Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Azungumza na Ujumbe wa Chuo Kikuu Cha Misri Waliofika Ofisini Kwake Vuga Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kushoto akizungumza na Timu ya Madaktari Bingwa wa Watoto Kutoka Chuo Kikuu cha Alexandria Misri waliokuwepo Zanzibar kufanya upasuaji kwa maradhi ya Watoto.
Wa kwanza kutoka Kulia ya Balozi Seif ni Kiongozi wa Timu hiyo Profesa Saber Waheels na Kushoto ya Balozi Seif ni Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Misri Major General Issa Suleiman Nassor.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kushoto akizungumza na Timu ya Madaktari Bingwa wa Watoto Kutoka Chuo Kikuu cha Alexandria Misri waliokuwepo Zanzibar kufanya upasuaji kwa maradhi ya Watoto.
Wa kwanza kutoka Kulia ya Balozi Seif ni Kiongozi wa Timu hiyo Profesa Saber Waheels na Kushoto ya Balozi Seif ni Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Misri Major General Issa Suleiman Nassor.
 Kiongozi wa Timu ya Madaktari Bingwa kutoka Chuo Kikuu cha Alexandria Misri Profesa Saber Waheels akimueleza Balozi Seif nia ya Chuo hicho ya kutaka kujenga Hospitali ya Watoto Visiwani Zanzibar.
Profesa Saber Waheels akimkabidhi Balozi Seif zawadi maalum kutoka Uongozi wa Chuo Kikuu cha Alexandria cha Nchini Misri.
Balozi Seif akimkabidhi Profesa Saber zawadi ya Mlango wa Zanzibar kama ishara ya Timu yake kukaribishwa Zanzibar muda wowote kutoa huduma za Kitaalamu.
Balozi Seif  kati kati waliokaa vitini akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Madaktari Bingwa kutoka Nchini Misri pamoja na Uongozi wa Wizara ya Afya mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.Kulia ya Balozi Seif ni Kiongozi wa Madaktari bingwa wa Misri Profesa Saber Waheels, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga na  Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Zanzibar Balozi Mohamed Haji Hamza.Kushoto ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Afya Mh. Harusi Said Suleiman, Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Misri Major General Issa Suleiman Nassor na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bibi Halima Maulid Salum.
 Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Misri Major General Issa Suleiman Nassor aliyevaa suti ya buluu akiteta jambo na Balozi Seif  kati kati huku Profesa Saber Waheels akishuhudia.

Balozi Seif kulia akiagana na Kiongozi wa Timu ya Madaktari Bingwa wa Chuo Kikuu cha Alexandria Nchini Misri Profesa Saber Waheels baada ya kumaliza mazungumzo yao. Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.
Uongozi wa Chuo Kikuu cha Alexandria  Nchini Misri umeonyesha nia ya kutaka kujenga Hospitali  kubwa ya kuhudumia  maradhi mbali mbali  ya Watoto hapa Zanzibar katika mpango wake wa kuendelea kutoa huduma za Afya hasa masuala ya upasuaji.
Hatua hiyo mbali ya kuimarisha Ushirikiano wa Kihistoria wa Muda mrefu uliopo kati ya Wananchi wa Zanzibar na Misri lakini pia utapunguza gharama  za matibabu zinazowakumba wanafamilia za Wagonjwa wa Watoto wa Zanzibar ambao wana kipato kidogo.
Kiongozi wa Madaktari Tisa  Bingwa wa Magonjwa ya Watoto kutoka Chuo Kikuu cha Alexandria cha Nchini Misri Profesa Saber Waheels alisema hayo akiiongoza Timu ya Madaktari hao walipofika Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  kwa mazungumzo.
Madaktari hao Tisa ambao wanaelekea Jijini Dar es salaam kuendelea na ratiba zao za kutoa huduma walikuwepo Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kutoa huduma za Upasuaji kwa Watoto mbali mbali wa Zanzibar.
Profesa Saber Waheels alisema Vyuo Vikuu mbali mbali Nchini Misri kikiwemo kile cha Alexandria vimekuwa na Mpango Maalum wa kuwaandaa  Wasomi wa Nchi hiyo kutoa huduma za Kitaalamu nje ya Mipaka ya Misri wakilenga zaidi Mataifa ya Afrika.
Kiongozi huyo wa Madaktari Tisa  Bingwa wa Magonjwa ya Watoto kutoka Chuo Kikuu cha Alexandria cha Nchini Misri alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba  nia ya kutaka kuanzisha Ujenzi wa Hospitali ya Watoto Zanzibar ni muendelezo wa fikra na Mipango hiyo.
Akitoa shukrani zake  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alisema Misri kupitia Vyuo Vikuu vyake iko makini katika kuona Sekta ya Afya Visiwani Zanzibar inaendelea kuimarika zaidi.
Balozi Seif  aliishukuru Nchi hiyo kutokana na mfumo wake wa kuiunga mkono Zanzibar katika masuala ya Afya hasa pale inapotoa Walaamu wake kufanya kazi pamoja na Wataalamu wa Kizalendo kwenye sekta tofauti za Maendeleo.
“ Mfumo wa Wataalamu wa Misri kujumuika pamoja na Wataalamu Wazalendo unaongeza uwajibikaji mkubwa unaoleta faraja kwa Wananchi walio wengi pale wanapopata huduma hizo”. Alisema Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba kutokana na Mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuandaa sera ya kuwa na huduma za Afya kila umbali wa Kilomita Tano Zanzibar bado inahitaji kuungwa mkono katika Sekta ya Afya kutoka Nchini Misri.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliihakikishia Timu hiyo ya Madaktari Bingwa kutoka Chuo Kikuu cha Alexandria Nchini Misri kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  haina pingamizi ya upatikanaji wa eneo la ardhi kwa ajili ya Ujenzi wa Hospitali hiyo pale kazi hiyo itakapowadia.
Mapema Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Misri Major General Issa Suleiman Nassor alisema  Timu hiyo ya Madaktari Bingwa kutoka Nchini Misri  imefanya Operesheni  36 za Watoto katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.

Balozi Issa alisema opersheni hizo zilifanyika ikiwa ni muendelezo wa ratiba za Madaktari Bingwa kutoka Chuo Kikuu cha Alexandria  wanazozifanya Nchini Tanzania ambapo Siku mbili zijazo wanatarajiwa kutoa huduma kama hizo katika Hospitali ya Rufaa Muhimbili Jijini Da es salaam.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.