Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Ulinzi Zanzibar Luteni Kanali Jabir Hamza, akizungumza na waandishi
wa habari katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni mjini
Zanzibar.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Ulinzi
Zanzibar Kanali Mstaafu Makame Mabrouk Hassan, akizungumza na waandishi wa habari
katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni mjini Zanzibar.
Waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari, wakifuatilia mazungumzo
ya viongozi ya Wakala wa Ulinzi wa Serikali yaliyofanyika katika ukumbi wa
zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni mjini Zanzibar. (Picha na Miza Othman-
MAELEZO)
Na
Ali Issa-MAELEZO
WAKALA wa Ulinzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
umesema kuwa umeundwa kwa lengo la kutoa huduma bora za ulinzi zinazoendeshwa
kisasa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika
ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, Mkurugenzi Mtendaji wa wakala huo
Kanali Jabir Hamza, amesema serikali imechukua hatua hiyo baada ya kubaini
kasoro zinazowapa mwanya wahalifu kuhujumu miradi katiia maeneo ya uwekezaji hasa
utalii na mengine.
Kanali Hamza amesema kuwa, wakala huo ambao
ni taasisi ya serikali upo kisheria, ukiwa umeanzishwa chini ya kifungu cha sheria namba mbili ya
mwaka 2015.
Alifahamisha kuwa, kuja kwa wakala huo ni
njia iliyokusudiwa kutoa ulinzi kwa kutumia silaha za kijeshi na kuwahamasisha
wamiliki wa kampuni na miradi kuondokana na ulinzi wa silaha za kienyeji kama
marungu.
“Katika ulimwengu huu ambao wahalifu
wanabuni mbinu mpya kila uchao, hatuwezi kuendelea kulinda kwa magongo kwani
ulinzi wa aina hiyo hauna usalama kwa walinzi wala wanaolindiwa,” alisema.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alisema wakala
huo haukuja kwa nia ya kuzifuta kampuni binafsi zinazotoa huduma za ulinzi,
bali upo kwa ajili ya kuzielekeza kampuni hizo kwa kutoa miongozo itakayozifanya
zibadii mfumo wao wa ulinzi.
Aidha alisema, lengo la wakala huo ni
kuepusha majanga ya kutekwa kwa walinzi wasiokuwa na silaha za kisasa wala
ujuzi wa kupambana na wahalifu, hali inayosanabisha kuibiwa mali za wawekezaji
na wafanyabiashara wengine, na hata kushambuliwa kwa silaha za moto na mapanga.
Alieleza matumaini yake kuwa, kampuni
nyengine za ulinzi zina haki ya kutoa huduma, lakini wakala wake utaendelea
kuwashajiisha wamiliki wa mali na miradi kutumia ulinzi wa uhakika kwa kuwa
kazi hiyo inafanywa kibiashara na serikali inategemea mapato.
Mbali ya mapato, kwa serikali, Kanali Hamza
alisema, fedha zinazopatikana pia zinasaidia kugharamia mahitaji mengine ya
Jeshi la Kujenga Uchumi.
Kwa upande mwengine, alisema kuundwa kwa wakala huo, kutasaidia
kupunguza uhaba wa ajira kwani litatoa fursa kwa vijana hasa waliopata mafunzo
kupitia Jeshi la Kujenga Uchumi, kuajiriwa na kwa wale waliofikia umri wa miaka
27 kupewa ajira za mkataba.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala huo Kanali
mstaafu Makame Mbarouk Hassan, alisema kazi yao nyengine ni kuvipa elimu na miongozo
vikundi vinavyoendesha ulinzi kwa njia ya doria.
Aidha, alisema kwa kuwa serikali inategemea
zaidi sekta ya utalii kiuchumi ambapo mara kadhaa wageni wamekuwa
wakishambuliwa, wakala huo ndio muarubaini wa kukomesha vitendo hivyo
vinavyoitia doa Zanzibar.
Alitumia fursa ya mkutano huo na waandishi wa
habari, kuomba ushirikiano wa kutosha kutoka kwa kampuni na watu binafsi
akiwahakikishia kuwa huduma zao zinalindwa na mikataba iliyotengenezwa na
wanasheria wa serikali
No comments:
Post a Comment