MAELEZO YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB) AKIWASILISHA MAPENDEKEZO YA
SERIKALI YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA
NA YA KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI YA
SERIKALI KWA MWAKA 2018/19
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA FEDHA NA MPANGO
MACHI, 2018
MAELEZO YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT.
PHILIP I. MPANGO (MB) AKIWASILISHA MAPENDEKEZO YA
SERIKALI YA MPANGO WA MAENDELEO
WA TAIFA NA YA KIWANGO NA UKOMO
WA BAJETI YA SERIKALI KWA
MWAKA 2018/19
UTANGULIZI
1.Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea
kutujalia uhai na afya. Aidha, tunamshukuru kwa kutuwezesha kukutana tena hapa
mjini Dodoma, kupokea mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa
na Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19, kwa mujibu wa
Kanuni ya 97 ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Januari 2016.
2.Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge
wote kwa kuteuliwa kwao kuwa wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kuanzia sasa.
Aidha, niwapongeze Wenyeviti wote na Makamu wao ambao wamechaguliwa kushika
dhamana ya kuziongoza Kamati hizo. Ni matumaini yangu kuwa Waheshimiwa Wabunge katika nafasi zenu
kwenye Kamati, bila kujali itikadi, mtaisaidia kuishauri Serikali ipasavyo
katika kuijenga nchi yetu kwa manufaa ya Watanzania wote.
3.Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muhtasari, matokeo ya utekelezaji wa Mpango na
Bajeti katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja
na: nchi yetu kuendelea kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi ya wastani wa
asilimia 7.0 kwa mwaka ambayo inatafsiri Pato la wastani la kila mtu kuwa shilingi
2,131,299 mwaka 2016 kutoka shilingi 1,918,930.9 mwaka 2015; kupungua kwa mfumuko
wa bei kufikia asilimia 4.1 Februari 2018; kuongezeka kwa mapato ya ndani
kufikia wastani wa shilingi trilioni 1.3 kwa mwezi kutoka wastani wa shilingi
bilioni 850; kuimarika kwa utoaji wa huduma za jamii hususan elimu msingi bila
ada, kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za afya katika vituo vya kutolea
huduma kwa ngazi zote ikiwemo huduma za matibabu ya kibingwa, kuimarika
usambazaji wa maji mijini (kufikia wastani wa asilimia 78) na vijijini (wastani
wa asilimi 55.5), umeme mijini na vijijini kufikia wastani wa uunganishaji wa
asilimia 67.5 kitaifa na kuweka mazingira wezeshi kwa ujenzi wa viwanda ambapo
viwanda vipya 3,306 vimejengwa.
4.Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mpango na Bajeti ya mwaka 2018/19 ni mwendelezo
wa utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano, shughuli na
miradi mingi iliyopangwa kutekelezwa ni ile ambayo haijakamilika na hivyo
utekelezaji wake utaendelea katika mwaka ujao wa fedha. Aidha, maeneo mengine
yaliyozingatiwa ni yale yatakayoongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango na kutoa
majibu endelevu kwa kero na mahitaji ya msingi ya wananchi walio wengi.
5.Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/19 vimeweka mkazo katika
kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini na kuimarisha uzalishaji,
tija na uhakika wa masoko kwa sekta pana ya kilimo (ikijumuisha uzalishaji wa
mazao, mifugo na bidhaa za mifugo, uvuvi na misitu) kuwezesha upatikanaji wa
chakula na malighafi za kutosha kwa uzalishaji viwandani na ongezeko la idadi
ya watu. Msukumo pia umewekwa katika kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi unakuwa jumuishi.
Katika hili, msukumo umewekwa katika kuendeleza ujenzi wa miundombinu wezeshi
katika sekta za uchukuzi, usafirishaji, nishati, kilimo na mawasiliano; na
uboreshaji wa sekta ya huduma za fedha. Katika kulinda tunu kuu za Watanzania, yaani
amani na umoja, msukumo umewekwa pia katika kuimarisha ulinzi na usalama,
upatikanaji wa haki, utawala wa sheria na utawala bora na upatikanaji wa huduma
za msingi kwa ustawi wa jamii.
6. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla, utayarishaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa
wa Mwaka 2018/19 umezingatia: azma ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025; sera na malengo ya kisekta; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka
2015-2020; makubaliano ya kikanda (EAC na SADC); Ajenda 2063 ya Maendeleo ya
Afrika; na Ajenda ya Dunia ya Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030. Aidha,
umezingatia mapitio ya hali ya uchumi kwa mwaka 2017 na mwelekeo kwa mwaka 2018
kitaifa, kikanda na Dunia na hali halisi ya utekelezaji wa Mpango wa mwaka
2017/18 hadi Februari, 2018.
7.Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii ina sehemu kuu tatu: Sehemu ya kwanza inatoa
tathmini ya mwenendo wa uchumi na ustawi wa Jamii; Sehemu ya pili inaelezea
Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa ya mwaka 2018/19; na Sehemu
ya tatu ni mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya 2017/18 na mapendekezo ya
kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19.
SEHEMU
YA KWANZA
TATHMINI
YA MWENENDO WA UCHUMI NA USTAWI WA JAMII KWA MWAKA 2017
8.Mheshimiwa Mwenyekiti, Uchumi wa nchi yetu umeendelea kushamiri katika viashiria
vingi. Katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba 2017, Uchumi ulikua kwa
kiwango cha wastani wa asilimia 6.8, kiwango ambacho kilikuwa cha juu zaidi ikilinganishwa
na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki: Kenya (asilimia 6.1), Rwanda
(asilimia 6.0), Uganda (asilimia 5.5), Burundi (asilimia 0.0) na Sudani Kusini (asilimia
hasi 6.3). Kwa kulinganisha na nchi zote za bara la Afrika, kasi ya ukuaji wa
uchumi wa Tanzania ulikuwa wa tatu baada ya Ethiopia (asilimia 8.2) na Ivory
Coast (asilimia 7.6).
9.Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiasi kikubwa, ukuaji huu ulichangiwa na ongezeko la shughuli
za: Uchimbaji Madini na Mawe (asilimia 20.3); Habari na Mawasiliano (asilimia
13.1); Usafirishaji na Hifadhi ya Mizigo (asilimia 11.9); Uzalishaji Viwandani
(asilimia 9.8); na Ujenzi (asilimia 9.5). Ukuaji wa sekta ya kilimo ulikuwa asilimia
3.3 katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2017 ikilinganishwa na asilimia
2.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Kwa kuzingatia umuhimu wa sekta ya
kilimo kwa maisha na uchumi wa wananchi wengi, Serikali kupitia mpango huu, itaendelea
kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji, upatikanaji wa pembejeo za kilimo,
huduma za ugani, na maghala ya kuhifadhi mazao na upatikanaji wa masoko. Msukumo
pia umewekwa katika kufungamanisha sekta ya kilimo na sekta ya viwanda kwa
lengo la kuongeza thamani na faida ya shughuli za kilimo.
10.Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mwaka 2017, mwenendo wa mfumuko wa bei ulikuwa tulivu kutokana na kuimarika kwa upatikanaji
wa chakula nchini, utulivu wa bei za nishati hasa mafuta katika soko la ndani
na nje ya nchi na usimamizi thabiti wa sera za fedha na za bajeti. Hadi kufikia
mwishoni mwa mwaka 2017 mfumuko wa bei ulikuwa wastani wa asilimia 5.3 na
umeendelea kupungua na kufikia asilimia 4.1 mwezi Februari, 2018.
11. Mheshimiwa
Mwenyekiti, Akiba ya fedha za kigeni katika kipindi
kinachoishia Desemba 2017, ilifikia Dola za Marekani milioni 5,906.2
ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 4,325.6 katika kipindi kama hicho
mwaka 2016. Kiasi hicho kilichofikiwa mwezi Desemba 2017 kilikuwa kinatosheleza
kugharamia ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 6.0 na hivyo kuzidi
kiwango cha angalau miezi 4.5 kilichowekwa kukidhi matakwa ya hatua za
mtangamano wa Umoja wa Fedha kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
12. Mheshimiwa
Mwenyekiti,
katika kipindi cha mwaka ulioishia Desemba 2017, mwenendo wa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi
ya dola ya Marekani uliendelea kuwa wa kuridhisha. Katika kipindi cha mwezi
Desemba 2017, Dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi
2,230.1 ikilinganishwa na wastani wa shilingi 2,172.6 katika kipindi kama hicho
mwaka 2016, ikiwa ni tofauti ya wastani wa shilingi 57.4. Mwenendo huu
ulitokana na kuboreshwa kwa usimamizi, pamoja na utekelezaji wa sera thabiti za
bajeti na fedha (prudent fiscal and monetary policies) sanjari na mwenendo
mzuri wa urari wa mapato ya fedha za kigeni.
13. Mheshimiwa Mwenyekiti,
katika kipindi cha mwaka unaoishia Desemba 2017, wastani wa riba za amana
uliongezeka kufikia asilimia 9.6 kutoka wastani wa asilimia 8.8 Desemba 2016.
Viwango vya riba za amana za mwaka mmoja vilipungua kutoka asilimia 11.0
Desemba 2016 hadi asilimia 10.9 Desemba 2017. Hata hivyo, viwango vya riba za
mikopo ya hadi mwaka mmoja viliongezeka kufikia asilimia 18.2 Desemba 2017
kutoka wastani wa asilimia 12.9 Desemba 2016. Hii ilitokana na mabenki kuchukua
tahadhari kubwa kwa wateja wanaoshindwa kurejesha mikopo. Hata hivyo, riba
katika soko la fedha baina ya mabenki ilipungua na kufikia wastani wa
asilimia 3.3 Desemba 2017 kutoka
asilimia 13.5 Desemba 2016. Riba kwenye dhamana za Serikali ilipungua kutoka
asilimia 15.1 Desemba 2016 hadi asilimia 8.2 Desemba 2017.
14.Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali
kupitia Benki Kuu imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuongeza ukwasi
katika uchumi na ukuaji wa mikopo yenye gharama nafuu kwa sekta binafsi. Hatua
hizo ni pamoja na: kupunguza kiwango cha chini cha sehemu ya amana za benki za
biashara kinachotakiwa kuhifadhiwa Benki Kuu (SMR)kutoka asilimia 10 hadi 8
mwezi April 2017; Kupunguza kiwango cha riba cha benki za biashara kukopa Benki
Kuu kutoka asilimia 16 hadi asilimia 12 na kwa mara nyingine hadi asilimia 9
mwezi Agosti 2017, lengo lilikuwa kuyawezesha mabenki kukopa na kukopesha kwa
riba nafuu; mabenki na taasisi za fedha kutakiwa kutumia taarifa zitolewazo na
mfumo wa upatikanaji wa taarifa za wakopaji (credit refence system) kufanya
maamuzi sahihi katika ukopeshaji; na hivi
karibuni Benki Kuu imeelekeza mabenki ya biashara kufanya marekebisho ya muda
wa marejesho ya mikopo na kuanzisha kitengo cha ufuatiliaji wa madeni. Kufuatia hatua hizo zilizochukuliwa na Serikali za
kuimarisha sekta ya fedha, mwenendo wa mikopo kwa sekta binafsi umeanza
kuongezeka kutoka kiwango cha ukuaji hasi wa asilimia 1.5 mwezi Oktoba 2017
hadi ukuaji chanya wa asilimia 2.0 mwezi Januari 2018. Aidha, mikopo chechefu
imeanza kupungua kutoka asilimia 12.5 ya mikopo kwa sekta binafsi mwezi
Septemba 2017 hadi kuwa asilimia 11.2
mwezi Desemba 2017.
15. Mheshimiwa
Mwenyekiti, hadi kufikia Desemba
2017, deni la Serikali lilifikia
dola za Marekani milioni 21,308.7 sawa na shilingi bilioni 47,756.3
ikilinganishwa na dola za Marekani 19,957 milioni Juni, 2016. Kati ya kiasi
hicho, deni la nje ni dola milioni 15,237.0, sawa na shilingi bilioni 34,148.6,
ikiwa ni asilimia 71.5 ya deni lote. Deni la ndani lilikuwa shilingi bilioni
13,607.7 sawa na asilimia 28.5 ya deni lote. Ongezeko la deni kwa kipindi cha
Juni 2016 hadi Desemba, 2017 lilitokana na mikpo mipya na mabadiliko ya kiwango
cha ubadilishaji fedha (exchange rate fluctuations). Tathmini ya uhimilivu wa
deni iliyofanyika mwezi Novemba 2017 kwa kipindi kilichoishia Juni, 2017
inaonesha kuwa deni ni himilivu kwa kipindi cha muda wa kati na muda mrefu.
Uwiano wa deni la ndani na nje kwa Pato la Taifa kwa mwaka 2017/18 ni asilimia
34.4 ikinganishwa na ukomo wa asilimia 56, hivyo deni bado lipo chini ya
kiwango cha hatari. Aidha, uwiano wa deni la nje na mauzo ya nje ni asilimia
81.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150. Hii inamaanisha kuwa uwezo wetu
wa kulipa deni bado ni imara.
SEHEMU
YA PILI
MPANGO
WA MAENDELEO WA TAIFA YA MWAKA 2018/19
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo
wa Taifa wa Mwaka 2017/18
16. Mheshimiwa
Mwenyekiti, hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa baadhi ya miradi ya
maendeleo kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Januari 2018 ni kama ifuatavyo:
i.
Mradi
wa kuzalisha umeme wa maji Rufiji (Rufiji Hydropower Project): shilingi bilioni
3.2 zimetumika kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa mradi. Mchakato
wa kumpata mkandarasi wa ujenzi unaendelea na ujenzi wa njia ya usafirishaji
umeme wa msongo wa kV 33 kutoka Dakawa hadi eneo la mradi (km 53) ambapo km 8.5
zimesimikwa nguzo za miti, na kukamilika kwa matayarisho ya km 36
zitakazosimikwa nguzo za zege;
ii.
Ujenzi
wa Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge: Kwa ujumla utekelezaji wa mradi
huu umefikia asilimia 8 na unatarajiwa kufikia asilimia 15 ifikapo Juni 2018. Kwa
kipande cha Dar es Salaam – Morogoro, shilingi bilioni 4.04 zimetolewa kwa kazi
ya usanifu wa mradi na tathmini ya muundo wa ardhi (soil structure). Aidha, ili
kulipa fidia uthaminishaji wa mali zitakazoathiriwa na ujenzi wa mradi unaendelea.
Mkandarasi wa ujenzi amelipwa shilingi bilioni 415.14 ambapo ujenzi wa kambi za
Dar es Salaam umekamilika kwa asilimia 99, Soga asilimia 89 na Ngerengere
asilimia 67 na uinuaji wa tuta la reli umefikia asilimia 15. Kwa kipande cha
Morogoro – Makutupora tayari mkandarasi wa ujenzi amepatikana na kulipwa malipo
ya awali ya shilingi bilioni 492.6;
iii.
Kuboresha
Shirika la Ndege Tanzania: shilingi bilioni 7.85 zimetolewa kutekeleza mkataba
wa ununuzi wa ndege, ambapo ndege mbili za aina ya Bombadier CS 300 zimelipiwa kwa
asilimia 30 na ndege moja kubwa ya masafa marefu, Boeing 787, kwa asilimia 52;
iv.
Ujenzi
wa barabara za kuunganisha makao makuu ya mikoa na zile zinazounganisha
Tanzania na nchi jirani: barabara za Dodoma – Babati (sehemu ya Mayamaya – Mela - Bonga km 188.15),
Sumbawanga-Kanazi (km 75.0), Kanazi-Kizi-Kibaoni (km 76.6), Kyaka-Bugene (km
59.1), Kaliua – Kazilambwa (km 58.9), Magore
– Turiani (km 48.8), Uyovu – Bwanga (km 45) zimekamilika kwa kiwango cha
lami na ujenzi wa madaraja ya Kilombero na Kavuu umekamilika. Vile vile, ujenzi
wa barabara ya juu ya TAZARA umefikia asilimia 70 na ile ya Ubungo Interchange imeanza
kujengwa;
v.
Ujenzi
wa jengo la abiria pamoja na miundombinu yake katika kiwanja cha ndege cha
kimataifa cha Julius Nyerere umefikia asilimia 68;
vi.
Ujenzi
wa ukuta katika machimbo ya Tanzanite – Mererani umekamilika kwa gharama ya shilingi
bilioni 5.42;
vii.
Shamba
la Miwa na Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi: hekta 300 tayari zimepandwa miwa na ujenzi
wa boma la kiwanda cha sukari umekamilika, kuwezesha hatua za kuagiza mitambo;
viii.
Ujenzi
wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi Tanga-Tanzania: upembuzi yakinifu
kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya kupakulia mafuta umekamilika na wananchi wa
Chongoleani - Tanga watakaopisha ujenzi wa bomba wamelipwa fidia;
ix.
Chuo
Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili - kampasi ya Mloganzila kimezinduliwa
rasmi na Mhe. Dkt. John P. Magufuli, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania
Novemba, 2017 na shilingi bilioni 4 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi unaoendelea wa
mabweni na majengo mengine ya kufundishia;
x. Shilingi
bilioni 80 fedha za ndani zimetumika kununua na kusambaza dawa, vifaa tiba na
vitendanishi kwa vituo vya kutolea huduma nchi nzima; na
xi.
Shilingi
bilioni 3 fedha za ndani na milioni 800 fedha za nje zimetumika kununua chanjo
za kudhibiti magonjwa mbalimbali; kulipa mchango wa Serikali katika Shirika la
GAVI kwa ajili ya chanjo; na kutolewa kwa mafunzo ya namna ya kukabiliana na
saratani ya kizazi.
17. Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mafanikio mengine
yaliyopa-tikana ni pamoja na: (i) Kuendelea kugharamia elimumsingi bila ada;
(ii) Kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika shule 180 za
msingi na 110 za sekondari; (iii) Kukamilika kwa ukarabati wa vituo vya afya
204 na miundombinu yake nchi nzima. Vile vile, kupitia Shirika la Ushirikiano
wa Maendeleo la Korea (KOICA) ukarabati wa zahanati 28, vituo vya afya 21,
hospitali ya wilaya 1 na ya mkoa 1 umekamilishwa; (iv) Ununuzi wa mitambo na
vifaa vya kufundishia na kujifunzia vya uhandisi umeme katika vyuo vya ufundi
stadi vya Mtwara, Morogoro, Njombe na Dodoma unaendelea; (v) Kukamilika kwa
visima 19 katika maeneo ya Kimbiji na Mpera, Dar es Salaam; (vi) Kukamilika kwa
mradi wa kupeleka maji katika miji ya Mwadui, Kishapu, Kolandoto na Maganzo
ambapo wakazi 58,155 wamenufaika; na kuendelea na ujenzi wa njia ya kuruka na
kutua ndege, kiungio na maegesho ya ndege katika kiwanja kipya cha ndege cha
Geita.
18.Mheshimiwa
Mwenyekiti, hadi sasa viwanda
vipya vilivyojengwa katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya
Tano ni zaidi ya 3,600. Kwa upande wa sekta binafsi, mafanikio yaliyopatikana
ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi na kuzinduliwa kwa viwanda vifuatavyo: (i)
Saruji: Kilimanjaro Cement na upanuzi wa viwanda vya Tanga Cement na Mbeya
Cement ambapo vimeongeza uzalishaji kufikia tani milioni 11.28 na kutoa ajira
8000; (ii) Marumaru: Goodwill Ceramic Ltd cha Mkuranga kilichozalisha ajira
4,500; (iii) Chuma: Kilua Steel-Mlandizi chenye uwezo wa kuzalisha tani 500,000
kwa mwaka na ajira 800; (iv) Kusindika Matunda: Elven Agri Co. Ltd chenye uwezo
wa kukausha matunda tani 2,500, kusindika nyanya tani 1,000 kwa mwaka na ajira
300; na (v) Kiwanda cha Sigara cha Phillip Morris – Morogoro na Kiwanda cha
kuzalisha Mita za Umeme (LUKU) cha INHEMETER – Dar es Salaam. Aidha, kiwanda
cha kukamua mafuta ya alizeti cha Mount Meru – Singida, Kahama Oil Mills,
viwanda vya plastiki, chuma, mabati na mabomba vilivyopo Kahama vimezinduliwa
na vinafanya kazi.
Vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo
wa Mwaka 2018/19
19. Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mpango unaowasilishwa
ni watatu katika hatua za utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka
Mitano 2016/17-2020/21 wenye dhima ya “Kujenga Uchumi wa Viwanda ili kuchochea
Mageuzi ya Uchumi na Maendeleo ya Watu”. Hivyo, vipaumbele vya Mpango wa
Maendeleo kwa mwaka 2018/19 vitazingatia maeneo mbalimbali ya Mpango wa Pili wa
Maendeleo wa Miaka Mitano. Aidha, sehemu kubwa ya miradi itakayotekelezwa
katika maeneo hayo ya vipaumbele ni ile inayoendelea kama ifuatavyo:
(a) Miradi
ya Kielelezo na Itakayopewa Msukumo wa Kipekee
20. Mheshimiwa
Mwenyekiti, Miradi
itakayotekelezwa ni pamoja na: kituo cha kuzalisha umeme wa maji katika Mto
Rufiji (MW 2100); ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge,
hususan, vipande vya Dar es Salaam hadi Morogoro (km 300) na Morogoro hadi Makutupora
(km 336); kuboresha Shirika la Ndege Tanzania; ujenzi wa bomba la kusafirisha
mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Tanga; uzalishaji wa makaa ya mawe na
umeme - Mchuchuma na chuma - Liganga; uendelezaji wa shamba la miwa na ujenzi
wa kiwanda cha sukari Mkulazi; Kituo cha Biashara na Huduma Kurasini;
uendelezaji wa kanda maalum za kiuchumi hususan, Bagamoyo na Kigamboni;
uanzishwaji wa kiwanda cha kusindika gesi asilia kuwa kimiminika – Lindi na
kuongeza idadi ya wataalam katika fani adimu.
(b) Miradi
Mingine ya Kukuza Uchumi wa Viwanda
21. Mheshimiwa
Mwenyekiti, Miradi ya kukuza
uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda inalenga kuendelea kujenga
viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi nchini, hususan za
kilimo, madini na gesi asilia. Katika eneo hili, miradi itakayopewa kipaumbele
ni pamoja na: kuimarisha shughuli za Shirika la Viwanda Vidogo – SIDO; Kiwanda
cha Ngozi na Bidhaa za Ngozi-Karanga; Mradi wa Magadi Soda - Bonde la Engaruka;
Kituo cha zana za Kilimo na Ufundi Vijijini-CARMATEC; na viwanda vya Nyumbu na
Mzinga.
(c) Miradi
ya Kufungamanisha Maendeleo ya Viwanda na Maendeleo ya Watu
22. Mheshimiwa
Mwenyekiti, eneo hili linalenga
kuendeleza mafanikio ya upatikanaji wa huduma msingi kwa ustawi wa maisha ya Watanzania.
Miradi katika eneo hili ni pamoja na: ujenzi na ukarabati wa maktaba za mikoa;
ujenzi na uboreshaji wa maabara katika shule na taasisi; kuendeleza ujenzi na
kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji, kupanua huduma za elimu ya afya na
usafi wa mazingira shuleni, mijini na vijijini; kuimarisha upatikanaji wa
huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma kwa ngazi zote ikiwemo zahanati,
vituo vya afya, hospitali za mikoa, kanda na kitaifa, huduma za matibabu ya
kibingwa, kupunguza vifo vya
akina mama wajawazito, kuimarisha upatikanaji na usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, sambamba na
kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya; kukamilisha ujenzi na
ukarabati wa vyuo vya ufundi stadi vya wilaya na mikoa; utoaji wa mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu; na kuimarisha programu ya kukuza ujuzi.
(d) Miradi
ya Ujenzi wa Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara na Uwekezaji
23. Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika eneo hili
Serikali imejielekeza katika kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu,
ikijumuisha miundombinu ya nishati, usafirishaji (reli, barabara, madaraja,
viwanja vya ndege na bandari) na ununuzi na ukarabati wa meli na vivuko. Baadhi
ya miradi iliyozingatiwa katika eneo hili ni: kuendelea na ukarabati wa reli ya
kati na TAZARA ikiwemo ununuzi wa injini na mabehewa; kuendelea na ujenzi wa
barabara zinazounganisha makao makuu ya mikoa, zinazounganisha masoko ya
kikanda na barabara za kupunguza msongamano mijini; na miradi ya kuzalisha na
kusambaza umeme. Aidha, ujenzi wa mazingira wezeshi utahusu pia uimarishaji wa
ulinzi na usalama, upatikanaji wa haki, utawala wa sheria na utawala bora.
(e) Kuimarisha
Usimamizi na Utekelezaji wa Mpango
24. Mheshimiwa
Mwenyekiti, Shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na: kuimarisha
mifumo ya kitaasisi kwa lengo la kuimarisha ufuatiliaji na tathmini kwa
kuzingatia Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma; kujenga uwezo wa
wataalam katika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi ya maendeleo; na
kuimarisha mifumo ya uhifadhi na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa miradi
kulingana na thamani ya fedha (value for money).
(f) Mikakati
ya Kuchochea Ukuaji wa Sekta za Kilimo
25. Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali katika kuchochea ukuaji wa sekta za kilimo
itaendelea: kuboresha miundombinu ya umwagiliaji; kuongeza upatikanaji wa zana
na pembejeo za kilimo; kuongeza huduma za ugani; kuboresha upatikanaji wa miundombinu
ya hifadhi ya mazao na masoko; na kutatua vikwazo mbalimbali vinavyosababisha
viwanda vya ndani vinavyotumia malighafi zitokanazo na kilimo kushindwa
kushindana na bidhaa husika kutoka nje.
Mikakati ya Kuchochea Ushiriki wa Sekta Binafsi
26. Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mpango unasisitiza
ujenzi wa mazingira yatakayochochea na kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi
katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Pamoja na hatua za kuondoa vikwazo
katika uwekezaji na ufanyaji biashara, Mpango umezingatia utekelezaji wa
mapendekezo ya marekebisho ya sheria, kanuni na taratibu kwa miradi ya ubia
(PPP) na kuhakikisha upatikanaji rahisi wa maeneo ya uwekezaji. Hatua nyingine
zitakazochukuliwa ni pamoja na: kuandaa Sera ya Maendeleo ya Sekta Binafsi;
kuimarisha mfumo rekebu na miundo - taasisi; kuimarisha mfumo wa majadiliano
kati ya Serikali na sekta binafsi; kuweka vivutio na sera za kibajeti kuwezesha
sekta binafsi kuwekeza katika maeneo ya kipaumbele na kushindana katika soko la
ndani na kimataifa; na kusimamia ubora wa bidhaa na kuhamasisha wananchi
kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini.
27. Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika mwaka 2018/19,
Serikali inategemea kufanya upembuzi yakinifu kuainisha uwezekano wa kutekeleza
miradi ifuatayo kwa utaratibu wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP): miradi
ya bandari ya Mwambani, reli ya Mtwara-Mchuchuma/Liganga kwa kiwango cha
standard gauge, reli ya Tanga-Arusha-Musoma kwa kiwango cha standard gauge,
ujenzi wa miundombinu ya reli na uendeshaji wa treni ya abiria katika jiji la
DSM, usambazaji wa gesi asilia nchini na mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART)
awamu ya II hadi IV.
SEHEMU
YA TATU
MFUMO
NA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2018/19
Mwenendo wa Mapato na Matumizi Hadi Februari 2018
28. Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika mwaka 2017/18, Serikali
ilipanga kukusanya na kutumia jumla ya shilingi bilioni 31,712.0. Hadi kufikia
mwezi Januari 2018, jumla ya mapato kutoka vyanzo vyote yalifikia shilingi
bilioni 17,401.9 sawa na asilimia 85.0 ya lengo la
kipindi hicho, ambapo:
(i)
Mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 10,036.3
sawa na asilimia 88.3 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 11,360.8;
(ii)
Mapato yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 1,456.1
sawa na asilimia 98.2 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 1,483.4;
(iii)
Mapato yaliyokusanywa na Halmashauri yalikuwa shilingi
bilioni 345.9 sawa na asilimia 74.1 ya makadirio ya shilingi bilioni 466.9;
(iv)
Misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa
Maendeleo ilifikia shilingi bilioni 1,408.5, sawa na asilimia 66 ya lengo la
shilingi bilioni 2,145.1;
(v)
Mikopo ya ndani ilifikia shilingi bilioni 3,931.0
ikiwa ni asilimia 95.6 ya kiasi kilichopangwa kukopwa, ikijumuisha shilingi
bilioni 3,246.0 zilizokopwa kulipia amana za Serikali zilizoiva (rollover) na
mikopo mipya ya shilingi bilioni 685.0; na
(vi)
Mikopo ya nje ya kibiashara ilifikia shilingi
bilioni 224.1.
29. Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika kipindi hicho,
Serikali iliweza kutoa mgao wa shilingi bilioni 17,401.9 kwa mafungu mbalimbali
kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti, sawa na asilimia 85.0 ya makadirio ya
bajeti hadi Januari 2018. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 13,349.9
zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 4,052.0 kwa
matumizi ya maendeleo, zikijumuisha shilingi bilioni 3,447.3 za ndani na
shilingi bilioni 604.5 za nje.
30. Mheshimiwa Mwenyekiti, Maeneo yaliyopewa kipaumbele
katika mgao wa bajeti ni pamoja na: kulipa deni la Serikali na mishahara ya
watumishi wa umma; kugharamia ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli na
viwanja vya ndege; kulipia malimbikizo ya madai ya wazabuni, wakandarasi na
watumishi wa umma; kuendelea na utekelezaji wa miradi ya uzalishaji na
usambazaji wa umeme na kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; kugharamia
elimu-msingi bila ada; utekelezaji wa miradi ya maji; na kununua dawa na vifaa
tiba.
31. Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafanikio yaliyopatikana
katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2017/18 katika kipindi cha Julai 2017
hadi Februari 2018 ni pamoja na:
(i)
Kuimarisha
na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ambapo jumla ya shilingi bilioni
59.0 zimetolewa kwa Halmashauri za Wilaya 110 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati
wa vituo vya afya, shilingi bilioni 24.1 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali za
mikoa 24. Aidha, jumla ya shilingi bilioni 125.7 zimetolewa kwa ajili ya
ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi;
(ii)
Katika
kutekeleza lengo la kuwapatia wananchi mijini na vijijini huduma ya maji safi
na salama kiasi cha shilingi bilioni 149.3 kimetolewa kwa ajili ya kutekeleza
miradi ya maji;
(iii)
Katika
jitihada za kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme ili kuhakikisha wananchi
wanafikiwa na huduma hii muhimu, kiasi cha shilingi bilioni 300.9 kimetolewa
kwa ajili miradi ya nishati vijijini, umeme wa jotoardhi, uzalishaji wa umeme
katika vyanzo mbalimbali na usambazaji wa gesi asilia;
(iv)
Katika
kutekeleza azma ya kutoa elimu msingi bila ada na kugharamia mikopo ya
wanafunzi wa elimu ya juu, Serikali imetoa shilingi bilioni 543.5;
(v)
Serikali
imeendelea kutekeleza ujenzi wa miundombinu ili kupanua fursa za uchumi,
kilimo, biashara na viwanda ikiwemo barabara zinazounganisha mikoa na nchi
jirani, barabara zinazopunguza msongamano katika majiji, barabara za vijijini,
reli, viwanja vya ndege, na bandari. Katika eneo hili kiasi cha shilingi
bilioni 1,451.5 kimetolewa;
(vi)
Serikali
imeendelea kulipa malimbikizo ya madai ya watumishi umma, wazabuni, wakandarasi
na watoa huduma ambapo kiasi cha shilingi bilioni 939.5 kimelipwa; na
(vii) Serikali imeendelea kusimamia matumizi bora ya fedha za
umma kwa kufanya ufuatiliaji na uhakiki wa madai mbalimbali ikijumuisha uhakiki
wa madai ya fidia kwa wananchi wanaopisha miradi ya maendeleo na malimbikizo ya
madai ya watumishi wa umma. Kati ya
madai yaliyowasilishwa ya shilingi bilioni 312.6, shilingi bilioni 156.8
zilikubaliwa baada ya kukidhi vigezo na hivyo Serikali imeokoa shilingi bilioni
155.8.
32. Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya mafanikio
yaliyopatikana kulikuwa na changamoto za utekelezaji wa Mpango na
Bajeti kwa mwaka 2017/18, hususan kutokana na kutofikiwa kwa malengo ya makusanyo ya mapato kulikosababishwa
na:
(i)
Mwamko mdogo wa kulipa kodi na hususan kuzingatia
matumizi ya mashine za kielektroniki;
(ii)
Masharti magumu ya upatikanaji wa mikopo ya
kibiashara kutoka nje; na
(iii)
Mabadiliko ya sera za misaada katika nchi
zilizokuwa zikitupatia misaada ya kibajeti.
Aidha, utekelezaji wa
Mpango na Bajeti uliathiriwa pia na uwepo wa malimbikizo ya madai; ugumu wa upatikanaji
wa maeneo ya uwekezaji; matayarisho hafifu ya miradi; na mabadiliko ya tabia
nchi ambayo yalisababisha uharibifu wa miundombinu ya usafiri kutokana na mvua
kubwa katika baadhi ya maeneo.
33. Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizochukuliwa kukabiliana na
changamoto hizo ni pamoja na:
(i)
Kuendelea
kutoa elimu juu ya umuhimu na faida za kulipa kodi kwa kutumia mitandao ya
kielektroniki. Aidha, Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala za Serikali zilihimizwa
kutumia mabenki katika kukusanya maduhuli;
(ii)
Kuwezesha
mifumo ya kodi kutambua malipo kwa kutumia huduma za simu za mkononi kukusanyia
kodi mbalimbali. Kwa kufanya hivyo
itatoa fursa kwa walipa kodi kulipa kodi kwa urahisi na kuwezesha kodi nyingi
kukusanywa;
(iii)
Kuanza
kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Stempu za Kodi (Electronic Tax Stamps) kwenye
viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa na zile
zinazoingizwa nchini. Mfumo huu utasaidia kupata taarifa kamili za uzalishaji
viwandani pale tu kiwanda kinapofanya uzalishaji na kupunguza uvujaji wa mapato
ya Serikali;
(iv)
Kuboresha
na kuimarisha mfumo wa kielektroniki wa kutolea risiti za kodi (EFDMS) ili kuwezesha
ufuatiliaji wa karibu wa mauzo na utoaji wa risiti kwa kila manunuzi badala ya
kutumia risiti za makundi (batch). Hii itasaidia kupata taarifa za uhakika za
walipa kodi zitakazotumika katika kukokotoa kodi kwa usahihi na kuweza kutoa
makadirio stahiki ya kodi;
(v)
Kutekeleza
mradi wa dirisha moja la Forodha (Tanzania Electronic Single Window System) ili
kuwaweka pamoja wadau wote wa kuondosha mizigo bandarini na mipakani. Lengo ni
kusogeza huduma karibu na waagizaji bidhaa na hivyo kuongeza kasi ya uingizaji
bidhaa nchini (Turn around);
(vi)
Kutekeleza
Mwongozo wa Ushirikiano baina ya Serikali na Washirika wa Maendeleo
(Development Cooperation Framework - DCF) ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa
fedha kutokana na ahadi zao;
(vii) Kuendelea kusisitiza nidhamu katika utekelezaji wa bajeti
kama ilivyoidhinishwa na Bunge kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka
2015;
(viii) Kuendelea kuwianisha mapato na matumizi kwa kuhakikisha
kuwa mgao wa fedha unaendana na upatikanaji wa mapato na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima;
(ix)
Kuzuia
ongezeko la malimbikizo mapya ya madai na kulipa madai yaliyohakikiwa ikiwa ni
pamoja na kusaidia kuongeza ukwasi na kuchochea shughuli za kiuchumi; na
(x)
Kuanza
utekelezaji wa mkakati wa kufanya maboresho ya mazingira ya biashara nchini
(Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment).
Sera za
Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2018/19
34. Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera za mapato kwa mwaka 2018/19 kwa ujumla wake
zitalenga kuongeza mapato ya ndani kwa kurahisisha ulipaji wa kodi kwa kutumia
mifumo ya kielektroniki; kuendelea na zoezi la kurasimisha sekta isiyo rasmi
ikiwa ni pamoja na kupima na kutoa hati miliki za makazi/viwanja, mashamba na kuthaminisha majengo; kuimarisha mazingira
ya kuvutia uwekezaji na biashara ili kufikia azma ya Serikali ya kujenga uchumi
wa viwanda, hii ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama, utawala wa sheria na
utawala bora; kutekeleza mkakati wa kufanya maboresho ya mazingira ya biashara
nchini; na kusimamia mfumo wa Serikali wa ukusanyaji wa maduhuli kwa njia ya
kieletroniki (GePG). Aidha, kwa upande wa misaada na mikopo nafuu, Serikali
itaendelea kuimarisha mahusiano na Washirika wa Maendeleo kwa kutumia Mwongozo
wa Ushirikiano baina ya Serikali na Washirika wa Maendeleo. Uboreshaji huu unatarajiwa kuongeza uwekezaji,
uzalishaji, ajira na miamala ya biashara na hivyo kupanua wigo wa mapato.
35. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018/19, Serikali itaendelea
kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na.
11 ya mwaka 2015. Lengo kuu ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba
mianya ya uvujaji wa fedha za umma, kudhibiti malimbikizo ya madai mapya na
kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi ya kielelezo. Serikali
itachukua hatua mbalimbali ili kutimiza azma hii kama ifuatavyo:
(i)
Kuwianisha matumizi na mapato halisi
yatakayopatikana kwa kila mwezi;
(ii)
Kuhakikisha kuwa ununuzi wa umma unazingatia
thamani ya fedha;
(iii)
Kusimamia kikamilifu na kuzuia matumizi na miadi ya
matumizi nje ya mfumo wa “IFMS”;
(iv)
Kuendelea kufanya uhakiki wa madai mbalimbali na
kulipa madai yaliyohakikiwa;
(v)
Kuimarisha maandalizi na uchambuzi wa miradi; na
(vi)
Kuimarisha ufuatiliaji wa matumizi ya Serikali ili kupata
thamani ya fedha.
Kiwango
na Ukomo wa Bajeti kwa Mwaka 2018/19
36. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia shabaha, na sera za bajeti kwa mwaka
2018/19, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla ya Shilingi bilioni 32,476.0
zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho. Mfumo na ukomo wa
bajeti ya mwaka 2018/19 umezingatia hali halisi ya upatikanaji wa mapato kutoka
vyanzo mbalimbali.
37. Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya
Halmashauri yanatarajiwa kuwa Shilingi bilioni 20,894.6 sawa na asilimia 64 ya
bajeti yote. Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya
jumla ya Shilingi bilioni 18,000.2 sawa na asilimia 13.6 ya Pato la Taifa.
Mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 2,158.8 na mapato
kutoka vyanzo vya Halmashauri ni Shilingi bilioni 735.6.
38. Mheshimiwa Mwenyekiti, vyanzo vingine vya mapato ni pamoja na misaada na
mikopo yenye masharti nafuu ya Shilingi bilioni 2,676.6 kutoka kwa Washirika wa
Maendeleo, ikiwa ni asilimia 8 ya bajeti yote. Serikali pia inatarajia kukopa
Shilingi bilioni 5,793.7 kutoka soko la ndani, ambapo shilingi bilioni 4,600.0 kwa ajili ya kulipia
hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na Shilingi bilioni 1,193.7 ni
mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Kiasi cha Shilingi
bilioni 1,193.7 ambazo ni mikopo mipya ni sawa na asilimia 0.9 ya Pato la
Taifa. Ili kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi muhimu ya miundombinu,
Serikali inatarajia kukopa shilingi bilioni 3,111.1 kutoka soko la nje.
39. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa matumizi, katika mwaka 2018/19
Serikali inapanga kutumia jumla ya Shilingi bilioni 32,476.0. Kati ya fedha
hizo, Shilingi bilioni 20,468.7 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia
63 ya bajeti. Matumizi ya kawaida yanajumuisha Shilingi bilioni 10,004.5
kulipia deni la Serikali, shilingi bilioni 7,369.7 mishahara, shilingi bilioni 3,094.5
matumizi mengineyo (OC) na shilingi bilioni 389.9 matumizi yatokanayo na vyanzo
vya ndani vya Halmashauri.
Kwa
upande wa matumizi ya maendeleo, Serikali itatumia shilingi bilioni 12,007.3
sawa na asilimia 37 ya bajeti. Kiasi hiki kinajumuisha Shilingi bilioni 9,876.4
sawa na asilimia 82.3 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 2,130.9 sawa na
asilimia 17.7 ni fedha za nje. Hata hivyo, kiasi hiki hakihusishi uwekezaji wa
moja kwa moja wa sekta binafsi, mashirika ya Umma na ubia kati ya sekta ya umma
na binafsi. Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kuwezesha mashirika ya
Umma na sekta binafsi kutekeleza miradi ya maendeleo.
40. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia maelezo hayo, kiwango na ukomo wa
bajeti kwa mwaka 2018/19 ni kama inavyooneshwa katika Jedwali Na. 1.
Jedwali Na. 1: Mfumo wa Bajeti ya
Mwaka 2018/19
Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango
HITIMISHO
41. Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango na Bajeti ya mwaka
2018/19 vinalenga hasa katika kuendelea kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya
Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kuboresha ustawi wa jamii. Aidha, Serikali
itaendelea kujizatiti katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuendelea
kudhibiti mianya ya ukwepaji wa kodi.
42. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa matumizi,
serikali itaendelea kuweka mkazo katika usimamizi na udhibiti wa matumizi ya
fedha za umma ili zitumike zaidi kugharamia miradi ya kipaumbele na kuboresha
upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.
43. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
No comments:
Post a Comment