Habari za Punde

Jeshi la Polisi Kufanya Operesheni Kali Katika Visiwa Vya Ziwa Viktoria.


Na. Jeshi la Polisi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro amesema Jeshi hilo litafanya Operesheni kali ya kupambana na wahalifu katika maeneo ya Visiwa vilivyopo katika ziwa Viktoria ili kuhakikisha kuwa wavuvi wanafanya kazi zao bila woga wala hofu ya kufanyiwa uhalifu.

IGP Sirro ameyasema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Kata za Kagongo, Nyasaungu na Kiriba ambazo zipo katika Visiwa vilivyopo Ziwa Viktoria Mkoani Mara wakati wa ziara yake inayoendelea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa lengo la kubaini changamoto za kiuhalifu na kuzipatia ufumbuzi wa haraka ili wananchi waendelee kufanya kazi zao kwa Amani na utulivu.

Amesema Jeshi hilo limejipanga ipasavyo kuhakikisha kuwa kila mwananchi anafanya kazi zake salama kwakuwa uwezo na nguvu wanayo na ndio maana uhalifu unaendelea kupungua hapa nchini.

“Uhalifu wa kutumia silaha ndugu zangu umepungua kwa kiasi kikubwa kwaiyo hata hao wanaotujaribu huko ziwani nawapa salamu waache mara moja kabla ya moto mkali haujawafikia mana hatuna mchezo tunapokutana na mhalifu hususani anayetumia silaha” Aisema Sirro.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kiriba Msendo Nyamsora alimweleza IGP kuwa tatizo kubwa linalowasumbua ni baadhi ya wahalifu ambao wanadaiwa kutoka nchi jirani za Uganda na Kenya kuwavamia wavuvi wawapo ziwani huku vyombo vyao vya uvuvi vikiwa vinapeperusha bendera za Tanzania ambapo aliziomba mamlaka husika kusimamia kwa makini utaratibu wa kupeperusha bendera hizo.

Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Juma Ndaki amesema atahakikisha vikundi vya ulinzi shirikishi vinaimarishwa katika maeneo hayo ili visaidiane na askari Polisi kufanya doria za mara kwa mara.

IGP anaendelea na ziara yake katika mikao ya kanda ya ziwa huku akitumia usafiri wa Helkopta ili kujionea kwa uhalisia maeneo hayo ili kuweza kuzipatia ufumbuzi changamoto za uhalifu katika maeneo ya Visiwa vya Ziwa Viktoria.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.