Habari za Punde

Kuwepo na utamaduni wa kubadilishana mawazo na kushirikiana katika mambo ya Katiba na Sheria: Waziri Haroun

Na Raya Hamad ORKSUUUB

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora  Mhe Haroun Ali Suleiman Mhe Haroun Ali Suleiman ametaka kuwepo kwa utamaduni wa kubadilishana mawazo na kushirikiana juu mambo mbali mbali yanayohusu Katiba Sheria  ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa 

Waziri Haroun ameyasema hayo wakati alipokutana  na Waziri wa Katiba na Sheria Prof.Palamagamba Kabudi  wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ofisini kwake Mazizini  ambapo wamekubalina kushirikiana  pamoja kwa baadhi ya masuala yanayohusu na  yasiyohusu Muungano 

“ wizara zetu hasihusiani na Masuala ya Muungano lakini si vibaya tukawa tunashirikiana baadhi ya mambo mfano ndani ya Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na Baraza la Wawakilishi mara nyingi linapokuja  suala la Katiba changamoto nyingi  zinajitokeza  hivyo changamoto hizi zinapokuja na tukiwa na mashirikiano ya karibu hazitakuwa kikwazo ” 

Zanzibar ina Katiba yake na Tanzania ina Katiba yake lakini kumekuwa kukijitokeza mijadala ya mara kwa mara hasa  suala la Katiba hivyo  Mawasiliano ya mara kwa mara hasa yanayohusu mijadala ya Katiba na sheria  itasaidia sana kiutendaji na  kiutekelezaji kwa kuondosha kasoro ndogo ndogo zilizopo na kutekeleza  majukumu ya Taasisi hizi kwa ufanisi 

Nae Prof. Palamagamba Kabudi  ametilia mkazo baadhi ya maeneo ambayo yanahitaji  ushirikiano zaidi ikiwemo kushirikiana kwenye Utungaji wa sheria, mafunzo juu ya uandishi wa sheria kwa kutumia lugha ya Kiswahili ambapo Zanzibar ndio kunakopatikana lugha fasaha ya Kiswahili  “Watanzania wetu ni waswahili na wasomaji wetu ni waswahili ”alisisitiza waziri huyo

Aidha eneo jengine ni suala la kushirikiana katika mafunzo yakiwemo ya Mahakimu , waendesha mashtaka ambapo ameahidi kuleta watendaji ili kubadilishana uzowefu na kujifunza zaidi mbinu na mikakati katika kupata mafanikio 

 Prof . Kabudi pia amesifu juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hasa katika kusimamia masuala ya Katiba na Sheria na kuona umuhimu wa kuzibadilisha sheria ambazo zimeshapitwa na wakati na zile ambazo zinahitaji kufanyiwa marekebisho .

Mawaziri hao kwa pamoja wamekubaliana  kukaa na kubainisha maeneo ambayo yanahitaji kuongeza ushirikiano ili kuhakikisha pande zote mbili zinanufaika kwa kuwashirikisha watendaji wakuu ili wakae pamoja na  kupanga mikakati endelevu ya ushirikiano ikiwemo fursa mbali mbali za mafunzo ndani na nje ya nchi , kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka Tanzania Bara kuja Zanzibar na Zanzibar  kwenda Tanzania Bara .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.