Habari za Punde

Kamati teule ZFA yawashukuru wadau wa soka kwa ushirikiano

Kamati Teule ya Chama cha Soka Visiwani Zanzibar (ZFA) inayoongozwa chini ya Mwenyekiti Mwalimu Ali Mwalimu na Katibu wake Khamis Abdallah Said inatoa shukrani za dhati kwa wadau wote wa Soka kwa ushirikiano wao mpaka jana kumaliza ligi kuu soka ya Zanzibar na kumpata Bingwa ambae ni JKU na makamo Bingwa Zimamoto ambao wataiwakilisha Zanzibar katika Mashindano ya klabu bingwa na kombe la shirikisho Barani Afrika kwa msimu wa mwaka 2018-2019.

Kamati inajivunia kumaliza ligi kuu pasipo kuwepo rufaa ya aina yoyote, ni kitu cha kujivunia baada ya kuona mpaka jana inachezwa michezo ya mwisho ya kumaliza ligi bingwa bado alikuwa hajajulikana, hivyo tunavipongeza vilabu vyote shiriki, viongozi, wachezaji, Waamuzi na Wadau wote wa soka kwa mashirikiano makubwa kwa kumaliza ligi kwa amani na salama.

Pia tunawashukuru Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) pamoja na taasisi nyengine za Serikali kwa kuinga mkono Kamati mpaka kumaliza ligi salama pamoja na kuwa na changamoto mbali mbali.

Tunawashukuru wale wote walojitolea kuisadia kamati kwa kufanikisha kutoa zawadi wakiwemo Assalam Air pamoja na Wadau wengine, zawadi za Bingwa wa ligi kuu na Bingwa wa Kombe la FA linaloendelea sasa zitatolewa kwenye uzinduzi wa msimu mpya wa mwaka 2018-2019 katika mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Bingwa wa ligi kuu (Zimamoto) dhidi ya Bingwa wa kombe la FA (Bado hajajulikana) mchezo huo utachezwa siku ya Alhamis ya Oktoba 18, 2018 saa 10:00 za jioni katika Uwanja wa Amaan.

Kamati inaomba radhi kwa mtu au timu yoyote tuloikwaza hatukuwa na nia hiyo bali, lengo letu ni kuleta maendeleo ya soka Zanzibar.
Kwasasa tunamsubiri Mrajis wa Vyama vya Michezo Zanzibar kuipitisha Rasimu ya Kanuni, na tunategemea muda wowote kuanzia sasa kupitishwa, hivyo tunatoa wito kwa Vilabu na Viongozi kuifata na kuipitia vizuri kalenda ya ZFA ya Mwaka 2018-2019 na kamati haitovumilia kuona Kalenda inayumbishwa.

Mwisho tunawashukuru sana sana Vyombo vya Habari hasa vya ndani kwa uzalendo wao mkubwa wa kujitolea kuutetea mpira wa Zanzibar na tunawaomba waendelee kujitolea kuinua Michezo Zanzibar.

IMETOLEWA NA MSEMAJI WA KAMATI TEULE YA ZFA ABUBAKAR KHATIB KISANDU.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.