Habari za Punde

Balozi Seif ziarani Pemba

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali wa Pili kutoka Kulia akipokea Maelezo kutoka Maafisa wa Ofisi ya Idaya ya Mazingira pamoja na Mamlaka ya Mazingira Macho Mane Chake Chake Pemba akiwa katika zaiara ya siku Tatu Kisiwani humo.
Kulia ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Mihayo Juma N’hunga.
 Mkuu wa Ofisi Ndogo ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar  {ZEC} Chake chake Pemba Nd. Ali Mohamed akimpatia maelezo Balozi Seif aliyefika Ofisini hapo.
 Kamanda wa Kitengo cha Ufundi wa Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar {KMKM} CDR – Hamad Masoud Khamis akimpatia maelezo Balozi Seif  juu ya kukamilika kwa ujenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Kikosi hicho kilichojengwa pembezoni mwa Bandari ya Mkoa Kisiwani Pemba.
Balozi Seif akizungumza na Wananchi wa Kaya Maskini wa Mjini Wingwi alipotembelea Shamba Darasa linalowahusisha Wananchi hao juu ya ukulima bora wa Kilimo cha Tungule, Vitunguu na Alizeti.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kumuongezea ujuzi Mfanyakazi wake popote kama ilivyofanya kwa wale ambao kwa sasa wameshamaliza masomo na wanawajibika vyema katika kulitumikia vyema Taifa.
Alisema Serikali inaona fahari na kupata faraja pale inapokuwa na Wafanyakazi weny Ujuzi na taaluma kubwa ya kukidhi mahitaji ya Watendaji wenye kiwango kinachokidhi mahitaji yote ya Utumishi wa Umma.
Balozi Seif Ali Iddi alisem hayo wakati akizungumza na Watendaji wa Idara na Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake Kisiwani Pemba hapo katika Ukumbi wa Tasaf baada ya kufanya ziara ya kutembelea Taasisi hizo zikiwemo pia zile zilizohamishiwa kwenye Ofisi hiyo kufuatia mabadiliko ya hivi karibuni.
Alisema atamuagiza Katibu Mkuu kuangalia yule Mfanyakazi aliyetayari kutitumia fursa hiyo na anavigezo kamili vya kuendelea na masomo katika ngazi ya juu anaandaliwa mazingira ya haraka kwa ajili ya kuwezesha kupata nafasi hizo muhimu.
“ Mfanyakazi ye yote mwenye vigezo vinavyokubalika kwa ajili ya kuendelea na masomo ya ngazi ya juu kamwe asione shida kwa kujipatia fursa hiyo”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pilinwa Rais wa Zanzibar alielez kwamba Tanzania pekee tayari imeshabarikiwa kuwa na vyuo vingi vinavyotoa Elimu ya juu na kufikia hata ngazi ya Shahada ya Udaktari ambayo Watumishi wa Umma wenye vigezo kamili wanaweza kuichangamkia.
Balozi Seif Ali Iddi aliwasisitiza Watendaji walio chini ya Ofisi yake Kisiwani Pemba waendelee kufanyakazi kwa ushirikiano ili kila Mmoja miongoni mwao ajione kwa mwenzake kama ni ndugu yake hali itakayolea upendo na furaha kwao na hata muingiliano wa familia zao.
Hata hivyo Balozi Seif  aliwapongeza Viongozi na Watendaji wa Taasisi hizo kwa kufanya kazi kwa bidii na nidhamu iliyopelekea Wananchi walio wengi Kisiwani Pemba kuridhika na huduma zinazosimamiwa na Watendaji hao.
Alisema Serikali wakati huu ikiendelea kupiga vita Dawa za kulevya sambamba na mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa Kijinsia mambo ambayo Viongozi bado wana wajibu wa kuendelea kutoa elimu kwa Wananchi jinsi ya kuondosha majanga hayo Mawili.
Balozi Seif alisisitiza kwamba vitendo hivyo viwili vinavyoonekana kuendelea kulitia aibu Taifa vinarudisha nyuma ustawi wa Wananchi hasa Vijana kiasi kwamba Taifa linapunguza nguvu Kazi inayoitegemea kutoka kwa Kundi hilo.
Mapema Afisa mdhamini Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ndugu Ali Salim Mattar alisema stahiki za Watendaji wa Ofisi hiyo zinazopatikana  kwa wakati ni uthibitisho wa Uwajibikaji wa Serikali katika kuwajengea mazingira bora Watumishi wake wa Umma.
Nd. Mattar alisema hatua hiyo imepelekea Watendaji hao kuendeleza ushirikiano wa karibu ambao umezaa matumaini mema ya uwajibikaji hasa katika kuhamasisha  uhifadhi wa Mazingira na Tabia Nchini kutekelezwa kwa asilimia kubwa zaidi.
Alisema yapo mafanikio ya wazi yanayoshuhudiwa miongoni mwa Wananchi ambayo husimamiwa na Taasisi na Vitengo vya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Kisiwani Pemba akaitolea mifano miradi inayopata ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF}.
Nd. Mattar alieleza kwamba zipo ajira za muda 216 za Wananchi wa Kaya Maskini zilizopatikana kutoka Shehia 78 Kisiwani Pemba zilizotokana kupitia vikundi vya ushirika pamoja na matengenezo ya Matuta Matano ya kuzuia Maji ya Chumvi.
Mapema Balozi Seif Ali Iddi alitembelea Ofisi ya Mazingira Machomane, Ofisi ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Tibirinzi, Ofisi Ndogo ya Tume ya Uchaguzi Chake Chake, Jengo Jipya  la Mafunzo la Kikosi cha Kuzuia Magendo Mkoani, Bara bara iliyojengwa na Wananchi wenyewe kwa kutumia vifaa vya kawaida ya Kijiji cha Wingwi.
Miradi mengine aliyoikagua ni maendeleo ya Ujenzi wa Hanga la Kikosi cha Kuzuia Magendo {KMKM} liliopo katika Kijiji cha Likoni Chwale pamoja na Shamba Darasa la Mjini Ole.
Akizungumza na Wananchi pamoja na Wakulima wa Bonde hilo huku Mvua za Masika zikiendelea Makamu wa nPili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema nia ya Serikali kuanzisha mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} ni kuwakomboa Wananchi na Umaskini.
Balozi Seif alisema kwa Vile Wananchi tayari wamejikita katika uzalishaji ipo haja kwao kuwa makini katika kuitunza Miradi waliyoianzisha ili iendelee kustawisha Maisha yao kwa kuongeza kipatoa itakachowawezesha kukimu hahitaji yao ya msingi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea faraja yake kutoka na Miradi iliyoanzishwa na kupata msukumo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} inaenda vizuri kiasi kwamba Makao Makuu ya Mfuko huo yameisifia Zanzibar kwa kupata mafanikio makubwa kwenye miradi hiyo.
Akitoa Taarifa fupi Mratibu wa TASAF Kisiwani Pemba Nd. Mussa Said Kisenge alieleza kwamba zipo ajira za muda zilizopatikana kupitia Miradi ya ujenzi wa Bwawa la uhifadhi wa Maji ya Mvua yanayotumiwa kwenye Kilimo na Mifugo pamoja na shamba Darasa linalohudumia Kaya Maskini kutoka Shehia 78.
Nd. Mussa alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba  shamba hilo Darasa limelenga kutoa mafunzo ya ukulima wa kisasa wa kilimo cha Alizeti, Vitunguu na tungule ili baadae Wakulima hao waweze kujiendesha wenyewe katika Maisha yao ya baadae.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.