Habari za Punde

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed Azindia Mkoba wa Mama Mzazi Zanzibar.Utakaotolewa Bure Kwa Mazazi Anapojifungua.

Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa Mkoba wa Vifaa vya Mama Mzazi katika sherehe zilizofanyika katika Viwanja vya Wizara ya Afya Mnazi Mmoja Mjini Zaznibar aliekamata Mkoba huo ni Muuguzi Dhamana Hospitali ya Mnazi Mmoja Nasra Ishaka.
WAZIRI wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akionesha aina ya Mkoba, anaotakiwa kupewa Mama Mzazi atakaefika katika Kituo cha Afya cha SMZ (BURE) kwaajili ya kujifungua Mtoto (kushoto) Mkurugezi Kinga na Elimu ya Afya Dkt. Fadhil Mohammed Abdalla,(kulia) Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Halima Maulid Salum.
MWAKILISHI Kutoka Mashirika ya Umoja wa Mataifa Mariam Seif Hemmed akizungumza katika sherehe  za Uzinduzi wa Mkoba wa Vifaa vya Mama Mzazi zilizofanyika katika Viwanja vya Wizara ya Afya Mnazi Mmoja Mjini Zaznibar.
MWAKILISHI wa Bohari ya Dawa Tanzania ( msd) Marco Masalo akizungumza katika sherehe  za Uzinduzi wa Mkoba wa Vifaa vya Mama Mzazi zilizofanyika katika Viwanja vya Wizara ya Afya Mnazi Mmoja Mjini Zaznibar.

BAADHI yaWafanyakazi wa Wizara ya Afya Zanzibar waliohudhuria katika sherehe  za Uzinduzi wa Mkoba wa Vifaa vya Mama Mzazi zilizofanyika katika Viwanja vya Wizara ya Afya Mnazi Mmoja Mjini Zaznibar (Picha na Abdalla Omar - Maelezo  Zanzibar)

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar.22.6.2018
Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohammed amevitaka vitego vilivyomo ndani ya Wizara hiyo kuweka mahitaji sahihi ya dawa ya mwaka kwani dawa za kutosha zipo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Amesema Serikali imeongeza Bajeti ya kununua dawa kutoka shilingi bilioni saba mwaka unaomalizika kufikia shilingi bilioni 12.7 mwaka 2018/2019 na hakutakuwa na upungufu wa dawa katika Hospitali na vituo vyote vya afya Zanzibar.
Waziri Hamad ametoa agizo hilo Wizarani kwake Mnazimmoja alipokuwa akizindua Mkoba wa Vifaa vya mama mzazi ambao utatolewa bila malipo kwa wajawazito wanaofika Hospitali na Vituo vya afya kujifungua.
Amesema vifaa hivyo vitasambazwa katika Hospitali na vituo vyote vya afya vinavyotoa huduma ya kuzalisha na amewashauri mama wajawazito kuitumia fursa hiyo kujifungua katika vituo vilivyokaribu nao.
Waziri wa afya amewasisitiza wananchi wasikubali kununua mikoba hiyo kwani inatolewa bure na iwapo akitokea mfanyakazi wa kituo cha afya akitaka kuwauzia watoe taarifa ili kuchukuliwa hatua.
Amewaagiza viongozi wa Wizara hiyo kusimamia nidhamu ya kazi ili kuongeza ufanisi na kusimamia matumizi bora ya dawa na kuhakikisha zinawafikia wananchi.
Amekemea tabia ya baadhi ya Madaktari kuwaandikia dawa wagonjwa ambazo hazipo kwenye vituo ili wakanunue wakati dawa nyengine mbadala wa matatizo yao zipo na ametaka tabia hiyo waiache kwani haileti tija .
“Madaktari andikeni dawa sahihi zinazopatikana katika Hospitali na vituo vya afya ili kuwasaidia wananachi wetu, kwa kweli mnakatisha watu tamaa, ” alisema Waziri Hamad Rashid.
Aidha Waziri wa Afya amewataka akinababa kushirikiana na wake zao katika suala la uzazi wa mpango kwa lengo la kulinda afya ya mama na mtoto alisisitiza afya ya mtu ni jambo la msingi.
Mkurugenzi wa Kinga Dkt. Fadhil Abdalla aliweka bayana kuwa  idadi ya mama wajawazito wanaojifungua katika vituo vya afya imeongezeka lakini bado haijaridhisha hivyo amewashauri kujenga tabia ya kwenda vituoni tokea hatua za awali kupata ujauzito hadi kujifungua.
Amewahakikishia wananchi kuwa mikoba hiyo itapelekwa pia katika vituo vya afya vya binafasi vinavyotoa huduma ya kuzalia kwa masharti kuwa wataitoa bure  kama inavyotolewa katika vituo vya Serikali.
Mwakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Maryam Seif Hemed aliahidi kuwa wataendelea kushirikiana na kuunga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha huduma za mama na mtoto zinaimarika.
Hata hivyo alitoa wito kwa Wizara ya Afya kuhakikisha inaweka mikakati ya kuvitunza vifaa tiba na kuviondosha vilivyoharibika kwenye vituo vya afya ili kulinda afya za wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.