Habari za Punde

Uongozi wa Baraza la Mji Wilaya ya Mkoani Watembelea Miundo Mbinu ya Mitaro.Kuhakikisha Iko Salama Kuepusha Madhara Wakati wa Mvua za Masika.
MKURUGENZI Baraza la mji Wilaya ya Mkoani Kisiwani Pemba, amewataka wananchi wilayani humo kuendeleza na kudumisha usafi wa mazingira yaliyowazunguka katika kipindi hichi cha mvua,  ili kujikinga na maradhi ya mripuko yakiwemo kipindupindu na kuharisha.

Aliyasena hayo, alipokuwa akizungumza na gazeti hili, huko ofisini kwake Mkoani kufuatia mvua za masika zilizoanza kunyesha.

Alieleza katika kipindi hichi cha mvua ni vyema wananchi wakawa makini katika kudumisha usafi wa mazingira, kwani kutofanya hivyo inaweza kuwa sababu ya kupata maradhiya kipindupindu ama kuharisha.

Alifahamisha kuwa wananchi waache tabia ya kutupa taka ovyo na badala yake wayatumie madampo yaliyojengwa na baraza la mji, ili mji uweze kuwa safi na wenye kupendeza.

"Kutupa taka ovyo kunachangia kuleta maradhi ya mripuko lazima wananchi wawe makini na waangalifu",alisema.

Alisema ni jambo la kushangaza kwa wananchi kutoyatumia madampo hayo, wakati baraza la mji huo limejenga kwa gharama ili kuweza kutumiwa kwa kutupia taka. 

Akizungumzia kuhusu usafi kwa wafanya biashara alisema hatomvumilia mfanya biashara yoyote atakayekwenda kinyume na maagizo watakayopewa na Serikali kuhusiana na kudumisha usafi na namna ya kuzihifadhi biashara zao.

Alisema kutodumisha usafi katika biashara ya vyakula kuna uwezekano mkubwa wa kupata maambukizo ya maradhi hayo, kwani wanaonunuwa biashara hizo ni watu wa maeneo tofauti.

"Biashara nazo zinahitaji kuwekwa katika hali ya usafi kwani zikiwa na vimelea vya maradhi ya kuharisha vinaenea kwa haraka na kusababisha janga kubwa katika nchi",alisema.

Kwa upande wao wananchi Wilayani humo, walimuomba Mkurugenzi huyo kuendelea na mkakati wake wa kupitia nyumba kwa nyumba kuangalia hali ya usafi wa mji huo kwani imechangia kudumishwa usafi na muonekano wake unaridhisha .

Hivyo walisema kila mmoja atakuwa mlinzi wa mwenzake kuhakikisha usafi unadumishwa ili wilaya hiyo iweze kuwa salama na kuepukana na maradhi ya mripuko.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.