Habari za Punde

Wizara ya Afya Zanzibar Kupokea Malalamiko ya Wananchi Kwa Njia ya Simu.

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed akizungumza na waandishi wa habari wa Uongozi wa Wizara hiyo. kuhusiana na kupokea malalamiko ya Wananchi kupitia katika mawasiliano ya simu.  

Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 17.03.2018
Wizara ya Afya Zanzibar inakusudia kuweka Namba maalum za mawasiliano ili Wananchi wazitumie kwa ajili ya kuwasilisha malalamiko wanayokumbana nayo wakati wa kutafuta matibabu.
Hatua hiyo ni njia moja wapo ya Wizara kukabiliana na malalamiko ya muda mrefu ambayo wananchi wengi wanadai kukumbana nayo wanapohitaji matibabu katika vituo vya afya.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Wizara hiyo Hamad Rashid Ofisini kwake alipozungumza na Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi iliyoenda kuwasilisha taarifa ya ziara ya Kamati hiyo katika vitengo vya Wizara hiyo.
Amesema utaratibu utakapokamilika Wananchi watapata fursa ya kupiga simu moja kwa moja kwa lengo la kuwasilisha malalamiko yao.
Aidha Wahusika ambao Wizara itawapangia kazi ya kusikiliza malalamiko hayo watayafanyia uchunguzi ili kubaini uhalisia na kuchukua hatua stahiki.
“Kimsingi malalamiko yatakayotolewa tutayachuja maana wapo ambao malalamiko yao siyo ya msingi lakini wapo ambao wanakumbana na kadhia za kutisha ambazo zitatulazimisha kuchukua hatua ili kukabiliana na uzembe” Alisema Waziri Hamad.
Katika hatua nyingine Waziri huyo pia aliielezea kamati hiyo changamoto alizozizishuhudia alipofanya ziara yake katika Hosptal za Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja na Hosptial ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na idadi kubwa ya Wananchi wanaolala Hosptal ikilinganishwa na Wagonjwa hali inayopelekea usumbufu kwa Madaktari na Walinzi wa Hosptal.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Asha Abdulla aliwaelezea Wanakamati hiyo kile ambacho Wizara imetekeleza kwa kipindi cha Octoba hadi Disemba 2017/2018.
Amesema Wizara hiyo inasimamia Miradi sita ya maendeleo ikiwemo Mradi shirikishi wa Afya ya mama na mtoto, Mradi shirikishi wa kupambana na maradhi ya Ukimwi, Kifua kikuu na Ukoma, Mradi wa kumaliza Malaria Zanzibar, Mradi wa kupandisha hadhi hospital ya Mnazi mmoja na Mradi wa ujenzi wa maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.  
Katibu Asha alisema Wizara itaendelea kutoa huduma zilizo na viwango kwa jamii ili kuhakikisha afya za watu zinalindwa na kuimarishwa.
Aidha Wizara itaendelea kupokea maagizo na ushauri kutoka Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi na sehemu nyengine kwa lengo la kuziimarisha huduma zinazotolewa kwani maagizo hayo huzidisha kasi ya utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Mwinyihaji Makame aliipongeza Wizara kwa kutekeleza vyema majukumu yake ya kila siku licha ya changamoto wanazokabiliana nazo.
Hata hivyo Wajumbe hao waliiomba Wizara kuwapatia Elimu Wafanyabiashara juu ya namna bora ya uhifadhi wa chakula kwenye maghala ili kuepuka upangaji mbaya wa vyakula.
“Yapo baadhi ya Maghala ya kuhifadhia chakula yana hali nzuri lakini wapo baadhi ya wafanabiashara wanahfadhi chakula na Dawa kwa pamoja hali ambayo ni hatari kwa aafya za watumiaji” Alisema Mwenyekiti.
Katika ziara hiyo ya Wiki moja Kamati ilifanikiwa kutembelea Kitengo cha huduma ya Damu salama, Bodi ya Ushauri ya Mnazi mmoja na machinjio ya Kisakasaka na Muwanda ambapo kamati iliwasilisha kile walichojifunza na kuomba Wizara izidi kuviboresha vituo hivyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.