Habari za Punde

Serikali hushughulikia watoto bila kujali umri wao

Na.Takdir Ali. Maelezo Zanzibar.                               
NAIBU  Waziri wa Wizara ya Kazi,Uwezeshaji,Vijana,Wanawake na Watoto Mh.Shadya Muhammed Suleiman amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inashughulikia watoto kama wanavyotambulika kisheria bila ya kuangalia kigezo cha umri alivyonavyo.
Ameyasema hayo huko Baraza la Wawakilishi Chukwani wakati alipokuwa akijibu suala la mwakilishi wa jimbo la Chake chake Suleiman Farhan Saidi alitaka kujuwa serikali haioni umuhimu wa kubadilisha umri wa mtoto wa miaka saba kwa vile bado hajajitambua.
Amefafanua kuwa Wizara inashughulikia masuala ya watoto mara zote huangalia kwanza maslahi bora kwa mtoto husika kwani serikali haijaweka kigezo cha umri katika kuweka miongozo,sera na sheria zake.
Aidha amesema Serikali imeweka misingi hiyo kwa kuzingatia mila na desturi za jamii yetu sambamba na mikataba na miongozo ya kimataifa inayohusiana na watoto ambapo na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kama ni sehemu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  imeridhia na inatekeleza.
Ameweka wazi ya kuwa umri wa miaka saba sio kigezo ambacho Wizara inakitumia katika kuamua masuala yote yanayohusu ustawi pamoja na maslahi bora ya mtoto ikiwa ni suala la ulezi,matunzo,ukaazi au vyenginevyo.
Shadya amesema kuwa Sheria ya watoto nambar 6 ya mwaka 2011,haikuweka umri wa miaka saba,kwa mujibu wa sheria hiyo,utaratibu uliowekwa katika kushughulikia masuala ya mtoto ni kuzingatia maslahi bora ya mtoto husika na sio kwa kutazama umri wake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.