Habari za Punde

Kidungu Hutumika Kufukizia Ndege Katika Mashamba ya Mpunga.

Kidungu hutumiwa na Wakulima wa Kilimo cha Mpinga Zanzibar kwa ajili ya kuwindia Ndege kuushambulia mpunga wakati ukiwa shambani kama kinavyoonekana katika moja ya shamba la mpunga. 
Na. Hamad Hassan,  PEMBA
Zanzibar kama nchi ya visiwa, imejaaliwa kuwa na tamaduni nyingi ambazo ni kielelezo madhubuti cha wazanzibari.
Tamaduni hizo tangu enzi na dahar (zama) nyingi zilizopita, ni muhimu sana kwa wwananchi kuenzi tamaduni hizo.
Miongoni mwa tamaduni hizo ambazo huwenda zinavitofautisha visiwa hivi na maeneo mengine ni pamoja na mavazi, aina ya mapishi na hata jinsi ya watu wanavyoishi kwa ujamaa zaidi.
Lakini pia visiwa hivi vimebarikiwa kuwa na ardhi yenye rutba ya asili, jambo linalowasukuma watu wengi kuelekeza nguvu zao kwenye kilimo.
Wapo waliojikita kilimo cha mihogo, ndizi, mtama, mikarafuu na kundi kubwa likionekana kwenye kilimo cha mpunga.
Kilimo hichi ni muhimu sana kutokana na kuwasaidia wananchi hawa kupata chakula chao cha kujikimu kimaisha.
Pamoja na juhudi za wakulima, kulima na kufanya juhudi ili kupata mazao yaliyo ya kutosha, lakini wana kumbana na adha kubwa dhidi ya makundi na aina mbali mbali ya ndege wanao haribu mpunga, ikiwemo kweche, kuku na hata njiwa.
Hayaaa!!!.. haooo !!!…eeehayaaa.. hao haooo, hizi ni nyimbona semi nyingi, zinazo tumika ilimradi kumfanya ndege aweze kukimbia, huku wengine wakipiga vibati au makopo ilimradi kukamilisha lengo lao la kuuweka mpunga ukiwa salama.
Wakulima wa mpunga hulazimika kutafuta na kubuni njia mbali mbali ikiwemo majengo maalum yanayotumia miti mitupu, kwa ajili ya ulinzi wa mpunga wao.
Si unajua upatacho upetee kata, ndivyo walivyotuwasa wale waliokuwepo kabla yetu.
Jengo hilo kwa ajili ya shambani ‘kidungu au dungu’ ni ujenzi wenye kuchomeka miti mikubwa minne ilio na ukubwa sawa iliosimamishwa, kisha kutanguliwa na na mengine kadhaa iliolazwa.
Hapo humruhusu mtu anaeulinda mpunga kukaa juu, huku akiendeleza kazi ya kuhakikisha hakuna ndege anaeushambulia mpunga wake.
Katika makala haya mwandishi anakusudia kuonesha jinsi ya utengenezaji wa Kidungu na matumizi yake, kwa wakulima wa mpunga hapa visiwani.
Vidungu vipo vya aina nyingi, kuna vidungu vya kuingia mpunga ,vidungu vya majukwaa ya mikutano na hata vidungu vinavyojengwa kwa ajili ya sherehe mbalimbali kama vile mwaka kogwa.
Lengo kuu hasa la kidungu au dungu ni kuwarahisishia wahusika kupata sehemu za kukaa na kuangalia michezo mbali mbali, kwa lungha nyengine ni kujiongezea urefu wa kuona jambo.
Kwa leo kalama ya makala hii, inaangazia kidungu au dungu la kuindia ndege, pale mpunga unapokuwa katika mazingira ya kuanza kupasua (kuchanua au kufumua).
Kidungu cha kuingia ndege ni miongoni mwa ubunifu mahiri, uliofanywa na watu ambao wametutangulia, si kitu ambacho kimeletwa na wageni.
Tumezoea kuona vitu vingi vikiletwa na wageni wakiwemo wazungu, wagiriki au waarabu ambao walitawala kwa karne zaidi ya 18, ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Kidungu kilianza kutumika kwa zaidi ya karne mbili sasa, katika shughuli za kilimo cha mpunga, wakati wa kupalia na hasa wakati wa kuinga ndege.
Subira Ali Hababi miaka 53 wa shehia ya Ndagoni wilaya ya Chake Chake, anasema kidungu moja ya jengo la tamaduni ulioanza anza tangu kwa wazazi wake walipokuwa akikitumia kuingia ndege.
“Takriban karne na karne zilizopita, baadae kurithiwa na mabibi na mababu wa enzi hizo na hata wao, katika kizazi hiki bado wanatumia faida ya ubunifu wa matumizi ya kidungu,”anasimulia.
Anaeleza kuwa kwa wao kidungu walikikuta tayari kinatumika, lakini kina mchango mkubwa katika shughuli zao za kilimo, bila ya kidungu shughuli nzima ya ulinzi (uingaji) wa ndege wanao haribu mpunga ingelikuwa ugumu kwao.
“Kama kidungu kingelikuwa hakipo tungekuwa tikipata mazao kidogo, huku nguvu nyingi zimetumika katika kufikia hadi mpungua umeweza kuchanua na kuanza kutegemea kupata chakula,”anasema.
Saida Juma miaka 45 nae akiwa huko huko Ndagoni, anasema kidungu ni urithi walioukuta tayari kimekuwa na faida kubwa kwao, matumizi yake kubwa ni kuingia mpunga.
“Kidungu sisi tumekikuta hivi hivi, walikuwa wakitumia wazee wa zamani, lakini kutokana na kazi yake kubwa ya kukimbizia ndege ili mpunga ubakie salama, akimaanisha kibanda pekee hakikidhi haja.
Khamisi Zaidi wa Mgogoni Kaskazini Pemba, anasema kidungu kwake yeye ni zaidi ya banda hasa wakati ule, mpunga ukiwa na miezi mwezi mmoja tokea kufumua.
“Unajua hawa ndege wanaupenda zaidi mpunga ukiwa mchanga, na sasa kama utakaa kibandani tu bila ya kuwa na kidungu, ambacho hujengwa karibu na ule mpuga uliofumua basi huna mamavuno,”anaeleza.
Kwa upande wa shughuli za kuinga mpunga, kidungu husaidia sana kwani, mara nyingi hujengwa katikati ya shamba, hivyo humuwezesha mtu kuangalia eneo lote la pembe nne za shamba kama kuna ndege waharibifu au laa.
Halila Khalfani Suleimani miaka (40) anaeishi Kwale Chake Chake, anasema historia halisi anavyoelewa ni kuwa kidungu ni urathi unaotoka na ubunifu wa wazee na hajui jengingine.
Kwa alivyonieleza, kumbe uwepo wa jengo la miti linaloitwa kidungu, chimbuko lake ni hapa hapa kwetu visiwani.
Hapo zamani, kidungu kilijengwa kwa kutumia kamba zilizo madhubuti , ili kukiwezesha kuwa imara na kukaliwa na mtu juu yake, kwa shughuli za kuinga ndege.
Hapa sasa, tunajifunza kuwa, kidungu sio lazima kijengwa kwa kutumia miti pekee, lakini hata kamba madhubuti, ingawa kwa karne hii, sasa wanajenga wanatumia miti zaidi kuliko kamba.
Wengine walithubutu kukiita kidungu kisaidizi, kiona mbali katika shughuli za kuinga ndege, ili wasile mpunga hii ni kwa sababu humuwezesha muinga ndege, kuona hadi mwisho wa pande zote nne za shamba.
Kwa zama hizi na hizo zilizopita, hivi ni nani asiejua umuhimu au thamani ya kidungu? Ni katika shughuli nzima ya uingaji ndege kwa zao la mpunga, hii inatokana na mchango wake mkubwa katika shughuli za uingaji wa ndege kwenye kilimo cha mpunga.
Matumizi ya kidungu, kumbe hayaishi tu, kwenye ulinzi wa ndege, maana Halim Juma Omar wa Sizini, anasema hata baada ya majira ya jioni kumaliza kazi ya kuingia ndege, hukitumia kwa kuhifadhi baadhi ya vyombo vyake.
“Kwa mfano vitu kama mbuzi, kinu, nchi, sahani na madishi basi mimi huhifadhi juu ya kidungu,”anaeleza.
Kidungu huwaunganisha watu walio katika shughuli moja ya kilimo cha mpunga kuishi kwa pamoja, kuoneana huruma kwa kusaidiana kufanya kazi kama timu moja ya kuwakimbiza ndege.
Ili kuupata ukweli halisi wa umuhimu wa kidungu, makala hii ilifunga safari hadi kupiga hodi katika makumbusho kuu iliyapo Chake Chake Pemba , kukutana na afisa historia mambo ya kale Khamis Ali Juma.
Anasema kidungu asili yake ni hapa hapa Zanzibar, na wala hakijarithiwa kutoka kwa wageni wala sehemu nyengine ya ulimwengu.
Aanakiri kuwa ni ubunifu kutoka kwa wazee wa zamani kutokana na mahitaji yao hasa kwa wale wanaolima mpunga.
Anakumbuka sana, kuwa kule kwao Pujini na Vitongoji zilizoko ukanda mashariki mwa kisiwa cha Pemba, Wilaya ya Chake Chake, kilijengwa kwa kutumia miti iliyo imara na kulaza mbao ya mvumo juu yake na kufunga kwa kamba zilizo imara, ili kukifanya kiwe imara zaidi,
Kama alietoa wito kwa jamii ya wazanzibar, kwamba wawe na tabia ya kutunza tamaduni zao kwani, ni miongoni mwa utambulisho wa watu kitaifa na kimataifa duniani kote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.