Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Akiendelea na Ziara Yake Kisiwani Pemba Kutembelea Miradi ya Maendeleo.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akitembelea Skuli ya Sekondari ya Uwelezni kuangalia maendeleo ya Ujenzi wa Jengo jipya la gorofa ili kukidhi mahitaji ya ongezeko la Wanafunzi Skulini hapo.
Muonekano ya Jengo jipya la Madarasa Sita linalojengwa katika Skuli ya Sekondari ya Uweleni kwa nguvu za Walimu, Wazazi na Wahisani mbali mbali likiwa katika hatua za uwezekaji ambazo zimeshachukuliwa na Wizara ya Elimu Zanzibar.
Balozi Seif akizungumza na Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Uweleni hawapo pichani mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo jipya la Skuli hiyo loinalojengwa kwa nguvu za Walimu, Wazazi na Baadhi ya Wahisani.
 Baadhi ya Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Uweleni wakimsikiliza Balozi Seif wakati akiwanasihi kujikita zaidi katyika masomo yao ili waje kuwa Viongozi bora wa Baadaye.


Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameonya kumuwajibisha Kiongozi au Mtendaji yeyote wa Wizara ya Afya atakayehusika na ucheleweshaji wa ununuzi wa Vifaa vya kupoza Umeme kwa ajili ya Mashine za Maabara ya Hospitali ya Abdullah Mzee Mkoani.
Alisema hatua hiyo atalazimika kuitekeleza mara moja dhidi ya mtendaji au Kiongozi muhusika atapoamua kufanya ziara nyengine katika Hospitali hiyo ataporejea tena Kisiwani Pemba muda wowote kuanzia sasa.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo alipofika kuangalia uwajibikaji wa Watendaji katika kutoa Huduma za Afya kwa Wananchi katika Hospitali ya Rufaa ya Abdullah Mzee Mkoani ikiwa ni utaratibu wake aliojipangia wa mara kwa mara anapofanya ziara Kisiwani Pemba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema inasikitisha kuona kwamba Serikali Kuu kwa kusaidiana na Washirika wa Maendeleo inajikita kuimarisha Miundombinu katika Sekta ya Afya kwa alengo la kutoa huduma sahihi za Afya lakini wapo baadhi ya Watendaji wamekuwa na tabia ya kuleta dharau katika matumizi ya Vifaa wanavyopatiwa.
“ Nikija tena katika ziara zangu za mara kwa mara kama havijawekwa Vifaa vya  kupoza Umeme unaoingia katika Mashine za Maabara nitalazimika kuchukuwa hatua ziazostahiki kwa Mtendaji mzembe”. Alisisitiza Balozi Seif.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika jitihada zake za kuimarisha Sekta ya Afya kwa kugharamia  ununuzi wa vifaa vya kisasa  vyenyethamani kubwa isingependa kuona zipo dalili zinazoashiria hujuma za makusudi zinazojaribu kuvita jitihada hizo muhimu kwa ustawi wa Jamii.
Mapema Mkuu wa Kitengo cha Maabara cha Hoapitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee Mkoani Dr.Mohamed Mjaka Khamis alisema changamoto kubwa inayowakumba katika utendaji wao wa kila siku ni uzimikaji wa mara kwa mara wa huduma za Umeme.
Dr. Mjaka alisema changamoto hiyo wakati mwengine ndio inayosababisha baadhi ya Mashine za Maabara hiyo kuharibika kutokana na ukosefu wa Vifaa vya kupoza Umeme kwa ajili ya ulinzi wa Mashine za Maabara ya Hospitali hiyo.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi alikagua Maendeleo hya Ujenzi wa Jengo Jipya la Skuli ya Sekondari ya Uweleni iliyopo ndani ya Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba unaofanywa kwa Nguvu za Wananchi wanaoungwa Mkono na Washirika mbali mbali wa Maendeleo ndani na nje ya Nchi.
Akizungumza na Uongozi wa Skuli hiyo Balozi Seif  alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutafuta wafadhili ili kuona changamoto inayowakwaza Wanafunzi wa Skuli hiyo ya uhaba wa Madasrasa inatanzuka.
Alisema Sera ya Elimu Zanzibar katika Miundombinu ya ujenzi wa Majengo ya Madarsa sehemu mbali mbali Unguja na Pemba ni kwa Wizara husika ya Elimu na Mafunzo ya Amali kukamilisha uwezekaji pamoja na samani za ndani kwa Madarasa yote yaliyoanzishwa na Wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wananchi, Wazazi,Walimu, pamoja na wafadhili wa Wilaya ya Mkoanuikutokana na hamasa zao za muamko uliopelekea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuimarisha Sekta ya Elimu Nchini.
Balozi Seif alisisitiza kwamba hakuna mtaji  au Rasilmali kubwa na muhimu ambayo mzazi anaweza kuwekeza kwa Mtoto wake isipokuwa Elimu ambayo ndio njia sahihi ya kumjengea hatma njema wakati wa Uzee wake.
Mapema akitoa Taarifa ya ujenzi wa Jengo Jipya la Skuli ya Sekondari ya Uweleni Mwalimu Mkuu wa Skuli Hiyo Shehe Hassan alisema wazo lka ujenzi huo limekuja kufuatia changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili Wanmafunzi wa Skuli hiyo ya ufinyu wa Madarasa.
Mwalimu Shehe alisema Uongozi wa Skuli hiyo kwa kushirikiana na Wazazi wa Wanafunzi hao walilazimika kuanza michango iliyotokana na Mishahara yao kuanza ujeni huo ili ukidhi mahitaji ya ongezeko la Wanafunzi waliofikia Elifu 1,149 hivi sasa wanaolazimika kuingia Mikondo Miwili.
Alisema ujenzi  wa jengo hilo utakaokuwa na Madarasa Sita, Ukumbi wa Mikutano pamoja na Ofisi ya Walimu ulianza mnamo Mwaka 2011, lakini changamoto liliopo hivi sasa ni umaliziaji wa tofali za juu pamoja na ukuta wa kuhifadhia Jengo hilo.
Akitoa shukrani zake Waziri wa Elimu na Mfunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma aliuahidi Uongozi wa Skuli hiyo pamoja na Wazazi wa Uweleni kwamba Wizara ya Elimu itabeba jukumu la kumaliza kazi iliyobakia.
Alisema licha ya jukumu la Wizara kumalizia uwezekaji na samani ya Vifaa vya ndani lakini imekubali kusidia nguvu kutokana na jitihada kubwa iliyotekelezwa na Wazazi, Viongozi na Walimu katika kujenga Jengo hilo jipya la Skuli ya Uweleni ili kupunguza msongamano wa Wanafunzi wake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.