Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein akutana na kufanya mazungumzo na Mtukufu Sheikh Mohammed bin Rashid Al Makhtoum



STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Dubai                                                                  24.01.2018
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amekutana na kufanya mazungumzo na Mtukufu Sheikh Mohammed bin Rashid Al Makhtoum, Makamo wa Rais na Waziri Mkuu wa nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Mtawala wa Dubai ambapo viongozi hao wameahidi kushirikiana katika sekta mbali mbali za maendeleo zikiwemo za biashara, uwekezaji na utalii.

Viongozi hao walifanya mazungumzo hayo katika ukumbi wa Makaazi ya Sheikh Mohammed bin Rashid, mjini Dubai, ikiwa ni muendelezo wa ziara ya Dk. Shein katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Katika maelezo yao viongozi hao walieleza azma yao ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu ambao ni wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania ikiwemo Zanzibar na Dubai.

Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Zanzibar katika kuhakikisha sekta ya utalii inazidi kuimarika sambamba na ongezeko la watalii hivi sasa pamoja na malengo yaliyowekwa na Serikali katika kufikia watalii laki tano mnamo mwaka 2020, malengo ambayo yanaweza kufikiwa kabla ya mwaka huo kutokana na ongezeko la watalii kila uchao.

Aidha, Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo vivutio kadhaa vya asili vilivyopo Zanzibar vikiwemo Mji Mkongwe wa kihistoria, fukwe za bahari, viungo, utamaduni na silka za Wazanzibari, mazingira, ukarimu pamoja na mambo mengineyo bila ya kusahau amani na utulivu mkubwa uliopo ambao ndio chachu ya kuimarisha sekta ya Utalii Zanzibar.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo mikakati iliyowekwa katika kuhakikisha sekta hiyo inaimarika zaidi hasa katika kuendeleza sekta hiyo kwa sayansi na teknolojia iliyopo jambo ambalo bado linataka kuungwa mkono ili liweze kuleta tija.

Pia, Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika kuimarisha sekta ya uwekezaji na biashara hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar ina historia kubwa ya kibiashara kati yake na nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ikiwemo Dubai huku akisisitiza haja kwa Kampuni ya ndege ya “Emirate” kufanya safari kati ya Dubai na Zanzibar ili kuzidi kuimarisha sekta hizo.

Nae Sheikh Mohammed bin Rashid Al Makhtoum alimuhakikishiaDk. Shein kuwa atahakikisha juhudi za makusudi zinachukuliwakatika kuhakikisha uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu ulipo kati ya pande mbili hizo unaimarishwa.

Aidha, kiongozi huyo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa nchi yake inathamini uhusiano na ushirikiano uliopo na kuahidi kuuendeleza kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo ikiwemo utalii, uwekezaji na biashara.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya ndege ya Emirate Sheikh Ahmed Bin Saeed Al Makhtoum alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Kampuni ya ndege ya “Fly Dubai” chini itazidi kuonngeza safari zake kati ya Zanzibar na Dubai.   

Wakati huo huo, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wawekezaji na Wenyeviwanda wa Dubai na kuwakaribisha huku akiwataka kuendelea kuekeza Zanzibar na kueleza kuwa Jumuiya hiyo imeundwa na wanachama wenye uzoefu mkubwa katika sekta ya biashara, viwanda, utalii na uwekezaji ambapo mchango wao umeifanya Dubai kupata maendeleo ya haraka ambayo ni mfano duniani kote.

Hivyo, kwa kutunia uzoefu walionao, Dk. Shein aliwataka wawekezaji hao wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, wawekezaji na wenye viwanda wa Dubai kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar katika sekta zote za uwekezaji zilizopo.

Dk. Shein aliwahakikishia kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla zina usalama na amani ya kutosha jambo ambalo limekuwa ni chachu ya maendeleo yanayoendelea kupatikana hivi sasa.

Aidha, Dk. Shein aliwaeleza mipango ya Serikali ya kuhakikisha kuwa rasilimali za wawekezaji zinaleindwa kutokana na kutunga sheria mbali mbali zenye lengo la kuimarisha uwekezaji pamoja na kulinda rasilimali za wawekezaji.

Baada ya kusema hayo, Dk. Shein alimkaribisha Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji, Vitega Uvhumi Zanzibar (ZIPA), Salum Khamis Nassor kutoka maelezo na ufafanuzi juu ya fursa na mikakati ya Serikali pamoja na Sheria zilizopo katika nyanja mbali mbali za uwekezaji.

Aidha, alitoa ufafanuzi juu ya masuala mbali mbali yaliyoulizwa na wanachama wa Jumuiya ambao nao kwa upande wao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jumiya hiyo Majid Saif Al Ghurair ambaye alitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa kwenda kukutana nao na kumuhakikikishia kwamba Jumuiya yake itaandaa mikakati maalum itakayowawezesha kuzifahamu na kuzitumia fursa za wawekezaji zilizopo Zanzibar.

Mapema, Dk. Shein alitembelea na kuona jinsi Bandari ya Jebel Ali inavyoendeshwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa na kuifanya kuwa ni miongoni mwa Bandari yenye  ufanisi wa hali ya juu duniani

Dk. Shein alipata maelezo kutoka kwa uongozi wa Bandari hiyo kwa jinsi inavyofanya kazi na kuelezwa maslahi ya wafanyakazi, juu ya usalama wa bandari pamoja na mipango iliyowekwa kayika kuhakikisha mizigo yote inatolewa salama na kwa wakati muwafaka kwa kutumia teknolojiaya kisasa.

Katika ziara yake hiyo, Dk. Shein alipendezewa na taarifa zilizotolewa na viongozi wa Bandari hiyo juu ya mikakati ya utoaji wa mafunzo, kulinda na kuimarisha maslahi ya wafanyakazi pamoja na mipango ya baadae iliyowekwa katika kuhakikisha sekta ya usafiri na usafirishaji mizigo inaimarika.

Aidha, Dk. Shein alitembelea mradi wa mji mpya wa kisasa wa Nakheel pamoja na Mradi wa Palm Jumeirah na kupata fursa ya kuona jinsi unavyoendeshwa na kuutembea huku akipataa maelezo juu ya hatua zilizofikiwa katika mradi huo ikiwa ni pamoja na ufukiaji mkubwa wa bahari uliofanyika na kueleza historia pamoja na jinsi sekta ya utalii na biashara zilivyoimarika katika eneo hilo.

Pia. Dk. Shein alipata maeleza juu ya uendelezaji sambamba na hatua zilizochukuliwa katika kuuimarisha mji wa Dubai tokea miaka ya 1950 pamoja na azma ya ujenzi wa mji mpya wa kisasa wa Nakheel na Mradi wa Palm Jumeirah ambao ni maarufu kwa utalii, uwekezai na biashara kutokana na eneo hilo kuwa na nyumba za kuishi za kisasa, hoteli, sehemu za kibiashara, burudani na za mapumziko.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.