Habari za Punde

Mama Mwanamwema Shein Azindua Chanjo ya Shingo ya Mlango wa Kizazi.


MKE wa Rais wa  Zanzibar Mama Mwanamwema Shein amesema kuwa kuanzishwa kwa Chanjo mpya ya maradhi ya Saratani ya Shingo ya Mlango wa Kizazi itatokomeza maradhi hayo kama yalivyotokomezwa maradhi mengine hapa Zanzibar.

Mama Shein aliyasema hayo leo huko Skuli ya Dunga iliyopo Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja katika uzinduzi wa Chanjo mpya dhidi ya maradhi ya Saratani ya Shingo ya Mlango wa Kizazi, hafla ambayo imehudhuriwa na viongozi pamoja na wananchi kutoka maeneo mbali mbali.

Katika hotuba yake, Mama Shein alisema kuwa ugonjwa wa ndui uliathiri watu wengi hapa Zanzibar na kupelekea watu wengi kupoteza maisha na wengine kubaki na kovu mpaka kufa kwao lakini kutokana na chanjo ugonjwa huo ulitokomezwa kabisa.

Aliongeza kuwa baadhi ya maradhi kama shurua, pepo punda, donda koo, kifaduro pamoja na polio yalikuwa yakiwasumbua watoto kwa kiasi kikubwa yamepungua kutokana na chanjo ambapo hivi sasa maradhi ya polio yametokomezwa kabisa hapa Zanzibar.

Kwa hivyo, Mama Shein alisema kuwa maradhi ya Saratani ya Shingo ya Mlango wa Kizazi nayo yanaweza kutokomezwa kama yalivyotokomezwa maradhi hayo ukiwemo ugonjwa wa ndui.

Aidha, Mama Shein alisema kuwa lengo la  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa huduma za chanjo ni kuokoa maisha ya wananchi wakiwemo watoto, kwa maradhi ambayo yamethibitika kuwa yanaweza kuzuilika kwa chanjo.

Hivyo Mama Shein aliwashajiisha wanawake wenziwe kuwahamasisha vijana waendelee kujitokeza kwa wingi kwenda kufanikisha zoezi hilo kwa manufaa yao binafsi, wazazi na nchi nzima kwa jumla.

Zanzibar imeweza kupunguza maambukizo ya maradhi ya Malaria ambapo hivi sasa kiwango cha maambukizo kipo chini ya asilimia moja, hivyo anaamini kuwa uzinduzi wa chanjo hiyo kwa Unguja na Pemba ni safari nyengine ya mafanikio ambayo wananchi wa Zanzibar wameanza kwa kujiandaa vizuri.

“Tumuombe Mola wetu atujaalie iwe safari ya salama na ya mafanikio, ili Zanzibar na Tanzania kwa jumla iendelee kuwa mfano bora duniani katika kupambana na maradhi mbali mbali” Juu ya hili mimi sina shaka kutokana na juhudi zinazofanywa na Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dk. Ali Mohamed Shein” ,alisema Mama Shein.

Aidha alisema kuwa wakati jamii inahamasishwa kushiriki katika chanjo ni vyema ikaendelea kutekeleza vyema mikakati na mipango iliyopo ya mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na udhalilishaji wa wanawake na watoto.

Mama Shein alitoa nasaha zake kwa jamii na kutaka itoe ushirikiano kwa vyombo vinavyohusika kwa kuwaripotia watu wanaobainika kufanya vitendo vya aina hiyo ili sheria ichukue mkondo wake.

Pamoja na hayo, Mama Shein alitoa shukurani kwa uongozi wa Wizara ya Afya na wahusika wengine waliofanikisha hafla hiyo sambamba na kulishukuru Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Huduma za Chanjo (GAV), Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa michango yao mbali mbali katika kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapatiwa huduma za chanjo zilizo katika kiwango cha ubora kabisa.

Nae Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed alitoa pongezi kwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya yakiwemo UNFPA, UNICEF na WHO hasa kwa kutambua kuwa chanjo hiyo ni muhimu sana.

Alisema kuwa kazi iliyoko mbele ni kujenga Taifa ambalo lenye afya hivyo alisisitiza haja ya kumtunza mama hasa katika wakati wa ujauzito hadi pale anapozaa kwa kumpa msaada mapenzi na huruma huku akisisitiza matumizi mazuri ya lugha kwa akina mama hao.

Waziri Rashid alisema kuwa Zanzibar imepata mafanikio makubwa kutokana na uchumi wa Zanzibar kukua kwa asilimia 7.5  na kuondokana na utegemezi kutoka asilimia 31 hadi 7 hivi sasa licha ya baadhi ya wanasiasa kufanya kampeni nje ya nchi ili Zanzibar isisaidiwe huku akieleza kuwa hivi sasa kila mfanyakazi wa sekta ya umma amekuwa akipata mshahara si zaidi ya tarehe 25 baada ya nyongeza ya mshahara huo.

Aliongeza kuwa utafiti umefanywa kwa miaka mitano na chanjo hiyo haina tatizo na kuwataka wananchi kuachana na wale wanaosambaza uzushi kuwa chanjo hiyo inawazuia watu kuzaa na kusisitiza kuwa huo ni uzushi na hakuna haja ya kwenda kwa waganga na badala yake waendelee kupata chanjo hiyo na kusisitiza matumizi ya lugha nzuri kwa akina mama kutoka kwa wafanyakazi wa sekta ya afya.

Nae Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Idadi ya Watu Duniani (UNFPA)  Batula Abdia kwa niaba ya Mashirika ya Umoja huo aliahidi kuimarisha mashirikiano na Wizara ya Afya katika kupambana na maradhi mbali mbali huku akisisitiza haja ya jamii kuelimishwa.

Aliongeza kuwa saratani ya Shingo ya Mlango wa Kizazi ni saratani ya pili kwa ukumbwa inayoisumbua jamii ulimwenguni ambapo inakisiwa wanawake wapatao 270,000 wanakufa kila mwaka duniani ambapo asilimia 88 ya wanawake hao wanaishi katika  nchi masikini kama Zanzibar na kusisitiza kuwa chanjo hiyo ni muhimu sana na uwekezaji bora kwa Zanzibar.
Mapema Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya, Dk. Mohamed Dahoma akitoa maelezo ya kitaalamu alisema kuwa chanjo hiyo ina madhumuni ya kusaidia kupambana na kasi ya uendeleaji wa  maradhi ya saratani ya shingo ya mlango wa kizazi.

Aliongeza kuwa maradhi hayo yanayosababishwa na virusi kwa njia ya kujamiiana ambapo kwa asilimia 70 ya watu duniani wanatembea wakiwa na virusi hivyo kwa wanawake na wanaume ambapo wapo wanaoonesha dalili na wasioonesha dalili na uzuri wake ni kuwa virusi hivyo tayari vimepatiwa chanjo.

Alisema kuwa kwa hapa Unguja saratani hiyo ni miongoni mwa saratani mbili zinazoongoza ikiwemo saratani hiyo ya shingo ya mlango wa kizazi na ile ya matiti na kusema kuwa vijana watakaochanjwa ni wale wa kuanzia miaka 14 ambapo mwaka huu watachanjwa vijana 20815 kupitia skuli na katika vituo wakiwemo na wale kutoka mitaani.

Serikali kupitia kwa Wizara ya Afya imefanya mikakati mingi sana kuleta chanjo tangu mwaka 1981 ambapo vituo vyote 175 vilivyopo Zanzibar vitaendelea kutoa chanjo na hivi sasa chanjo zimeongezeka ikiwemo, kuharisha, kichomi,homa ya ini, uti wa mgongo ambapo lengo kuu ni kutoa kinga kwa watoto ambao wengi wao wanazaliwa wakiwa hawawezi kupambana na maradhi.

Alisema kuwa Kimataifa zoezi hilo litaanza tarehe 23 hadi 26 Aprili ambapo Wizara ya Afya kwa hapa Zanzibar itaendelea kushajiisha na kuielimisha jamii ili watu wote wawe na uwelewa wa chanjo hiyo hadi muda huo utakapofika ambapo wanaamini kuwa wananchi watakuwa  wamepata uwelewa mzuri huku akieleza kuwa ujumbe mkuu wa chanjo hiyo ni “Jamii iliyochanjwa  ni jamii yenye afya”.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.