Habari za Punde

Wanawake 1,316 Waachiwa Majukumu na Wanaume Zanzibar

Na. Zuhura Juma, PEMBA
TAASISI ya Milele Zanzibar Foundation (MZF) imegundua changamoto mbali mbali zinazoikabili jamii, ikiwemo familia 1,316 kuongozwa na mwanamke kati ya familia zaidi ya 14,000 walizozifanyia utafiti katika shehia 22 za Unguja na Pemba.
Katika utafiti huo pia waligundua  kuwa, zaidi ya asilimia 50 ya nyumba ndani ya shehia hizo, hazina huduma ya umeme na maji, udhaifu wa kamati za skuli kutokana na kukosa vitendea kazi, ukosefu wa vyoo kwa watoto wenye ulemavu.
Changamaoto nyengine zilizoibuliwa na Milele ni ukosefu wa maktaba, maabara, uchache wa madarasa, upungufu wa madaktari na nyumba katika vituo vya afya, pamoja na uelewa mdogo kwa wajasiriamali ambapo huzalisha bidhaa lakini kipato chao ni kidogo.
Akizungumza katika kikao cha mrejesho cha Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation baada ya kufanya utafiti kwenye shehia 22, Mkuu wa Miradi ya Milele Zanzibar Foundation Khadija Ahmad Sharif alisema, malengo yao kwa mwaka 2020 ni kuhakikisha wanazitatua changamoto zote zinazowakabili wananchi hao, ili kuwasaidia kujikomboa na umasikini.
Alisema kuwa, watahakikisha familia hizo zinazosimamiwa na wanawake wanazipa kipau mbele katika kuwasaidia, kwani wanaonekana kukosa huduma mbali mbali wanazostahiki kuzipata, jambo ambalo litawasaidia katika kupata haki zao na kuyamudu maisha yao.
“Kwa kweli baada ya kuona familia ambazo msimamizi wake ni mwanamke tumeshtuka sana na kuona ipo haja ya kuzisaidia kwanza, kwani wana hali ngumu ya maisha zaidi, ambapo watoto hukosa haki zao za msingi ikiwemo elimu”, alisema.
Kwa upande wake Mratibu wa miradi ya Elimu kutoka Taasisi hiyo Ali Bakari, alisema kuwa, katika utafiti huo waligundua kuwa umasikini mkubwa uliopo ndani ya jamii unasababisha watoto kutokwenda skuli, ambapo muda mwingi huutumia kujitafutia chakula wao pamoja na wazazi wao.
“Kuna tatizo kubwa la watoro kwa wanafunzi kuanzia darasa la nne kwenda juu, hivyo juhudi kubwa inahitajika kuwarejesha watoto skuli sambamba na wazazi kushirikiana na walimu katika kulipeleka mbele gurudumu la elimu kwa watoto”, alisema Mratibu huyo.
Nae Mratibu wa miradi ya Afya kutoka Taasisi hiyo Shemsa Mselem Nassor alieleza kuwa, katika utafiti huo waligundua kuwa, akina baba wengi hawashiriki ipasavyo katika upatikanaji wa lishe bora kwa watoto, jambo ambalo linapelekea kudumaza afya ya mtoto chini ya miaka mitano.
Aidha Shemsa alisema kuwa, waligundua akina mama wajawazito wana upungufu wa damu kwa asilimia 70 kwa mkoa wa Kaskazini Pemba na asilimia 68 kwa mkoa wa Kusini Pemba, jambo ambalo linaweza kuwasababishia vifo wakati wa kujifungua.
Mratibu kutoka Taasisi hiyo Alice Mushi alisema kuwa katika sekta ya kiuchumi wamegundua kuwa wanajamii walio wengi hulima mazao ya chakula na sio ya biashara na hutegemea kilimo cha mvua, hivyo Taasisi yao itawawezesha wananchi hao namna ya kuweza kujikomboa wenyewe na kujiletea maendeleao kwa kuwawezesha kimafunzo na kuwasaidia vitendea kazi. 
Mapema akifungua kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Rashid Hadid Rashid aliipongeza taasisi hiyo kwa kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kwenye jamii, pamoja na kuibua changamoto zinazowakabili wananchi ambazo zitaweza kupatiwa ufumbuzi unaofaa.
Nae akifunga kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Wete Abeid Juma Ali aliishukuru taasisi hiyo kwa walivyojitolea kwa lengo la kuipatia jamii maendeleo na kuwataka kuangalia suala zima la virusi vya ukimwi katika sekta ya afya, ili wasaidie kupambana na ugonjwa huo unaoathiri katika jamii.
Akichangia mada katika kikao hicho Mkurugenzi wa Baraza la Mji Wete Hamad Mbwana alisema kutokana na idadi kubwa ya familia zinazosimamiwa na mwanamke, hivyo ipo haja ya kuzisaidia familia hizo zaidi ili kuona wanaondokana na changamoto zinazowakabili.
Katibu Tawala Wilaya ya Micheweni Hassan Abdalla Rashid aliiomba Taasisi hiyo kuendelea na juhudi hiyo ya kuisaidia Serikali na jamii kwa ujumla katika suala la kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mkutano huo wa mrejesho wa utafiti uliofanywa na Milele Zanzibar Foundation, ambapo changamoto mbali mbali walizoziibua waliziwasilisha na kusema kuwa mwaka 2020 watahakikisha zinapatiwa ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.