Habari za Punde

Vyuo Vikuu Bora Duniani Vinavyowapendeza Waajiri Zaidi Afrika.

Baada ya Wahitimu, wa Vyuo Vikuu wakiwa katika mahafali baada ya kumaliza Masomo yao na kutafuta Ajira.
Chanzo cha Habari BBC.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti wa 'Kuajirika kwa Wanaofuzu na Shahada Duniani wa 2019' ambao umefanywa na kampuni ya QS Group na huwa kiashiria cha matumaini ambayo wanafunzi wanaweza kuwa nayo wakitafuta kazi baada ya kufuzu.
Aidha, huwa ni kiashiria kwa vyuo vikuu kwamba vinafaa kujivunia kazi na juhudi zao.
Kampuni ya QS Group pia hutayarisha Orodha ya Vyuo Vikuu Bora Duniani.
Orodha ya sasa imetayarishwa baada ya kutafuta maoni ya waajiri 42,000 kote duniani na ni kiashiria cha chuo kikuu gani kinapendwa zaidi na waajiri.
Waajiri waliulizwa kuhusu ni wapi watu wenye shahada walio na "ujuzi zaidi, ubunifu na uvumbuzi na wanaomudu kazi vyema zaidi" hutoka.
Orodha hiyo pia huzingatia takwimu za idadi ya wanafunzi waliohitimu vyuo mbalimbali ambao huajiriwa, ni wapi watu wenye vyeo vya juu mashirika mbalimbali walisomea na pia ushirikiano uliopo baina ya vyuo vikuu na waajiri mbalimbali.
Kwa jumla duniani, Massachusetts Institute of Technology (MIT) ndicho chuo kikuu kinachoongoza.
Vyuo vikuu vya Marekani vinashikilia nafasi nne za kwanza MIT, Stanford, University of California, Los Angeles (UCLA), na Harvard, ambapo wanafunzi wake hutafutwa zaidi na waajiri.
Majengo ya Chuo Kikuu cha MIT ndicho chuo kikuu kinachoongoza kwa kupendwa na waajiri.
MIT hufahamika sana kwa ufanisi wake katika teknolojia na uvumbuzi.
Wanafunzi waliosomea chuo kikuu hicho ni pamoja na mwanaanga Buzz Aldrin, katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan aliyefariki mwaka jana, na Amar Bose, mtaalamu wa uhandisi wa sauti ambaye kwa sasa ni bilionea.
Stanford, wanashikilia nafasi ya pili na wamekuwa ndio kitovu cha wasomi wengi wanaoangazia na kutafiti kuhusu uvumbuzi Silicon Valley. Wanafunzi wa zamani ni kama vile waanzilishi wa Google Larry Page na Sergey Brin na mwanzilishi wa Netflix Reed Hastings.
Orodha hiyo inaonesha vyuo vikuu vya Australia vimeanza kuimarika, ambapo University of Sydney na University of Melbourne vinashikilia nafasi ya tano na sita mtawalia.
Vyuo hivyo havijawahi kujumuishwa katika vyuo vikuu 30 bora katika Orodha ya Vyuo Vikuu Bora Duniani ya QS, lakini vinaonekana kupendwa sana na waajiri.

Kushindania nafasi za kazi

Ben Sowter, mkurugenzi wa utafiti katika QS, anasema vyuo vikuu vinavyosifika kwa utafiti duniani si lazima viwe ndivyo vinavyopendwa na waajiri.
Amesema pia kwamba gharama ya karo na ushindani sokoni vimesababisha wanafunzi kuangazia zaidi uwezekano wao kuajiriwa baada ya masomo na mafanikio yao ya baadaye.
Cambridge ndicho chuo kikuu cha Uingereza kilichoorodheshwa cha juu zaidi katika nafasi ya 10.
University College London ni cha 18. Kwa kuangazia sifa za vyuo vikuu miongoni mwa waajiri, Cambridge na Oxford ndivyo vinavyoongoza, lakini kwa jumla vyuo vikuu vya Uingereza vilishuka katika ushirikiano na waajiri na viwango vya kuajiriwa kwa wanafunzi wao.
Kuimarika kwa China kunadhihirishwa na kuorodheshwa kwa Tsinghua University nafasi ya tisa na University of Peking nafasi ya 20.
Kati ya vyuo vikuu 500 vilivyoorodheshwa, 102 vinatoka bara Asia, 144 kutoka Ulaya Magharibi. Marekani ina vyuo vikuu 83, ambapo 13 kati ya vyuo hivyo vimo katika orodha ya 30 bora. Afrika kuna vyuo vikuu 10.
Chuo hicho kikuu cha Nairobi ndicho pekee kutoka Afrika Mashariki ingawa kimeshuka kutoka nambari tano Afrika mwaka 2018, mwaka ambao kulikuwa na vyuo vikuu 11 vya Afrika katika vyuo vikuu 500 bora duniani kwenye orodha hiyo.
Vyuo Vikuu vinavyopendwa na waajiri Afrika 2019
  1. University of Cape Town, Afrika Kusini
  2. The American University in Cairo, Misri
  3. University of Witwatersrand, Afrika Kusini
  4. Cairo University, Misri
  5. Ain Shams University, Misri
  6. Stellenbosch University, Afrika Kusini
  7. University of Johannesburg, Afrika Kusini
  8. University of Kwazulu-Natal, Afrika Kusini
  9. University of Nairobi, Kenya
  10. University of Pretoria, Afrika Kusini
Chuo kikuu cha Alexandria cha Misri ndicho kilichotupwa nje katika orodha ya mwaka huu baada ya kuwa nambari nane Afrika mwaka uliopita.
Chuo kikuu cha Cape Town ambacho kinaongoza Afrika katika orodha ya jumla kinashikilia nafasi ya 101-110, na hakuna chuo kingine cha Afrika hadi baada ya vyuo mia ambapo ndipo unapata chuo kikuu cha Kimarekani cha Cairo na Chuo Kikuu cha Witwatersrand cha Afrika Kusini katika nafasi ya 201-250.
Chuo Kikuu cha Nairobi kinashikilia nafasi ya 301-500. Mwaka jana, kilikuwa katika nafasi ya 251-300 kwa jumla.



Mwaka 2017, Afrika ilikuwa na vyuo vikuu vinne pekee, wakati huo orodha hiyo kwa jumla ikishirikisha vyuo vikuu 300 duniani. Mwaka 2017 walishirikisha vyuo 494 na mwaka huu vyuo 497.
Majengo ya Chuo Kikuu cha Cambridge ndicho chuo kinachoongoza Uingereza.

Vyuo vikuu 30 bora duniani kwa kupendwa na waajiri

  1. Massachusetts Institute of Technology, US
  2. Stanford University, US
  3. University of California, Los Angeles, US
  4. Harvard University, US
  5. University of Sydney, Australia
  6. University of Melbourne, Australia
  7. University of Cambridge, UK
  8. University of California, Berkeley, US
  9. Tsinghua University, China
  10. University of Oxford, UK
  11. New York University, US
  12. University of Toronto, Canada
  13. University of Hong Kong, Hong Kong
  14. Yale University, US
  15. ETH Zurich, Switzerland
  16. Princeton University, US
  17. Columbia University, US
  18. University College London, UK
  19. University of Tokyo, Japan
  20. Peking University, China
  21. Cornell University, US
  22. University of Chicago, US
  23. Seoul National University, Korea Kusini
  24. University of Pennsylvania, US
  25. University of Michigan, US
  26. ( sawa na 25) University of Waterloo, Canada
  27. Fudan University, China
  28. Waseda University, Japan
  29. University of New South Wales, Australia
  30. Ecole Polytechnique, Ufaransa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.