Habari za Punde

ZURA Yatangaza Bei Mpya ya Mafuta Zanzibar.

Khuzaimat Bakari Kheir kwa Niaba ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ,Nishati na Maji Zanzibar (ZURA) akizungumza na waandishi wa habari huko Ofisi Maisara juu ya mabadiliko ya bei za mafuta ambazo zitaanza kutumika hapo kesho.(Picha na Kijakazi Abdalla   Maelezo Zanzibar.)
Na Kijakazi Abdalla       Maelezo     

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma, Nishati na Maji Zanzibar (ZURA) imesema kuwa bei ya mafuta ya Petroli na mafuta ya taa imepanda kwa mwezi wa Febuari.
Akizungumza na Waandishi wa habari huko Ofisi Maisara,kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma, Nishati na Maji (ZURA) Khuzaimat Bakari Kheir wakati akitoa taarifa juu ya mabadiliko ya bei za mafuta ambazo zitaanza kutumika hapo kesho Jumanne 13/02/2018.
Alisema kuwa Zura imepanga bei kwa kuzingatia mambo yafuatayo ikiwa ni wastani wa mabadiliko ya bei za mafuta Duniani katika mwezi wa Januari 2018,thamani ya shilingi ya Tanzania,Gharama za usafiri,Bima,kodi za Serikali pamoja na kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja.
Aidha alisema kuwa Bei ya Petroli imepanda kwa mwezi wa Febuari kwa shilingi 26 kwa lita kutoka shilingi 2,230 mwezi wa Januari 2018 hadi shilingi 2,256 kwa lita mwezi wa Febuari 2018 sawa na ongezeko la asilimia 1.1
Alisema  kuwa mafuta ya Dizeli kwa mwezi wa Febuari imeshuka kwa shilingi 15 kwa lita kutoka shilingi 2,190 kwa lita katika mwezi Januari 2018hadi shilingi 1619 kwa lita katika mwezi Januari hadi shilingi 1,641 katika mwezi Febuari sawa na asilimia 1.35.
Hata hivyo  Khuzaimat alisema kuwa mafuta ya taa yamepanda kwa shilingi 25 kwa lita kutoka shilingi 1619 kwa lita kwa mwezi wa Januari 2018 hadi shilingi 1,641 kwa mwezi wa Febuari 2018 sawa na ongezeko la asilimia 1.35
Aidha alisema kuwa Mafuta ya Banka kwa mwezi wa Febuari yameshuka kwa shilingi 15 kwa lita kutoka shilingi 2032 kwa lita katika mwezi wa Januari 2018 hadi shilingi 2,017 kwa mwezi wa Febuari 2018 sawa na asilimia 1.
Sambamba na hayo alisema kuwa zoezi la ukaguzi wa kubaini uchakachuaji wa mafuta utaendelea ikiwa na lengo la kuzuia magendo ya mafuta  na kuhakikisha ubora wa bidhaa hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.