Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Awataka Wahitimu wa Kidatu Cha Sita Kutumia Vizuri Zawadi Zao Kuendeleza Ndoto Zao za Elimu Ili Kuweza Kufaulu Elimu ya Juu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia Maonyesho ya Fani ya Ufundi ya Wanafunzi wa Skuli wa Vidato vya Sita Mkoa Mjini Magharibi waliofaulu vyema na kupata zawadi ya Laptop.

Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameitahadharisha Jamii kuendelea kuepuka Rushwa  sehemu zote yenye madhara makubwa yanayosababishwa na uwepo wa uadui unaotokana na kupindwa kwa Haki ya Mtu anayestahiki kupewa.
Alisema rushwa akitolea mfano ikitawala  katika Sekta ya Elimu husababisha wasiokuwa na uwezo wa kufaulu na kupasisha Watu ambao madhara yake  huibua Wafanyakazi dhaifu katika Taasisi za Umma wasio na upeo na uchungu wa Taifa lao.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akikabidhi zawadi za Laptop kwa Wanafunzi wa Mkoa Mjini Magharibi waliofanya vizuri katika Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Sita Mwaka 2018 hafla iliyofanyika katika Mnara wa Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar uliopo Michenzani Mjini Zanzibar.
Alisema Watendaji wengi waliopata ajira kwa kutumia njia ya mkato ya rushwa kutokana na vyeti vyao bandia huviza Maendeleo ya Taifa jambo ambalo ni hatari ya kuwa na Taifa lege lege hapo baadae.
Balozi Seif alizipongeza na kuzishukuru Taasisi na Mashirika mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa zikiwemo pia Jumuia za Kiraia kwa kuendelea kutoa michango yao katika kuimarisha Sekta ya Elimu Nchini.
Alieleza kwamba kipindi kirefu kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne na Sita hapa Zanzibar hakikuwa cha kuridhisha hali ambayo imepeleka Taasisi zinazohusika na suala la Elimu kubainisha changamoto zilizopo na kutafuta njia ya kukabiliana nazo.
Alisema Mikakati kadhaa ya muda mfupi na mrefu imewekwa na kutekelezwa katika ngazi ya Wizara na Mkoa ili kubadilisha hali hiyo na kushuhudia matokeo mazuri ya Mwaka huu katika Mtihani wa Kidato cha Sita matokeo ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajivunia sana.
Balozi Seif alifahamisha kwamba tukio lililowakutanisha wadau wa Elimu Uwanja wa Kumbu kumbu ya Mapinduzi ya Zanzibar Kisonge ni matunda ya jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kusimamia vyema na kutekeleza Mipango na Mikakati mbali mbali ya kisekta kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu Visiwani Zanzibar.
Alieleza kwamba Sekta ya Elimu ni miongoni mwa maeneo yaliyopewa  kipaumbele na Serikali hivyo jitihada zinazochukuliwa na Uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi ni hatua nzuri yenye kuunga mkono jitihada za Serikali Kuu za kuimarisha Miundombinu ya kuweka mazingira bora yatakayowezesha kuinua viwango vya ufaulu.
Akizungumzia suala la ufaulu na nidhamu Maskulini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwaasa wanafunzi kujikita zaidi katika kuzingatia masuala hayo yatakayowawezesha kukamilisha masomo yao kwa mafanikio na ufaulu mkubwa.
Balozi Seif alisema kwamba lazima wanafunzi wote watambue kwamba ufaulu na nidhamu ni Watoto pacha mambo yanayowajengea heshima wanafunzi kukubalika katika Jamii iliyomzunguuka.
Alifahamisha kwamba  nidhamu kwa upande wake ina umuhimu mkubwa  katika kumsaidia Mwanafunzi katika ufaulu wake  na kupata matokeo mazuri katika masomo yake, ufaulu unaotokana na asilimia 60% kwake mwenyewe na asilimia 40%  inayotokana na Mwalimu.
Kuhusu suala la vitendo vya udhalilishaji wa Kijinsia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema janga hilo lililoshamiri katika kipindi cha kati linadhoofisha ufaulu wa wanafunzi katika masomo yao.
Balozi Seif alisema ni vyema Jamii ikaendelea kuungana pamoja katika kupiga vita vitendo hivyo na kuondoa muhali wa aina zote katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba.
Alitahadharisha kwamba wasiposhughulikiwa na kuchukuliwa hatua sasa wenye vitendo vya udhalilishaji hakutakua na Jamii madhubuti hapo baadae kwa lugha nyengine kuwaachia  watu wenye vitendo hivyo ni sawa na kuyaachia maradhi ya saratani yaendelee kuathiri mwili.
Mapema Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimkiwa Ayoub Mohamed Mahmoud alisema matokeo ya Kidato cha Sita ya Mwaka 2017 yameleta faraja na kuuvua macho Mkoa mkoa ambo ndio kitovu cha Elimu hapa Zanzibar.
Mh. Ayoub alisema jitihada zitaendelea kufanywa kwa kuanzisha Mikakati mbali mbali itakayowawezesha Wanafunzi kudumu vyema katika kukabiliana na Mitihani yao ya Taifa.
Alisema jitihada hizi zina lengo la kuwaandaa Wataalamu watakaolivusha Taifa hili Kimaendeleo licha ya changamoto kubwa ya kuenea kwa vilabu vya pombe  vilivyochangia kuathiri baadhi ya Wanafunzi tabia ambayo Uongozi wa Mkoa wake ulijikita kupambana navyo.
Alielezea matumaini yake kwamba Zanzibar mpya itauza Wataalamu wengi wataowenza kutoa huduma ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki katika fani za Afya, Kilimo, wahandisi na hata Teknolojia ya Kisasa.
Mkuu huyo wa  Mkoa Mjini Magharibi alifahamisha kwamba hivi sasa zipo juhudi maalum za kuweka mkakati kwa wanafunzi wanaojiandaa kufanya mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne na kuweka milango wazi kwa Wananchi, Makampuni au Taasisi zitakazoguswa na Sekta hiyo muhimu kwa taifa.
Akimkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Elimu na Mfunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma aliupongeza Uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kwa jitihada zake za kuunga mkono Sekta ya Elimu inayoonekana kupiga hatua siku hadi siku.
Mh. Riziki pia akaishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Uongozi mahiri wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein kwa kutoa fursa 30 za Mafunzo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa Zanzibar wanaomaliza vyema masomo yao ya Darasa la 14.
Alisema  Serikali inaendelea kujali jitihada za Wanafunzi hao na kuahidi kuongeza fursa nyengine kadri hali ya Uchumi itaklavyoruhusu.
Hafla hiyo fupi ya kuwazawadia  Laptop Wanafunzi 96 wa Skuli 17 za Kidato cha sita Mkoa Mjini Magharibi imehudhuriwa pia na wadau mbali wa Sekta ya elimu wakiwemo pia Wawakilishi wa Jumuiya za Kiraia, Taasisi za Kujitolea pamoja na Viongozi wa Kisiasa kutoka  Vyama mbali mbali Nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.