Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapnduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akiwahutubia Waislam katika Ukumbi wa Sheikh.Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar wakati wa Baraza la Eid El Fitry, baada ya kumaliza Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan,
RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein
amewataka wananchi kuzingatia suala la kuendeleza malezi bora ya watoto kwa
mujibu wa maadili, silka na utamaduni ulioachwa na wazee.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hotuba
yake ya Baraza la Idd al Fitri aliyoitoa huko katika ukumbi wa Sheikh Idrisa
Abdul Wakil, Kikwajuni Mjini Zanzibar, ambapo hafla hiyo ilihudhuriwa na
viongozi mbali mbali akiwemo Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd,
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein na viongozi wengine wastaafu.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa
hivi sasa malezi yamekuwa yana mtihani kwani kila mzazi amekuwa akiishi na
mwanawe wakati hapo zamani watoto hulelewa na kiambo au mtaa mzima na kila mzee
katika mtaa alikuwa ni mzee wa watoto wote na walitakiwa wamuheshimu na wamtii.
Alhaj Dk. Shein alisema kuwa utamaduni huo
ulisaidia sana watu kuheshimiana na kuwapa usalama watoto katika mitaa, hata
pale wazazi wao wanapokuwa hawapo.
Kwa hivyo, Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa wazazi na
walimu wana wajibu wa kushirikiana katika kuhakikisha kwamba jamii inapata
mustakabali mwema.
Alieleza kuwa miongoni mwa jitihada za kuhakikisha
kwamba wananchi wanatimiza wajibu wao katika kuzingatia mpango wa miaka mitano
wa kupambana na unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia wazazi na walezi wote
inawalazimu kuongeza nguvu na kushirikiana katika malezi ya watoto wao.
“Ili tuweze kushinda vita vya unyanyasaji na
udhalilishaji wa kijinsia, lazima kila mmoja wetu atimize wajibu wake kwa
kuzingatia mpango wa miaka mitano wa kupambana na unyanyasaji na udhalilishaji
wa kijinsia ambao tuliuzindua mwezi wa Agosti mwaka 2017…naiagiza Wizara ya
Kazi, uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto kulishaughulikia suala hilo”,alisema
Dk. Shein.
Aidha, alilitaka Jeshi la Polisi, Ofisi ya
Makurugenzi wa Mshtaka na Mahakama nazo kuendelea kuyatekeleza majukumu yao
vizuri ili kesi za udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia ziweze kusikilizwa
kwa haraka.
Dk. Shein aliwaasa wazazi na walezi kwamba linapotokezea
kosa la udhalilishaji ambalo limefanywa na mtu wa familia, hawapaswi kulitolea
hukumu na kulimaliza kifamilia kwani wanapoamua hivyo wanadhoofisha jitihada za
Serikali na kuyaendeleza maovu.
Aliongeza kuwa katika jitihada za kuwajengea
watoto misingi imara ya maisha yao ya baadae ni kuimarisha ustawi wao na
kuwaandaa kuwa raia wema wenye elimu, maarifa na uwezo wa kukabiliana na
mabadiliko ya karne ya 21.
Rais Dk. Shein alieleza hatua zilizochukuliwa na
Serikali anayoiongoza katika kuhakikisha elimu ya msingi na sekondari inatolewa
bure kwa lengo la kutekeleza dhamira ya Mapinduzi matukufu ya 1964 kwa misingi
iliyoasisiwa na Marehemu Mzee Abeid Karume.
Alieleza kuwa katika kuona kuwa watoto hasa wa
Skuli za Sekondari wanapata mazingira mazuri ya kusoma, Serikali imeiagiza Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Amali ilifanyie kazi suala la kuziendeleza huduma za
dakhalia kwa ukamilifu.
Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali
itahakikisha kwamba huduma za dakhalia zinaendelezwa na zinafanikiwa kwani
huduma hizo mbali ya kuwapa wanafunzi muda mzuri wanapata utulivu wa
kushughulikia masomo yao na wazazi wanapata utulivu kwa kujua kwamba watoto wao
wanaishi katika mazingira salama.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliwataka wafanyakazi
wenzake walioko katika ajira kuwa ni wajibu kuithamini na kuishukuru neema ya
kupata ajira kwa kutekeleza dhamira na majukumu yao kwa misingi ya uadilifu.
Aliwataka kuzilinda na kuziheshimu mali za umma na
sehemu zao za kazi huku wakitambua kwamba wenzao hivi sasa wana mahitaji ya
kutaka kufanya kazi, ili wawe wafanyakazi kama wao lakini bado hawajapata
nafasi ya kuajiriwa.
Alitoa pongezi kwa wananchi kwa kuzingatia
maelekezo ya wataalamu wa afya katika kukabiliana na kujikinga na maradhi ya
miripuko na kudumisha usafi huku akieleza jinsi Serikali ilivyoongeza bajeti ya
afya ya TZS bilioni 12.7 kwa mwaka 2018/2019
kutoka TZS bilioni 7.0 za mwaka 2017/2018 sawa na ongezeko la asilimia
81.4.
Pia, alitumia fursa hiyo kuwataka wafanyakazi kuyaendeleza
mafunzo ya Ramadhani kwa kuendelea kuwa wakweli, waadilifu, wastahamilifu na
kuwa wakinaifu huku Serikali yao ikiendelea kuwachukulia hatua wale wote
wanaoendelea na vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na wanaoshindwa
kusimamia dhamana walizopewa.
Mapema, Alhaj Dk.
Shein aliungana na wananchi katika Sala ya Idd-El-Fitri huko Katika viwanja vya
Maisara Suleiman mjini Zanzibar ambapo viongozi mbali mbali walihudhuria katika
ibada hiyo, huku waislamu wakitakiwa kuwa wachamungu na kuyatumia vyema mafunzo
ya Ramadhan.
Wakati huo huo, Rais Dk. Shein aliungana na
viongozi, Masheikh na Maulamaa waliofika Ikulu Mjini Zanzibar kwa ajili ya
kusalimiana na kutakiana kheri ya Sikukuu ya Idd el Fitr ambapo Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kueleza haja ya kuendeleza umoja na mshikano.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alitoa mkono wa Idd
kwa wananchi wote waliofika katika viwanja vya Ikulu ya Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment