Habari za Punde

Makamu Mwenyekiti UWT awatembelea viongozi wa zamani wa Jumuiya kupata busara zao

Na Is-haka Omar, Zanzibar.

MAKAMU Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania wa Chama Cha Mapinduzi(UWT),Thuwayba Kisasi, amewaomba viongozi wa zamani wa jumuiya hiyo kuendelea kutoa maoni na ushauri utakosaidia kuimarisha taasisio hiyo kisiasa, kiutendaji na kiuongozi.

Ombi hilo amelitoa leo kwa wakati tofauti alipowatembelea viongozi wa zamani wa jumuiya hiyo kwa lengo la kupata ushauri unaotokana na uzoefu wao wa kisiasa na kiutendaji  wa viongozi hao wa zamani waliowahi kuiongoza taasisi hiyo kwa awamu tofauti.

 Viongozi waliotembelewa ni pamoja na  Bi. Fatma Mbarouk, Bi. Fatuma Theresa,  Bi. Asha Mwinyi, Bi. Salma Yusuph, Bi. Mwantantu Yusuph Shaaly  pamoja na Bi. Johari Yusuph Khatib.

Akizungumza baada ya kuwatembelea Makamu Mwenyekiti huyo alisema bado jumuiya hiyo inathamini juhudi za viongozi na watendaji hao  waliowahi kuongoza taasisi hiyo kwa mafanikio makubwa.

Makamu huyo aliongeza kuwa licha ya kupata michango yao ya maoni katika namna ya kuendesha jumuiya pia nifaraja kuwatembelea kwa lengo la kuwajulia hali na kwamba nao wanahisi  faraja.

Katika maelezo yake Thuwayba aliongeza kuwa haitaishia hapo kuwatembelea viongozi hao wa jumuiya hiyo ambapo UWT itaendelea kuwawekea kipaumbele bila kuchoka.

"Nimejifunza mengi kutoka kwa viongozi wetu wastaafu na wametushauri kuwa tuendelee  kushikamana, tupendane na kufanya kazi zetu kwa bidii.,"alifafanua  Makamu huyo.

Aliongeza kuwa viongozi hao wameshauri jumuiya hiyo iwe na Umoja, nguvu na kutoyumba kwa namna moja ama nyingine na kwamba kufanya hivyo UWT itakuwa imara.

Naye miongoni mwa viongozi hao waliotembelewa Johari Yusuph Khatib, aliwataka UWT kuwa karibu na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali zote mbili kwa lengo la kupata uzoefu mbali mbali wa masuala ya uongozi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.