Habari za Punde

SMZ Kuipa Ushirikiano Kampuni ya STL Group.Imeonesha Kuiunga Mkono Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akizungumza na Uongozi wa Taasisi ya Kimataifa ya Kitaalamu inayosimamia Makampuni  Sita yanayojihusisha na masuala ya Miundombinu, Afya, Elimu, Biashara, umeme na mawasiliano ya Kisasa ya STL Group Ofisini kwake Vuiga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif akimsisitiza jambo Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Amand Group iliyo chini ya Taasisi ya STL Group  Bwana Nadas Simhoni aliyeuongozi Ujumbe wa Viongozi Wanne wa Kampuni hiyo.(Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Uongozi wa Taasisi ya Kimataifa ya Kitaalamu inayosimamia Makampuni  Sita yanayojihusisha na masuala ya Miundombinu, Afya, Elimu, Biashara, umeme na mawasiliano ya Kisasa [STL Group} imeonyesha nia ya kutaka kuiunga mkono Zanzibar ili iweze kuongezea nguvu ya Uwezeshaji katika kubuni mbinu na Maarifa kwenye Sekta tofauti.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Amand Group iliyo chini ya Taasisi hiyo Bwana Nadas Simhoni akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Wanne wa Kampuni hiyo alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Simhoni alisema Amand Group yenye Wataalamu wa Kutosha ambao tayari wanawajibika katika Mataifa ya Ghana, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo {DRC}, Togo, Ivory Coast na Tanzania wana uzoefu wa kutosha katika kusarifu mambo tofauti ikiwemo michoro ya majengo mbali mbali.
Alisema miradi ya Maendeleo ikitolea mfano iliyo katika sekta za Elimu, Afya na Kilimo ambazo huijumuisha Jamii  kubwa ndio kipaumbele walichokiangalia zaidi kwa kujumuisha utekelezaji wake katika ngazi ya Kitaifa sambamba na Jumuiya za Kijamii.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliuhakikishia Uongozi wa Taasisi hiyo ya STL Group kwamba  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  iko tayari  kuipa ushirikiano Taasisi hiyo katika azma yake ya kuunga mkono Maendeleo ya Zanzibar.
Hata hivyo Balozi Seif  aliuambia Uongozi wa Taasisi hiyo kwamba  Serikali imeweka utaratibu maalum wa kutoa Tenda pale inapotaka kuanzisha Miradi yake ya Kiuchumi na hata ya Kijamii jambo ambalo Uongozi huo una fursa ya kuomba pale inapotokea masuala hayo.
Taasisi ya Kimataifa ya Kitaalamu  ya STL Group inasimamia Makampuni  Sita yanayojihusisha na masuala ya Miundombinu ya Ujenzi, Sekta za Afya, Elimu, Biashara, umeme, Mafuta, Gesi pamoja na Mtandao wa Mawasiliano ya Kisasa .

Makampuni hayo ni pamoja na Super Tech Limited, Amand Energy, Amand, Agritop Limited, Super lock pamoja na SAF STL Amand.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.