Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Aendelea na Ziara Yake Kisiwani Pemba kwa Kukabidhi Misaada.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwasili katika Hospitali ya Micheweni Pemba kukabidhi msaada wa vifaa uliotolewa na Mfanyabiashara Maarufu Zanzibar Said Nasser Nassor Bopar.
Mfanyabiashara Said Nasser Nassor Bopar akimkabidhi Balozi Seif  Mashine ya Uchunguzi wa Maradhi ya Tumbo {ULTRASOUND} kwa ajili ya Hospitali ya Micheweni.
Balozi Seif akizungumza na Wafanyakjazi wa Hospitali ya Micheweni na Wananchi wahapo pichani katika hafla fupi ya kukabidhi msaada wa vifaa mbali mbali kwa ajili ya Hospitali hiyo
Balozi Seif akiangalia vifaa katika Chumba Maalum cha Upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Micheweni mara baada ya kukabidhi msaafa wa vifaa tofauti Hospitalini hapo.
Balozi Seif akiwakagua baadhi ya Wagonjwa waliolazwa katika wodi za Hospitali ya Wilaya ya Micheweni mara baada ya kukabidhi msaada wa vifaa tofauti Hospitalini hapo.
Mfanyabiasha Maarufu Nchini Said Nasser Nassor Bopar akitoa zawadi mbali mbali kwa wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Micheweni kwa ajili ya kujiandaa na Siku Kuu ya Iddi el Fitri.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akitoa zawadi mbali mbali kwa wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Micheweni.
Mfanyabiashara Said Nasser Nassor Bopar akimkabidhi Balozi Seif  Meza 104 na Viti 213 kwa ajili ya Skuli ya Msingi ya Micheweni iliyomo ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.  Picha na – OMPR –ZNZ.

Na. Othman Khamis OMPR.
Makamu  wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, amesema Sekta ya elimu linahitaji mchango mkubwa kutoka kwa wahisani, Taasisi na Mashirika ya Kijamii pamoja na Wananchi Wazalendo kwa vile Serikali pekee haiwezi kukamilisha jukumu hilo kwa wakati mmoja.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Kamati iliyoiunda inaendelea na mchakato wa kuondosha tatizo la uhaba wa Vikalio katika Maskuli yake Unguja na Pemba linalohitaji kuungwa mkono na Taasisi nyengine ambapo makadirio halisi ya vikalio hivyo inafikia Madeski 45,000.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika viwanja vya shamemata micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba wakati alipokuwa akikabidhi madawati  104 na viti 208 vya kukalia, kwa skuli ya msingi  ya Micheweni Mkoa Kaskazini Pemba vilivyotolewa na Mfanya biashara maarufu Zanzibar Said Nasser Nassor {Bopari}.
Alisema Serikali inajitahidi kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo la vikalio Unguja na Pemba ili kuwajengea mazingira mazuri ya Kielimu wanafunzi wanaopaswa kufahamu jitihada zinazoendelea kufanywa  na Serikali kwa ajili yao.
Akimpongeza Mfanyabiashara Said Bopar kwa msaada wake huo mkubwa katika Sekta ya Elimu Balozi Seif aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika masomo yao, kwani elimu ndio kitu muhimu katika maisha ya Mwanaadamu.
“ Hivi sasa Kiwango cha elimu kimepanda tofauti na Karne ya 20, leo karne ya 21 Chuo kikuu kinazalisha kundi kubwa la wasomi hadi kufikia Shahada ya juu katika suala zima la elimu”alisema Balozi Seif.
Aliwanasihi wanafunzi Nchini kuzingatia zaidi masomo yao badala ya kuvamia mambo yanayoweza kuvuruga msingi wao mzima wa Kitaaluma unaohitaji maandalizi ya msingi yatakayojenga fursa za ajira zisizoshaka.
Akigusia jukumu la wazazi Balozi Seif aliwata kufuatilia maienendo ya watoto wao, ili hatimae kuzalisha wataalamu wa fani mbali mbali ikiwemo masomo ya sayansi yenye kustawisha Uchumi wa Taifa.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Taifa linahitaji kuwa na Wataalamu wake wenyewe  na kuacha tabia ya kutafuta walimu wa masomo hayo kutoka nje ya nchi ikiwemo Nigeria.
“ Serikali inahitaji walimu wa masomo ya sayansi ni wakati sasa kuekeza kwa vijana hawa, ili tupate wataalamu mbali mbali wa sayansi na kuacha kuagizia kutoka nje ya nchi”alisema Balozi Seif.
Akizungumzia suala la michango maskulini, Balozi Seif aliwanasihi walimu kuacha tabia ya kuwachangisha fedha wanafunzi, kwa vile serikali tayari imeshatangaza elimu bila ya Malipo ili Wananchi waridhike na faida ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Mapema Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Mmanga Mjengo Majawiri, aliwataka walimu na wanafunzi wa skuli ya Micheweni kuhakikisha wanavitunza na kuvithamini vifaa walivyopatiwa.
Mh. Mmanga alisema Wizara ya Elimu kupitia Sera yake tayari imeshaanda Mpango Maalum wa kuvitunza Vifaa vyote vilivyomo Maskulini kwa lengo la kutoa huduma kwa muda mrefu zaidi.
Akigusia upungufu wa Walimu katimka Wilayaya Micheweni Mh. Mmanga Mjengo Mjawiri aliwahakikishia Wananchi, Walimu na Wanafunzi wa Wilaya hiyo kwamba Wizara hivi sasa imepanga kuwatanguliza Walimu 37 kwenye Skuli zilizomo Wilayani humo ili kupunguza upungufu huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mapema asubuhi akikabidhi Msaada wa vifaa kwa uongozi wa hospitali ya Micheweni vilivyotolewa pia na Mfanyabiashara huyo Maarufu BwanA Said Nasser Nassor {Bopar}.
Vifaa alivyokabidhi Balozi Seif ni pamoja na mashine ya uchunguzi wa maradhi ya Tumbo {Ultrasound}, vitanda 20, mashuka 20, mito 20, Blangeti 20 pamoja na sabuni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliutaka uongozi wa Wizara ya Afya Pemba pamoja na Watendaji wa hospitali hiyo, kuvifanyia kazi vifaa hivyo kwa kuwahudumia wananchi wa micheweni pamoja na wale wa Mikoa mengine watakaohitaji huduma hizo.
Alionya kwamba hivyo ni vifaa vilivyotolewa kwa ajili ya Hospitali ya Micheweni na kuwasihi madaktari kuepuka ushawishi wa udokozi unaoibuka kwa baadhi ya watendaji hao wakiwa na nia ya kukatisha huduma hizo ili zihamie kwenye Hospitali binafsi wanazofanyia kazi katika muda wa ziada.
Balozi Seif alimshukuru na kumpongeza mfanya biashara Said Nassir Nassor (Bopari) kwa uamuzi wake wa kuendelea kuisaidia Sekta mbali mbali ikiwemo Sekta ya Afya, ambayo ndio sekta muhimu katika nchi.
Katika mazungumzo yake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitahadharisha kwamba si vyema kwa Watumishi wa Umma wakiwemo Madaktari na Walimu  wakaielekeza Jamiikatika masuala ya Kisiasa.
Alisema Jamii imeshuhudia Familia moja imekuwa na Watu waliotofautiana kiitikadi jambo ambalo haipendezi kuitumia nafasi hiyo kwa lengo la kuwafarakanisha.
Kwa upande wake Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba Shadiya Shaban Seif, alimshukuru Mfanyabiashara Said Nasser Nassor {Bopari} kwa msaada wake na kusema kuwa umefika kwa wakati muwafaka katika hospitali hiyo.
Hata hivyo aliwataka wafanya biashara wengine kujitokeza kwa hali na mali kusaidia vifaa mbali mbali vya Hospitali, kwa vile  huduma za afya ni muhimu zinazohitajika kila mara kwa jamii.
Akitoa shukrani za Wananchi wa Micheweni Mwakilishi wa Jimbo hilo ambae pia ni Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara maalumu za SMZ, Shamata Shaame Khamis alisema jimbo la Micheweni hivi sasa limepiga hatua kubwa kimaendeleo.
Mh. Shamata alisema hatua hiyo inatokana na jitihadakubwa zilizochukuwa na Serikali ya Mapinduzi y Zanzibar chini ya  Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Pili Balozi Seif wanaohakikisha maendeleo yanafika kwenye eneo yote Nchini.
Akimkaribisha Balozi Seif  kuzungumza na Wananchi wa Micheweni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Omar Khamis Othman, aliwataka madaktari kuhakikisha wanavitumia ipasavyo vifaa hivyo, ili kuwapunguzia mzigo wananchi wa micheweni katika kufuata huduma za Afya wete na Chake Chake.
Alisema kukabidhiwa kwa mashine hiyo ya Ultrasound katika hospitali ya Micheweni, itaweza kutoa huduama ipasavyo, huku akiwataka kuhakikisha wanaitunza na kuithamini ili idumu kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.