Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Atembelea Eneo Linalojengwa Nyumba za Wananchi Waliopata Maafaa ya Mvua za Masika Zanzibar.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikagua eneo lilolotengwa na Serikali kwa ajili ya Ujenzi wa Nyumba za Makaazi ya Wananchi walioathirika na Mvua za Masika katika Kijiji cha Nungwi Mkoa Kaskazini Uanguja.Wa kwanza kutoka Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “A” Ndugu Hassan Ali Kombo.
 Muonekano wa eneo linalotaka Kujengwa Nyumba hizo ambapo tayari harakati za Ujenzi zimeanza Tarehe 25 Agosti Mwaka 2018 Chini ya Usimamizi wa Ushauri Elekezi wa Kampuni ya Samkay Consult Cooperation Lilited.
 Mshauri Elekezi wa Kampuni ya Samkay Consult Cooperation Lilited Bwana Amour Hamad Omar akimpatia maelezo Balozi Seif namna Ujenzi huo utakavyoendelezwa.
 Mmoja wa Wataalamu wa Ujenzi wa Nyumba za Makaazi ya Wananchi walioathirika na Mvua za Masika akifafanua jambo wakati Balozi Seif alipofika kuangalia maandalizi ya Ujenzi wa Nyumba hizo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Haji Makame akitoa ufafanuzi wa ongezeko la eneo la hakiba linalojengwa nyumba za Makaazi ya Waathirika.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia uwepo wa huduma muhimu wakati nyumba hizo zitakapohamiwa na waathirika wa Mvua wa Masika yaliyopita.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wamewashauri na kuwaomba Wafadhili, Wahandisi na Mshauri elekezi wa Ujenzi wa Nyumba za Makaazi ya Wananchi walioathirika na Mvua za Masika kuzingatia huduma na mahitaji muhimu ya Wananchi  hao kabla ya kuanza kuhamia katika Makaazi yao Mapya.
Alisema maeneo yaliyoteuliwa kujengwa kwa nyumba hizo Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja na Msuka Kaskazini Pemba kimazingira bado yako mbali na maeneo ya Makaazi ya Wananchi wengine jambo ambalo linaweza kuleta usumbufu.
Akikagua eneo lililoanza harakati za Ujenzi wa Nyumba hizo Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja Balozi Seif Ali Iddi alisema licha ya Wafadhili wa Mradi huo kuzingatia umuhimu wa uwepo wa huduma muhimu katika Makaazi hayo zilizopangiwa kukamilishwa katika Awamu ya Pili lakini bado kuna haja ya kulitafakari kwa kina suala hilo ili lisije leta usumbufu kwa Wananchi hao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  ya kuanzisha Miji Mipya Nchini, mbali ya kuwapatia Makaazi bora Wananchi walioathirika na Mvua za Masika lakini pia imelenga kupunguza Ongezeko kubwa la Idadi ya Watu wanaohamia sehemu moja ya Mji.
Balozi Seif  aliwakumbusha Wananchi walioathirika na Mvua za Masika kutambua kwamba wakati ukiwadia kuhamia katika Makaazi Mpya Nyumba zao zitalazimika kuvunjwa kwa vile ziko katika maeneo hatarishi kwa Maisha na Ustawi wa Viumbe.
Alisema maeneo mengi ya nyumba zilizoathirika ni yale  yenye vianzio vya Maji kama chem Chem,Visima  na sehemu za mabondeni zilizotengwa kwa shughuli za Kilimo mabazo hazipaswi kutumiwa kwa ujenzi wa Nyumba za Makaazi kwa vile zinahatarisha uchafuzi wa mazingira na afya za Wanaadamu.
Mapema Mshauri Elekezi wa Ujenzi wa Nyumba hizo za Makaazi ya Waathirika wa Mvua za Masika za Mwaka uliopita kutoka Kampuni ya Samkay Consult Cooperation Lilited Bwana Amour Hamad Omar alisema Awamu ya kwanza ya ujenzi huo utazingatia Nyumba 15 za Makaazi.
Mhandisi Amour alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Kwamba Majengo hayo ambayo kila Nyumba itakuwa na Familia Mbili utaambatana na uwepo wa njia za kupitishia Maji ya Mvua kila baaba ya Nyumba Nne ili kuufanya uwe Mji wa Kisasa.
Alisema Awamu ya Pili ya Ujenzi wa Nyumba hizo utakamilisha Majengo ya huduma za Msikiti, Kituo cha Afya, Soko, Maduka pamoja na uwepo wa huduma zote muhimu anazopaswa kuzipata Mwanaadamu katika harakati za Maisha yake ya kila siku.
Mshauri Muelekezi huyo wa Usimamizi wa Ujenzi wa Nyuma hizo alimthibitishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Ujenzi huo utazingatia muda halisi uliokubalika katika Mkataba wa Ujenzi ambao kwa mujibu wa hali halisi ya kuepuka msimu wamasika ujao mradi huo umepangwa kukamilika ndani ya Kipindi cha Miezi Minane badala ya ule wa mwanzo wa Mwezi Machi Mwaka 2020.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Haji Makame alisema eneo hilo tayari limeshapimwa na kuthibitisha kuwa na ukubwa wa Square Meter  9,315
Hata hivyo Ndugu Makame alimueleza Balozi Seif  kwamba kutokana na shauku ya Wafadhili ya kuonyesha nia ya kusaidia miradi ya Kiamii  katika maeneo mapya, maombi ya Uongozi wa Kamisheni hiyo umezingatiwa na kumepelekea Wataalamu wa Idara ya Ardhi kuongeza ukubwa wa Square Meter 2,400 ili liwe na ukubwa unaofanana na lile liliopo Tumbe Kisiwani Pemba.
Ziara kama ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi tayari ameshaifanya katika Kijiji cha Tumbe Mkoa wa Kaskazini Pemba kuangalia maandalizi ya Ujenzi wa Nyumba 30 za Makaazi ya Wananchi walioathirika na Mvua za Masika Kisiwani Pemba.
Ujenzi wa Makaazi ya kudumu ya Nyumba za Wananchi walioathirika na Mvua za Masika za Mwaka uliopita katika Kijiji cha Tumbe Kaskazini Pemba na Nungwi Kaskazini Unguja unafadhiliwa  na Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Umoja wa Falme za Kiarabu{ Red Cresent}.
Mradi huo Mkubwa wa utakapokamilika unatarajiwa kugharimu jumla ya Dola     Laki 850,000 za Kimarekani sawa na Shilingi za Kitanzania zipatazo Bilioni  Moja Nukta Nane, Tisa, Saba.{ 1,897,200.000/-}.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.