Habari za Punde

Neymar asimulia alivyoomboleza Brazil kuondolewa Kombe la Dunia 2018

Mshambuliaji wa Brazil Neymar amesema hakutaka "kuuona mpira wowote karibu naye" au hata kutazama mechi zilizosalia za Kombe la Dunia baada ya taifa lake kuondolew akwenye michuano hiyo.
Brazil waliondolewa hatua ya robofainali baada ya kulazwa na Ubelgiji.
"Nilikuwa ninaomboleza, nilikuwa na huzuni sana, lakini uzuri huzuni huondoka siku zinavyosonga," amesema mchezaji huyo wa Paris St-Germain.
"Nina mwanangu wa kiume, familia yangu, marafiki zangu na hawapendi kuniona nikiwa nahuzunika na kujisikitikia nyumbani."
Mchezaji huyo wa miaka 26 pia amezungumzia tetesi ambazo zimekuwa zikimhusisha na kuhamia Real Madrid akisema huo ni "uvumi tu".
Neymar alihamia PSG kwa uhamisho wa £200m kutoka Barcelona ambao uliweka rekodi mpya ya dunia mwaka jana.
Amefunga mabao 28 katika mechi zote alizochezea klabu hiyo ya Ufaransa.
Mbrazil huyo alishutumiwa sana wakati wa Kombe la Dunia kwa kudaiwa kuigiza kila alipoguswa au kukabwa na wapinzani, lakini amesema kwamba alifaa kulindwa zaidi na waamuzi.


"Watu walikuwa wepesi sana wa kukosoa aliyekuwa anachezewa visivyo badala ya yule aliyefanya madhambi," Neymar ameambia AFP.
"Nilikwenda Kombe la Dunia kucheza, kuwashinda wapinzani, na si kugongwa kila wakati. Ukosoaji dhidi yangu ulitiwa chumvi, lakini mimi ni mwanamume sasa, nimezoea kukumbana na mambo kama haya."
"Siwezi kuwa mwamuzi na niwe nacheza wakati upo huo, lakini kuna nyakati huwa natamani kama naweza kufanya hivyo."

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.