Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Atembelea Miradi ya Kijamii na Kufuatilia Changamoto Zinazowakabili Wananchi Katika Utekelezaji Miradi Hiyo.

 Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi akikagua Miradi ya Mendeleo ndani ya Jimbo lake na kuona changamoto zinazowakabilki Wananchi wake.
 Balozi Seif akizungumza na Wanafunzi, Walimu na Wazee wa Mangapwani mara baada ya kukagua mradi wa maji safi Skulini hapo na kuishauri Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “B” kuuongezea nguvu Mradi huo.
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, akizungumza na kutowa ahadi kwa Wananchi wa Vuga Mkadini kwamba Uongozi wa Jimbo hilo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya hiyo kukamilisha jengo lao walilolilenga kusomeshea Wananfunzi wa Maandili katika Elimu ya Msingi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pia ni Mwakiliushi wa Jimbo la Mahonda Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akitembelea moja ya daraka la Kijiji cha Matetema lililojengwa kuwaondoshea usumbufu Wananchi wa Ng’ambo ya Pili ya Kazole.Kulia Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kaskazini “B” ambae pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo Nd. Rajab Ali Rajab.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Mzee wa Kijiji cha Kazole Matetema wakati wa ziara yake kutembelea Miradi ya ya Maendeleo na kujionea changamoto wanazopambana nazo Wananchi wa Kijiji hicho mbele ya Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda  Balozi Seif kutokana na kutokamilika kwa Kisiwa chao cha Maji Safi na salama.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi, akikagua Jengo Jipya la Skuli ya Msingi ya Kitope, wakati wa ziara yake lililojengwa kwa nguvu za Wananchi ambalo  tayari limefikia hatua ya kukabidhiwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa hatua za ukamilishaji ujenzi wake kwa ajili kutowa huduma kwa Wanafunzi wa eneo hilo.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Wanafunzi wanaweza kuwa Watumishi wazuri wa Serikali, Taasisi, Mashirika ya Umma na hata Sekta  Binafsi endapo wataamua kuzingatia mafunzo wanayopewa wakati wanapotafuta Elimu.
Alisema utumishi utakaotukuka wa Kikazi hicho cha sasa utazidi kuleta faida na neema kama pia Wanafunzi hao watafuata malezi bora ya Majumbani na hata Mitaani kwa vile sehemu kubwa ya malezi yao yanategemewa kupatikana kwa Wazazi wao.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya miradi tofauti ya Kijamii pamoja na kufuatilia changamoto zinazowakabili Wananchi katika uendelezaji wa Miradi hiyo ndani ya Jimbo analoliongoza la Mahonda liliomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”.
Alisema utafiti unaonyesha wazi kwamba Watoto wengi wamebarikiwa kuwa na akili nyingi za kutosha Kimasomo lakini kinachokosekana ndani ya Jamii katika kuwaendeleza Watoto hao ni ushirikiano wa karibu kati ya Walimu na Wazazi katika baadhi ya Maeneo Nchini.
Balozi Seif alieleza kwamba katika suala zima la kumuandaa Mtoto katika mazingira salama ya kupata malezi sambamba na Taaluma Wazazi wanaendelea kubeba dhima ya kufuatilia nyendo za Watoto wao hasa katika vipindi vya masomo ya ziara kwa nyakati za Jioni au usiku.
Alisema nyakati hizo za ziada mara nyingi  huonekana kutoa mwanya kwa baadhi ya Wanafunzi watukutu kufanya vitendo vilivyo nje ya Maadili yao na matokeo yake wengine huishia kupata Mimba za Utotoni jambo linalowasababishia kuacha kuendelea na masomo yao.
Kwa upande wa Walimu Balozi Seif  aliwakumbusha kuwasiliana na Wazazi wa wanafunzi pale wapothibitisha uwepo wa Tabia chafu za Mwanafunzi wakati wa masomo yao madarasani.
Katika ziara hiyo Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda alikagua Tangi la Maji safi na Salama liliopo katika Skuli ya Msingi ya Mangapwani na kuushauri Uongozi wa Hamashauri ya Wilaya ya Kaskazini “B”  kuangalia uwezekano wa kuwekwa kwa Tangi jengine kubwa la Maji ili kukidhi mahitaji ya Wanafunzi, Walimu pamoja na Baadhi ya Wananchi wanaoizunguuka Skuli hiyo.
Baadae Balozi Seif akakagua maendeleo ya Ujenzi wa Jengo Jipya lililolengwa kutumiwa na Wanafunzi wa Skuli ya  Maandalizi  ya Vuga Mkadini  kwa masomo ya Msingi hapo baadae na kuona Tangi la Maji ambalo kwa sasa linahitaji kuwekwa jengine kubwa kutokana na mahitaji zaidi ya Wananchi.
Balozi Seif aliwaeleza Wananchi wa Shehia hiyo ya Vuga Mkadini kwamba Uongozi wa Jimbo la Mahonda utashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “B” katika kuongeza nguvu za kukamilishwa kwa Jengo hilo kwa hatua ya Kifusi, Plasta na Saruji.
Akilikagua Daraja lililojengwa katika Bonde la  Matetema  ambalo litasaidia kuondosha usumbufu kwa Wananchi wa Ng’ambo ya Kazole Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda  aliwatahadharisha Viongozi wanaosimamia miradi ya Kijamii kuwa makini na Makandarasi wababaishaji.
Balozi Seif alisema miradi mingi ya Kijamii Majimboni huzorota au mengine kufifia kabisa kutokana na baadhi ya Viongozi kuwapa jukumu hiyo jamaa na marafiki zao kwa nia ya kumsaidia riziki lakini hatma yake hakuna kinachozingatiwa katika ukamilishwaji wa miradi hiyo kutokana na Ujamaa uliotawala katika mkazi hizo za Kijamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.