Habari za Punde

Hotuba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Katika Utoaji wa Zawadi Kwa Wanafunzi 96 Waliofanya Vizuri Mitihani Yao Kwa Mwaka 2017/2018.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi muhitimu wa Kidatu cha Sita Zanzibar Mwanafunzi Fahad Rashid Salum kwa kupata Division 1.3 , zawadi ya Komputa (Laptop) zilizotolewa na Kampuni ya Rom Sulution Ltd, ahadi ilioitowa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja kwa Wanafunzi 96 waliofanya vizuri mitihani yao ya Kidatu cha Sita kwa Skuli 17 za Mkoa wa Mjini Magharibi.


Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini /Magharibi,
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
Wenyeviti wa Chama cha Mapinduzi , Mkoa wa Mjini/ Magharibi,
Ndugu Walimu na Wanafunzi,
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana.

Assallam Aleykum,

Awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kutuwezesha kuwa hai leo hii tukiwa wazima wa afya na tukaweza kujumuika katika tukio hili muhimu kwa maendeleo ya elimu katika Mkoa wa Mjini/Magharibi na Zanzibar kiujumla.  Nichukue nafasi hii tena kuushukuru Uongozi wa Mkoa wa Mjini/Magharibi kwa kunipa heshima hii kubwa ya kujumuika nanyi jioni hii katika sherehe ya kukabidhi zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi katika matokeo mazuri ya kidato cha sita kwa mwaka 2018.

Ndugu Wananchi,

Tukio lililotukutanisha hapa ni matunda ya jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kusimamia vyema na kutekeleza mipango na mikakati mbali mbali ya kisekta kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu hapa Zanzibar.  Sekta ya Elimu ni miongoni mwa sekta zilizopewa kipaumbele sana na Serikali, hivyo, jitihad zinazochukuliwa na uongozi wa Mkoa wa Mjini/Magharibi ni hatua nzuri yenye kuunga mkono jitihada za Serikali Kuu za kuimarisha miundombinu na kuweka mazingira bora yatakayowezesha kuinua viwango vya ufaulu kwa wanafunzi wote wa skuli za Msingi na Sekondari ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015 – 2020.

Ndugu Wananchi,

Kwa heshima kubwa napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa jitihada zake binafsi na mkazo anaouweka katika kukuza elimu hapa Zanzibar. Ni dhahiri kuwa mafanikio yanayopatikana ni matunda ya miongozo na maelekezo anayoyatoa kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na viongozi wengine katika ngazi ya Mikoa na Wilaya. Sote ni mashahidi kuwa nchi yetu imepiga hatua kubwa ya maendeleo katika sekta zote, hali ambayo imeimarisha utoaji wa huduma bora za jamii ikiwemo elimu bora katika maeneo yote ya Unguja na Pemba.

Ndugu Wananchi,
Kwa kipindi kirefu kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne na cha sita hapa Zanzibar hakikuwa cha kuridhisha, hali ambayo imepelekea Taasisi mbali mbali zinazohusika na suala la elimu kubainisha changamoto zilizopo na kutafuta njia ya kukabiliana nazo ili kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wetu.  Mikakati kadhaa ya muda mfupi na mrefu imewekwa na kutekelezwa katika ngazi ya Wizara na Mkoa ili kubadilisha hali hiyo na tumeshuhudia matokeo mazuri ya mwaka huu kwa mtihani wa kidato cha sita, matokeo ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajivunia sana.

Ni jambo la kutia moyo na faraja kubwa kuona kuwa Mkoa wa Mjini/Magharibi umeondoka katika idadi ya Mikoa yenye skuli nyingi zilizofanya vibaya Tanzania, kwa matokeo ya mwaka huu zaidi ya wanafunzi 1264 sawa na asilimia 94 ya wahitimu wamepata madaraja (I - III) yanayowawezesha kuendelea na elimu ya juu katika Vyuo Vikuu vya ndani na nje ya nchi na hivyo kujenga matumaini mapya kwa Zanzibar.

Ndugu Wananchi,

Natoa pongezi kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kwa jitihada mbali mbali za kuinua elimu hapa Zanzibar. Napenda kumpongeza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali kwa utendaji mahiri wa Wizara yake na kwa hakika matunda yake tunayaona katika sekta nzima ya elimu na hasa leo hii kwa matokeo haya mazuri ya mtihani wa kidato cha sita. Kwa dhati kabisa, nimpongeze Mkuu wa Mkoa wa Mjini/Magharibi, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud na watendaji wake kwa jitihada zao kubwa zilizoleta mafanikio haya. Hatua iliyochukuliwa na Mkoa ya kuamua kuweka kambi kwa wanafunzi wote ili wajiandae na mitihani yao kwa kuwa karibu na walimu watakaoweza kuwasaidia ni ya kupigiwa mfano. 

Ndugu Wananchi,

Nimeelezwa kuwa Mkoa kupitia Taasisi ya MIMI na WEWE Foundation imeweza kugharamia kambi hizo kwa chakula na mahitaji mengine pamoja na upatikanaji wa vitabu vya mazoezi na mitihani iliyopita ambavyo vilisaidia sana. Suala la kuwapa motisha wanafunzi ni jambo la msingi sana, nimpongeze kwa mara nyengine tena Mkuu wa Mkoa wa Mjini/Magharibi kwa kuwapa moyo na ari wanafunzi hawa kwa kuwaahidi zawadi ya kompyuta kila mwanafunzi atakaefaulu kwa daraja la kwanza, hatua mbayo imewezesha kupatikana kwa wanafunzi 96 wenye daraja la kwanza. Niwashukuru sana washirika wetu wa maendeleo Kampuni ya ROM Solution kwa kuunga mkono jitihada za Mkoa na kutoa kompyuta zote 96 nitakazozikabidhi kwa wanafunzi hivi punde.

Ndugu Wananchi,
Akili inayong’ara ni chem chem neemevu inayomuendeleza mtu mbele zaidi kuliko mahitaji ya kidunia na inamjuilisha ulimwengu mwengine pia. Fikra nzito na za hali ya juu,, humzuia mwerevu asidanganyike na ulimwengu, afuate masuala ya msingi katika maisha yake na ndio maana Mtume wetu Muhammad (SAW) akasema ninakuu:-

          “Jifundisheni elimu na kuweni wanyenyekevu na watiifu kwa wanao      kusomesheni”.

Hivyo utaona suala la nidhamu kwa mwanafunzi kwa walimu ni jambo lisiloepukika na ni amri kutoka kwa Bwana Mtume (SAW).

Ndugu Wananchi,
Tutambue kuwa ufaulu na nidhamu ni watoto pacha. Mwanafunzi mzuri ni yule mwenye nidhamu. Kwa kiasi kikubwa nidhamu husaidia kujenga ufaulu vyuoni na maskulini. Nidhamu kwa upande wake ina umuhimu mkubwa katika kumsaidia mwanafunzi katika ufaulu wake na kupata matokeo mazuri katika masomo yake.  Ufaulu wa mwanafunzi unatokana na asilimia 60 kwake mwenyewe na 40 ndiyo inatokana na Mwalimu.
Katika zawadi tutakazotoa leo, napenda kutoa wasia wangu kwenu juu ya umuhimu wa suala zima la nidhamu.  Hivyo, nidhamu ndiyo itakayowawezesha kukamilisha masomo yenu kwa mafanikio na ufanisi mkubwa huko mwendako. 
Ndugu Wananchi,
Kwa namna ya kipekee naomba kutoa pongezi zangu kwa walimu, wazazi na wanafunzi wote mliotupatia heshima hii kubwa kwa matokeo mazuri katika mtihani huu wa kidato cha sita.  Nawaomba walimu na wazazi muendelee kushirikiana katika malezi bora ya watoto wetu na niwahakikishie kuwa Serikali iko pamoja nanyi na inatambua na kuthamini jitihada zenu. Nizidi kuwaomba wadau mbali mbali wa elimu hapa Zanzibar kama MIMI na WEWE Foundation, Greenlight Foundation na Mashirika mbali mbali kuendelea kutoa michango yenu katika kuimarisha maendeleo ya elimu Unguja na Pemba.   Nimeelezwa kuwa tayari Mkoa umeshaandaa Mkakati wa kuinua ufaulu wa Kidatu cha Nne, niwaombe wafanya biashara, wananchi na wadau wengine wote muendelee kuunga mkono jitihada za Mkoa na Wizara katika kuinua ufaulu kwa wanafunzi wetu.

Ndugu Wananchi,
Tutambue kuwa rushwa ni adui wa haki.   Nikiwa kiongozi wa Kitaifa Serikalini naelewa madhara ya rushwa.  Rushwa huviza maendeleo ya nchi na wananchi wakiwemo wanafunzi.  Rushwa katika elimu husababisha wasiokuwa na uwezo wa kufaulu na kupasishwa ambao madhara yake huwa na wafanyakazi dhaifu wasio na upeo na uchungu na nchi yao.  Watendaji hao wengi wao ndio huviza maendeleo ya Taasisi za Umma na huwa wasomi pesa baada ya kutoa huduma kwa wananchi nakuombeni mtakapomaliza masomo yenu msiwe wasomi pesa.
Ndugu Wananchi,
Suala la udhalilishaji linadhoofisha ufaulu wa wanafunzi katika masomo yao.  Ni vyema tukaungana pamoja katika kupiga vita vitendo hivyo na kuondoa muhali wa aina zote katika jamii yetu.  Kwani Waswahili wanasema:  “Usipoziba ufa utajenga ukuta”.  Tusipowashughulikia na kuwachukulia hatua sasa wenye vitendo vya udhalilishaji basi tujue hatutakuwa na jamii madhubuti kwa baadae.  Tuelewe na kutambua kuwa sisi ni wachunga na kesho tutaulizwa kwa tulichokichunga, kuwaachia watu wenye vitendo hivi ni sawa na kuiachia kansa kwenye mwili, tuwafichue na tuwapeleke katika vyombo vya sheria.

Ndugu Wananchi,
Matumizi ya dawa za kulevya ni adui mkubwa kwa vijana na nguvu kazi ya Taifa letu.  Tuhakikishe tunakuwa waadilifu katika kupiga vita na kupambana na wafanya biashara na watumiaji wa dawa za kulevya katika hali zote.
Wazee wenzangu tukumbuke Mzee Luqman alivyomuusia mwanawe katika Surati Luqman aya ya 17; na ninamnukuu:
       
                  “Ewe mwanangu, zihifadhi sala na amrisha kila wema, na kataza kila                 baya na stahamili kwa shida zinazokusibu.  Hakika anayousia Mwenyezi            Mungu ni katika mambo ambayo yanahitajia kufanyiwa hima na          kuyashikilia.”

Madawa ya kulevya ni jambo baya, na wauzaji ni watu wabaya, hivyo vijana tuwafichue na ni vyema tukatazane matumizi ya madawa hayo.  Pia naomba tujitahidi kuamrishana mema na kukatazana mabaya ikiwemo kuitunza na kuilinda amani ya nchi yetu sambamba na kuwa watiifu kwa Viongozi na Serikali yenu,

Ndugu Wananchi,
Nimalizie hotuba yangu kwa kuwashukuru tena waandaaji wa shughuli hii, na niwatakie kheri wanafunzi katika masomo yenu katika Vyuo mtakavyojiunga, lakini pia niwaase wale mnaojiandaa na mitihani ya Kidato cha Nne kujiandaa vizuri ili nanyi mpate matokeo mazuri yatakayowawezesha kuendelea na elimu ya Sekondari ya juu.
Mwisho niwapongeze Msoma Quran wetu, wasoma utenzi wetu pamoja na aliyetunga.  Pia niwashukuru wasanii wetu waliotutumbuiza.

Baada ya kusema hayo sasa niko tayari kukabidhi zawadi kwa wanafunzi.


AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.