Habari za Punde

Tume ya Taifa Kuratibu na Uthibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar Yateketeza Dawa za Kulevya.


Askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi wakichoma moto vipolo na vifushi vya bangi katika jaa la Kibele Mkoa wa Kusini Unguja. 
Mwanasheria kutoka Tume ya Taifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Juma Abrahman Zuheri akihakiki vipolo vya dawa za kulevya aina ya bangi katika Mahkama ya Mwera kabla ya kwenda kuangamizwa katika jaa la Kibele Mkoa Kusini Unguja.

Na. Miza Kona -Maelezo Zanzibar.  15/05/2018
KAMATI ya kuangamiza dawa za kulevya imeangamiza zaidi ya polo 35 za dawa za kulevya aina ya bangi katika jaa la kibele, Wilaya ya Kati Unguja.
Dawa hizo zilikamatwa kuanzia mwaka 2009 hadi 2016 zilikuwa ni vielelezo vya ushahidi katika mahkama na vituo vya polisi vya unguja na kesi zake  zimemalizika na kutolewa hukumu.
Mwenyekiti wa kamati ya kuangamiza dawa za kulevya  ambae pia  ni Mkurugenzi wa Mashtaka  Ibrahim Mzee alisema zoezi hilo limefanyika kwa mujibu wa sheria na kanuni ya mwaka  2009.
Amesema zoezi la kuangamiza dawa za kulevya linafanyika kwa utaalamu na utaratibu maalumu kwa vile haitakiwi kuchanganya aina tofauti za dawa za kulevya.
Amesema kamati yake imeanza kuangamiza bangi na baadae watafanya zoezi jengine  la kuangamiza aina nyengine ya dawa za kulevya ikiwemo heroin na cocaine.
Naibu katibu mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Abdalla Hassan  Mitawi amesema kuwepo kwa sheria ya dawa za kulevya itasaidia kupunguza ongezeko la waingizaji wa dawa hizo nchi kwani sheria hiyo inaweza kumtia hatiani hata muingizaji alioko nje ya nchi.
Mkuu wa kitengo cha Dawa za Kulevya kutoka Jeshi la Polisi, Omar Khamis Abdalla amesema kesi zilizopo mahkamani zinazohusiana na dawa za kulevya zinashughulikiwa na ameitaka jamii kuwa na imani na vyombo vya sheria kwa kutekeleza vyema majukumu yake.
 IMETOLEWA IDARA YA HABARI MAELEZO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.