Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Azungumza na Ujumbe wa Mamlaka ya Uhifadhi wa Nyaraka na Makumbusho wa Serikali ya Oman.

 Mwenyekiti  wa Mamlaka ya Uhifadhi Nyaraka na Makumbusho wa Serikali ya Oman Dr. Hamed  Mohammed Al- Dhawiyan Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Ofisini kwake kwa mazungumzo.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akizungumza na Ujumbe wa Mamlaka ya Uhifadhi Nyaraka na Makumbusho wa Serikali ya Oman  ukiongozwa na Mwenyekiti wake Dr. Hamed  Mohammed Al- Dhawiyan.
Mwenyekiti wake Dr. Hamed  Mohammed Al- Dhawiyan aliyevaa kilemba akielezea msimamo wa Serikali ya Oman kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati za Maendeleo.Kulia ya Dr. Hamed ni Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar  Bwana Hamoud Al – Habsy.
Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mh., Mahmoud Thabit Kombo akitoa ufafanuzi wa Majengo ya Kihistoria yanayoendelea na matengenezo makubwa ambayo yamepata ufadhili wa Serikali ya Oman.
Balozi Seif akipokea zawadi Maalum kutoka kwa Mwenyekiti wa Mamlaka ya Uhifadhi Nyaraka na Makumbusho wa Serikali ya Oman  Dr. Hamed  Mohammed Al- Dhawiyan.
Dr. Hamed  Mohammed Al- Dhawiyan akipokea zawadi ya mlango kutoka kwa Balozi Seif ikiwa ishara ya kuwekewa mlango wazi wakati wowote yeye na Viongozi wenzake wanapoamua kutaka kutembelea Zanzibar. Picha na – OMPR – ZNZ.


Na.Othman Khamis OMPR.
Oman ina wajibu wa kuendelea kuunga mkono harakati za Maendeleo za Zanzibar kufuatia uhusiano wa Kihistoria wa ndefu uliyopo baina ya pande hizo mbili zenye muingiliano wa Kidamu wa Watu wake.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Uhifadhi Nyaraka na Makumbusho wa Serikali ya Oman Dr. Hamed  Mohammed Al- Dhawiyan wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Dr. Hamed  Mohammed alisema Miradi ya Kijamii ikiwemo ile ya Kihistoria pamoja na Majengo ya Kale  yanayojengwa na yaliyopata baraka ya kutaka kujengwa na Zanzibar chini ya msaada na ufadhili wa Serikali ya Oman ni dalili ya kuendeleza udugu wa pande hizo mbili.
Alisema Oman katika juhudi za kuendelea kuitanga Zanzibar Kimataifa hasa katika masuala ya Kihistoria imeandaa Mkutano wa Kimataifa wa masuala ya Historia baina ya Oman na Zanzibar Nchini Ujerumani lengo likiwa kuutangaza uhusiano wa kidamu ulipo kati ya Nchi hiyo mbili.
Mwenyekiti  huyo wa Mamlaka ya Uhifadhi Nyaraka na Makumbusho wa Serikali ya Oman alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Taifa hilo halitasita kutumia Utaalamu na ufadhili iliyonao katika kuendelea kusaidia mambo mbali mbali ambayo Zanzibar itahisi kwamba yanaweza kufanywa.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  alisema ziara za mara kwa mara zinazowajumuisha Viongozi wa ngazi za juu wa pande zote mbili zinachangia kuimarisha Afya ya uhusiano huo.
Balozi Seif alimueleza Mwenyekiti huyo wa Mamlaka ya Uhifadhi Nyaraka na Makumbusho kwamba kitendo cha Serikali ya Oman chini ya Mfalme Qaboos cha kuwapa nafasi za juu za Uongozi Wananchi wenye asili ya Zanzibar ni thamani kubwa waliyonayo Waoman kwa ndugu zao wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea faraja yake kubwa aliyonayo kutokana na Oman kusaidia Ujenzi wa Msikiti Mkubwa wa Ijumaa Mazizini pamoja na Matengenezo ya Jumba la ajabu Forodhani, majengo  yatayoweka alama kubwa ya uhusiano wa pande hizo mbili.
Mapema Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo alisema ujenzi wa Jengo la Ajab Forodhani unaofadhiliwa na Serikali ya Oman kwa thamani ya Dola za Kimarekani Milioni Tano                  {US  5,000,000} hivi sasa unakamilisha awamu ya kwanza.
Mh. Mahmoud alisema awamu ya pili ya matengenezo makubwa ya Jumba hilo yanatarajiwa muda mfupi ujao huku program za matengenezo Makubwa ya majengo mengine kama Makumbusho ya Kifalme {Peoples Palace} yaliyopo Mizingani  bado mazungumzo yakiendelea vyema kati ya Serikali za Oman na Zanzibar.
Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar aliipongeza na kuishukuru Serikali ya Oman kwa Msaada wake wa  Vifaa mbali mbali kwa ajili ya huduma za Idara ya Nyaraka Zanzibar na Mambo ya Kake.
Ujumbe wa Mamlaka ya Uhifadhi Nyaraka na Makumbusho ya Serikali ya Oman ukiongozwa na Mwenyekiti wake Dr. Hamed  Mohammed Al- Dhawiyan uko Zanzibar kwa ziara maalum ya kutembelea Sekta  inayohusiana na Masuala ya Historia.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.