Habari za Punde

Wakalimali wa Lugha za Alama Wanatakiwa Kupata Ajira Katika Sehemu za Kazi- Mkuu wa Wilaya ya Mjini Mhe. Marina Thomas.

Na Takdir  Ali. Maelezo Zanzibar.
Taasisi za Kisheria zimetakiwa kuajiri wakalimani wa lugha za Alama katiaka sehemu zao za kazi ili kuweza kuondosha usumbufu wanaoupata Viziwi na kuweza kupata haki zao za msingi za mawasiliano.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Mjini Bibi Marina Joel Thomas huko katika ukumbi wa Mental Kidongo Chekundu wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya siku 5 ya ukalimani wa lugha ya Alama kwa baadhi ya watendaji wa Serikali.
Amesema Viziwi wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa katika kupata huduma kama vile Mahakamani, Jesshi la Polisi na Jeshi la Magereza hivyo iwapo wataajiri Wakalimani wa lugha ya Alama matatizo hayo yataweza kuondoka.
Amefahamisha kuwa Watu wenye Ulemavu ikiwemo viziwi ni sehemu ya Wanajamii hivyo hawapaswi kutengwa bali kinachohitajika ni kushirikishwa katika masuala yanayowahusu.
Hata hivyo amekemea baadhi ya wazazi wenye tabia ya kuwafungia majumbani watoto wenye ulemavu kwa madai ya kuwa ni mkosi katika maisha hiyo ni dhana potofu.
Aidha ameuagiza Uongozi wa Chama cha Viziwi Zanzibar (CHAVIZA) kuzidi kufanya uhamasishaji na Ushawishi kwa Wananchi waweze kusomea lugha hiyo ili waweze kutoa wataalamu wengi watakoweza kufanya kazi sehemu mbali mbali zinazotoa huduma za kijamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Zanzibar Haidar Hisham Madoea amesema Watu wenye mahitaji maalum wanapata tabu katika vyombo vya Mahakama, Polisi na Magereza kutokana na maumbile yao na baadhi ya wakati ni kutokana na kutokuwa na maelewano ya lugha katika maeneo tofauti ya eneo hilo jambo ambalo kwao imekuwa ni mtihani mkubwa wa kufikia haki zao za msingi.
Amesema Semina hiyo ya siku 5 kwa Wadau hao itaweza kuwasaidia kuleta mabadiliko katika vyombo hivyo itaweza kupiga hatua ya kuwepo kwa mawasiliano na kuweza kuondoka kabisa matatizo hayo.
Amewataka washiriki hao kujifunza ,kuielewa lugha ya alama ili iweze kuleta mustakbali mzuri wa mawasiliano kwa viziwi katika jamii iliotuzunguka sambamba na kuwataka kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao ambao hawajapata mafunzo  hayo.
Amesema Sheria no.9 mwaka 2006 inaitaka Mahakama ,Jeshi la Polisi kuwa watu wenye ulemavu  wanapokwenda katika sehemu hizo wapatiwe wakalimani wa lugha za Alama bure lakini lakusikikitisha imekuwa hawapatiwi wakalimani na hivyo kupelekea kufutiwa kesi zao kwa kutokuwepo mawasiliano kati ya vyombo hivyo na muhusika .   
Amefahamisha kuwa Viziwi wamekuwa hawetendewi haki kwa zaidi ya asilimia 90 kwa sababu kuna kesi nyingi za ubakaji ambazo haziendi kwa madai ya kutokuwepo kwa ushahidi ,hata mwenyewe akimtaja muhusika  amekuwa haaminiki kutokana na ulemavu alionao.
Aidha amesema kuna  baadhi ya watendaji wasiokuwa waaminifu wanaitumia njia hiyo kuzikwamisha kesi hizo na hivyo kuwakosesha kupata haki zao kama watu wengine katika jamii.
Nao washiriki hao wamesema mafunzo hayo yataweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha wanapata mawasiliano ili Viziwi waweze kupata haki yao ya mawasiliano.
Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.