa Mapinduzi, hivyo wanaoendesha mashindano hayo ni vyema wakatambua hilo.
“Hatuna mbadala na
Mapinduzi yetu, tutayaenzi Mapinduzi yetu tutayaendeleza Mapinduzi yetu,
tutayaenzi Mapinduzi yetu na wale wote wanaoyabeza Mapinduzi yetu na sisi tunawabeza
hivyo hivyo”,alisisitiza Dk. Shein.
Pia, Dk. Shein aliiagiza
Wizara hiyo kufikiria eneo jipya la kuanzia mazoezi hayo hadi kuishia katika
viwanja vya Mao Tse Tung huku akiitaka ZFA kufikiria kuanzisha mashindano ya
ZFA yatakayofanyika kwa njia ya kutoana yaana ‘knock out” yatakayoandaliwa kwa
kuzishrikisha timu za madaraja yote kama yalivyokuwa zamani na yanayofanyika
kwenye nchi mbali mbali.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alieleza kuwa licha ya mafanikio yanayoendelea kupatikana katika
kuimarisha sekta ya michezo hapa nchini bado jitihada za ziada zinahitajika kwa
ajili ya kuimarisha Ligi Kuu ya Mpira wa Miguu ya Zanzibar ligi yake imekosa
msisimko kutokana na kutotangazwa katika vyombo vya habari.
Hivyo, aliiagiza
Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo iuelekeze uongozi wa Gazeti la ‘Zanzibar
Leo’ uandae utaratibu ili kila siku wasomaji wapate kuuona msimamo wa ligi kuu
ya Zanzibar pamoja na kuchapisha orodha ya mechi zinazochezwa kwa wiki nzima,
ili kuwavutia wananchi kwenda viwanjani.
Nae Waziri wa Habari,
Utalii, Utamaduni na Michezo Rashid Ali Juma alimpongeza Dk. Shein kwa
kuendeleleza sekta ya michezo hapa nchini na juhudi zake katika kulifanikisha
tamasha hilo na kutumia fursa hiyo kuwapongeza wale wote waliounga mkono na kufanikisha
maadhimisho ya tamasha hilo la mwaka huu.
Mapema Kamishna wa
Michezo Sharifa Khamis alisema kuwa huu ni mwaka wa tano tokea Dk. Shein
ayatangaze rasmin maadhimisho ya siku hiyo ya Kitaifa ya michezo na tokea mwaka
huo yamekuwa yakienda vizuri huku akimpongeza Dk. Shein kwa zawadi
alizoizawadia timu na viongozi wa timu ya “Zanzibar Heroes”.
Katika risala yao nao
Wafanya Mazoezi ya Viungo walieleza kuwa
kufanya mazoezi ni njia moja ya kukuza uchumi wa Taifa ikiwa ni pamoja na
kupunguza kununua dawa na fedha hizo kuzielekeza kwenye kuiletea maendeleo nchi
yao.
Sambamba na hayo, walimpongeza
Rais Dk. Shein kwa juhudi zake za kuiinua Zanzibar kimaendeleo hasa katika sekta ya michezo,
elimu, afya, kilimo, mawasiliano na miundombinu pamoja na sekta nyenginezo huku
kaulimbiu ya Tamasha hilo mwaka huu ikiwani “Fanya mazoezi kwa maendeleo yako
na Taifa lako”.
Walieleza kuwa hivi
sasa kumekuwa na taasisi mbali mbali ambazo kwa kuimarisha na kuhamasisha
ufanyaji wa mazoezi wamekuwa wakihamasisha wafanyakazi wao kufanya mazoezi
pamoja na kuwepo taasisi zinazofanya utaratibu wa kupima afya za wafanyakazi
wao kwa kuwasogezea karibu huduma za upimaji wa afya.
Mapema Dk. Shein, alipokea
maandamano ya vikundi vya mazoezi kutoka ndani na nje ya Zanzibar vilivyowashirikisha
vijana, wazee, watoto, wanawake na wanaume pamoja na walemavu na kuonesha
mazoezi mepesi kiwanjani hapo pamoja na mashindano kwa wenye uzito wa zaidi ya
kilo mia moja na baadae alitoa vyeti maalum kwa vikundi vya mazoezi
vilivyoshiriki Tamasha hilo huku Balozi Seif Ali Idd akitoa vyeti maalum kwa waliochangia
kufanikisha Tamasha hilo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment