Habari za Punde

RC Ayoub akabidhiwa Kompyuta za Wafaulu wa kidato cha sita






































MKUU wa mkoa wa Mjini Magharibi ayoub mohammed Mahmoud (kushoto) akipokea moja ya kompyuta mpakato (compyuta) 96 kutoka kwa mkurugenzi wa kampuni ya ROM Solution Viorica Enescu (kulia). Kompyuta hizo zitakabidhiwa kwa wanafunzi waliopata daraja la A wa skuli za mkoa wa Mjini Magharibi

Na Mwinyimvua Nzukwi

WADAU wa sekta ya elimu na wananchi wa Zanzibar, wametakiwa kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali ili kuimarisha elimu nchini kwa kiwango kilicho bora.

Akizungumza baada ya kupokea kompyuta 96 aina ya laptop kutoka kampuni ya ROM Solutions, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud, amesema kufanya hivyo kutatanua wigo wa mafanikio katika sekta hiyo.

Amesema serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imekuwa ikitekeleza shughuli mbalimbali zikiwemo za ujenzi wa madarasa na kuondoa michango kwa wanafunzi wa ngazi zote ili kuondoa changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ambazo huchangia kupatikana matokeo yasiyoridhisha.



Ameipongeza kampuni hiyo kwa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya Zanzibar kielimu na sekta nyengine, akisema zawadi hizo zitaongeza hamasa ya wanafunzi na kuwawezesha kufanya vyema katika mitihani yao.

Amesema kompyuta hizo zitakazotolewa kwa wanafunzi wote waliofaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza kwenye mitihani ya kidato cha sita mwaka 2018 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati alipokutana nao wakati wakijiandaa kufanya mitihani hiyo mapema mwaka huu.

Aidha amewapongeza wanafunzi, walimu na wazazi kwa kushirikiana na kamati ya maendeleo ya elimu ya mkoa, hatua aliyosema iliwezesha kupatikana kwa matokeo mazuri ya mitihani hiyo.

Mapema, Mkurugenzi wa kampuni ya ROM Solutions Bi. Viorica Enescu, aliwapongeza wanafunzi kwa matokeo hayo na kusema kampuni yake itaendelea kushirikiana na serikali ya mkoa huo katika shughuli za maendeleo ya jamii.

Alisema ufaulu huo wa kiwango cha juu unaihakikishia nchi kupata wataalamu watakaosaidia kukuza uchumi na ustawi wa jamii.
Alitumia fursa hiyo kuwataka wanafunzi hao kuongeza bidii katika masomo yao watakapokuwa vyuoni.

Akitoa taarifa katika mkutano huo, Katibu Tawala wa mkoa huo Hamida Mussa Khamis, alisema mbali na zawadi hizo, ofisi ya mkuu wa mkoa ilichukua hatua ya kudhamini kambi za wanafunzi hao pamoja na upatikanaji wa vitabu.
Alisema shughuli hizo zilidhaminiwa na taasisi ya Mimi na Wewe, ambapo wanafunzi wa skuli zote za mkoa huo zilizokuwa na wanafunzi wa kidatu cha sita zilihusika na mpango huo.

Alieleza kuwa, mpango huo ulisaidia kupatikana kwa ufaulu wa daraja la kwanza kwa wanafunzi 96 na kupunguza idadi ya wanafunzi waliopata daraja sifuri kutoka 96 hadi 15.

Zaidi ya shilingi milioni 115 zimetumika kununulia kompyuta hizo zilizotolewa na kampuni ya ROM Solutions ambazo zitakabidhiwa kwa wanafunzi hao ili ziwasaidie katika maandalizi ya elimu ya juu.


.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.