MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza
kuwa uchumi wa Zanzibar umeendelea kuimarika kutokana na uongozi thabiti wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku akisisitiza kuwa hatokuwa na msamaha kwa yeyote
atakaebainika kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.
Dk. Shein ambaye pia, ni
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyasema hayo katika
ukumbi wa ‘Jamhuri Hall’ huko Wete wakati
alipokuwa akizungumza na Mabalozi wa Wilaya ya Wete katika Mkoa wa Kaskazini
Pemba.
Aliongeza kuwa uchumi wa
Zanzibar umezidi kuimarika kwa kiasi kikubwa na kutumia fursa hiyo kuendelea kusisitiza
kauli yake aliyoitoa katika maadhimisho ya kilele cha Mei Mosi mwaka huu kwa wale
wote wanaodiriki kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.
Makamo Mwenyekiti huyo
wa CCM Zanzibar alieleza jinsi Zanzibar ilivyokuwa na uwezo mkubwa wa kifedha
na uchumi hatua iliyompelekea kuongeza mishahara mara nne katika uongozi wake
sambamba na kuimarikaka kwa sekta za maendeleo.
Dk. Shein aliendelea
kusisitiza kauli yake kuwa ataendelea kuiongoza Zanzibar kwa uadilifu mkubwa na
kusisitiza kuwa viongozi wote walioteuliwa wanatekeleza Ilani ya CCM.
Katika maelezo yake,
Rais Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuwa ujenzi wa Chuo cha amali cha Daya-Mtambwe
utaanza hivi karibuni pamoja na ujenzi wa barabara ya Finya-Kicha itakayojengwa
kwa kiwango cha lami sambamba na kuzitafutia ufumbuzi changamoto nyengine
walizoziorodhesha.
Akiwaeleza wajibu wao kwa
mujibu wa Katiba ya CCM, Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao wajijue kuwa wao ni
Wenezi na Wahamasishaji wakuu wa CCM pamoja na kuwa na wajibu wa kuwaeleza
wanachama katika maamuzi yote ya CCM na kufikisha mapendekezo ya wanachama
katika vikao vya juu.
Alisema kuwa WanaCCM wote
wakiwemo viongozi hao wana kazi kubwa ya kufanya katika kusaidia ushindi wa CCM
na kila mmoja kwa ngazi yake kwa namna yake na kuwa na wajibu wa kufanya yeye
mwenyewe kwa uwezo wake kusaidia ushindi huo.
Aidha, alisisitiza kuwa
ushindi kwa CCM ni suala la lazima kutokana na maelekezo ya Katiba ya chama
hicho na hakuna mbadala wa ushindi kwa kufuata taratibu na namna zote za
kidemokrasi kwa lengo la kuyalinda
Mapinduzi ya Januari 12,1964 pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisisitiza haja ya
kupambana na udhalilishaji wa kijinsia kwa watoto na wanawake na kuwataka
wananchi wote kuzingatia maadili ya Kizanzibari.
Aliongeza kuwa Zanzibar
imeimarika kwa kiasi kikubwa na sio ile ya mwaka 1964 na imebadilika kwa kila
hali sambamba na kuongezeka kwa idadi ya watu hali iliyotokana na kuwepo kwa
amani na utulivu pamoja na chakula cha kutosha kwa watu wake.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa
CCM Zanzibar, Abdalla Juma Mabodi alieleza kuwa ziara ya Dk. Shein ya kukutana na Mabalozi
wote wa Zanzibar ni shemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM huku
akitumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa Mabalozi, Mashina na Matawi yake.
Naibu Katibu Mkuu huyo
wa CCM Zanzibar pia, alitumia fursa hiyo kueleza jinsi ya hatua mbali mbali
zinazochukuliwa na Chama hicho kupitia Mabaalozi wake na kusisitiza azma
walyokusudia ya kuwafuatilia Wawakilishi ni kwa vipi wanazitumia fedha za mfuko
wa Jimbo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa
wa Kaskazini Pemba Mberwa Hamad Mberwa alieleza juhudi kubwa zinazochukuliwa na
Mabalozi hao pamoja na viongozi wote wa Chama hicho katika Wilaya ya Wete.
Katika risala ya
Mabalozi wa Wilaya ya Wete iliyosomwa na Balozi Ali Khamis Ali ilieleza utekelezaji wa Ilani ni wenye
mafanikio makubwa hasa kwenye maeneo ya huduma za jamii kama vile Maji safi na
salama, Afya, Elimu, Miundo mbinu, Biashara, Viwanda pamoja na sekta
nyenginezo.
Aidha, walitoa shukurani
zao na kumpongeza sana kwa kushirikisns nso kstiks uzinduzi wa umeme katika
Kisiwa cha Fundo.
Sambamba na hayo,
Mabalozi hao wamempongeza Dk. Shein kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi asilimia
mia moja katika Mkutano Mkuu wa CCM Taifauliofanyika mwishoni mwa mwaka 2017.
Pia, Mabalozi hao
walimuomba Dk. Shein kuwapelekea salamu zao kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kwa
asilimiamia moja katika Mkutano Mkuu wa CCM Taifa na kumpongeza kwa kazi nzuri
anayofanya.
Dk. Shein amemaliza
ziara yake ya kukutana na Mabalozi wa Wilaya zote za Kisiwani Pemba ambapo
kuanzia kesho anatarajiwa kuendelea na ziara zake za kukutana na Mabalozi wa
Wilaya za Unguja ambapo pia, katika ziara hiyo Mama Mwanamwema Shein alishiriki
kikamilifu.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment