Habari za Punde

Kete 6,586 za madawa ya kulevya zanaswa Pemba

Na Salmin Juma, Pemba


JUMLA ya kete 6,586 zinazosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya, tayari zimeshakamatwa na Jeshi la Polisi la mikoa miwili ya Pemba, katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi mwaka huu 2018, sambamba na chupa 23 za ulevi aina ya gongo.

Mkoa wa kusini Pemba, ndio ulioongoza hadi sasa kwa wapiganaji wa Jeshi la Polisi, kukamata kete 5,243 na Mkoa wa kaskazini Pemba kwa kipindi hicho, ukiyanasa madawa hayo yanayosadikiwa kuwa ya kulevya kete 1,343 hadi Machi 20 mwaka huu.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa kusini Pemba Shehan Mohamed Shehan, alisema kazi hiyo haikufanywa na Jeshi la Polisi pekee, bali baadhi ya matukio yaliripotiwa na wananchi.

Alisema Jeshi la Polisi limekuwa na kazi ya kukamata na kupeleleza hivyo lazima wananchi waendelee kushirikiana nalo ili kuyafyeka madawa ya kulevya.

Alieleza kuwa, iwapo wananchi wataendelea na utamaduni huo wa kutoa taarifa za kuwepo kwa waingizaji, wasaambazaji, watumiaji na wauzaji vita dhidi ya dawa za kulevya inaweza kukoma.

“Mimi niendelee kuwataka wananchi wote kuhakikisha wanashirkiana na sisi katika kuendeleza vita dhidi ya utumiaji na uuzaji wa dawa za kulevya ndani na nje ya mkoa huu,”alieleza.

Katika hatua nyengine Kamanda huyo wa Polisi Mkoa wa kusini Pemba, Shehan Mohamed Shehan alisema kesi zaidi ya 12 zimeshafikishwa mahakamani na chache wanaendelea na upelelezi.

Hata hivyo tukio lililowasikitisha ni lile la kete 5115 zilizokamatwa Januari 25 mwaka huu, kwa kijana Othman Abdlla Hamad miaka 28, na mke wake Mtumwa Ramadhan Hamid, wa Machomane walipokamatwa kwa nyakati
tofauti.

Awali Othman alikamatwa na mafurushi matatu yenye idadi ya kete 352, kisha baada ya kufanyiwa upekuzi nyumbani kwake alikutwa na kete nyengine 4,763.

“Tukio hili hata watendaji wangu walipata mshangao kuona kijana huyo, anamzigo mkubwa cha kete za unga mafurushi kwa mafurushi hadi nyumbani kwake bila ya woga,”alieleza.

Nae Kamanda wa Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba Haji Khamis Haji, alisema bandari bubu zinaendelea kuwatesa kwa kuwepo wananchi kuendelea kupitisha dawa haramu.

Hivyo amewaomba wananchi kwa kutumia polisi jamii kuendelea kuzilinda bandari hizo na wakati mwengine kuendelea kutoa taarifa za kihalifu.

Kamanda huyo alimtaja kijaa Juma Said miaka 22, mkaazi wa Bopwe Wete kwamba, Machi 17 mwaka huu alikamatwa na kete 14 zinazosadikiwa ni dawa za kulevya .

Aidha alisema katika msako wao wa kawaida, Machi 16 walikamata pipa nne za pombe aina ya gongo na dumu 16 zenye ujazo wa lita 20, kila moja pamoja na mitambo miwili ya kutengenezea pombe hiyo.

Kwa mwaka 2017 pekee, Jeshi la Polisi Mkoa wa kusini lilikamata kete 3,621 za dawa zinazosadikiwa kuwa ni za kulevya, ingawa kwa mwaka huu, ndani ya kipindi cha miezi mitatu limeshakamata kete 5,243.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.