Habari za Punde

Wanaonusuriwa na umaskini Kengeja wapiga hatuaNA/ HAJI NASSOR, PEMBA

WANAWAKE waliomo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini kijiji cha Mkumbi shehia ya Kengeja wilaya ya Mkoani Pemba, ambao wamekujisanya pamoja na kuzalisha sabuni, wamesema wameshaondoka na utamaduni wa kukopa fedha kwa jirani, na sasa wanatumia kupitia ushirika wao.

Wamesema kwa sasa ushirika wao pamoja na kwamba bado ni mchanga, lakini umeshaanza kuwanesha njia ya mafanikio, kwa kule kuwa na sehemu ya uhakika wa kukopa fedha kwa ajili ya kuendeshea maisha.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, wanaushirika hao wa ‘mwanzo mgumu” walisema kabla ya kuja kwa TASAF na kuwawezesha kifedha walikuwa wakipata usumbufu pale wanapotaka fedha hata shilingi 500/= kwa ajili ya kuondowa shida zao.

Walieleza umaskini wao hasa ulikuwa kwenye kipato, jambo ambalo lilikuwa likiwakosesha raha na furaha ya maisha hasa pale wanapohitaji fedha kwa ajili kutatua shida zinazowakabili.

Mmoja kati ya wanachama hao, Fatma Rashid Hassan, alisema sasa ule utamduni wa kumpigia magoti jirani au wafanyabiashara kwa kukopa fedha ameshaanza kuusahau, kwa  vile ushirika wao umekuwa mkombozi.

Alisema fedha wanazowezeshwa na TASAF wao huzifanya kama za kununulia Madira na vipodozi pekee, bali waliamua kujikusanya pamoja idadi ya watu 15, na kuanzisha ushirika ambao leo wameshaanza kula matunda yake.

“Mimi sasa sikumbuki kumkopa mtu fedha kwa Tshilingi 100,000/= hadi Tshilingi 200,000/=, maana nikichacha napiga hodi kwenye ushirika wetu, jambo ambalo zamani sikuwahi kuzishika fedha kama hizo zikawa zangu,”alieleza.

Nae, Mwanajuma Makame Khatib, alisema ipo tofauti kubwa kabla na baada ya kuingia katika ushirika huo, kufutia kupokea fedha za TASAF za kunusuru kaya maskini.

Alieleza  kwa sasa anajihisi nae ni sehemu ya mtu mwenye maisha mazuri, kwa kule kuwa na uhakika wa kitu anachokihitaji jambo ambalo hapo kabla ilikuwa vigumu.

“Kwa kweli kwa sasa mimi binafsi sasa najihisi nimeshakomboka na umaskini hasa kwa hali ya maisha niliokuwa nayo kabla ya kuja TASAF na kuanzisha ushirika huu wa utengenezaji sabuni, maana ilikuwa tatizo na kipato,”alieleza.

Hata hivyo alisema amekuwa na msaada mkubwa ndani ya familia yake kwa kuchangia fedha za mahitaji ya kila siku wa wastani wa Tshilingi 5000/= kwa siku.,

Mapema Mwenyekiti wa ushirika wa uzalishaji sabuni Mwanaidi Khamis Kombo, alisema bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa soko la uhakika, ingawa kwa sasa wameanza kuuzia wanachama wenyewe.

Mwenyekiti huyo alisema, bado mafunzo waliopewa ya utengenezaji sabuni, bado hayajatosheleza na wanahitaji mafunzo zaidi ya uzalishaji sabuni iliobora.

“Kwa kweli soko bado dogo, lakini inawezekana linasababishwa na kwamba hatujaitangaaza sana sabuni yetu, maana bado ushirika wetu ni mchanga,”aliekeza.

Nae Katibu wa ushirika huo wa ‘mwanzo mgumu’, Fatma Juma Kombo, alisema waliamua kujiingiza kwenye utengenezaji wa sabuni ili kujikombowa na umaskini.

Alieleza  pamoja na kuwa na mradi huo wakati wowote wataanza na kilimo cha mboga mboga pamoja na ufugaji, ili kusaka njia ya kuhakikisha TASAF, ikimalizika wao wasirudi tena kwenye umaskini.

“Hali zetu za kimaisha kwa kweli zimeimarika ukilinganisha hapo zamani, na kama soko letu la sabuni litasimama badi sisi hatutoitwa tena kaya maskini,”alifafanua.

 Mapema Mratibu wa TASAF Pemba, Mussa Said Kisenge, amekuwa akirudia kauli yake ya kuwataka wananchi waliomo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini kubuni miradi ambayo itawakomboa na umaskini.

Alisema haitopendeza hata kidogo, kuona wananchi hao waliomo kwenye mpango huo, wanarudi tena kwenye umaskini mkubwa, mara TASAF itakapo ondoka kuwawezesha kifedha

Katika mikoa miwili ya Pemba, TASAF inawalengwa 14,378 wanaopokea fedha ambapo tayari wameshanzisha vikundi 942 vikiwemo vinavyojishughulisha na kilimo, ufugaji wa wanyama, utengenezaji sabuni, uhifadhi wa mazingira na kilimo cha Alizeti.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.