Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na mgeni wake Mtawala wa Ras Al Khaimah Shaikh Saud bin Saqr Al Qasimi (kushoto) wakati alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kabla ya kuondoka nchi akimaliza ziara yake akiwa na ujumbe wa Viongozi mbali mbali aliofutana nao,[Picha na Ikulu.] 24/10/2018.
Mtawala wa Ras al Khaimah Shaikh Saud Bin Saqr Al
Qasimi amemuhakikishia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Dk. Ali Mohamed Shein kuwa serikali yake itatoa ushirikiano katika kufanikisha
shughuli ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kupitia Mkataba uliosainiwa hapo
jana.
Shaikh Saud Bin Saqr Al
Qasimi aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na mwenyeji wake Rais
Dk. Shein katika ukumbi wa Ikulu mjini Zanzibar, ambapo katika mazungumzo
hayo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd alihudhuria pamoja na viongozi
wa Ras al Khaimah na wa Zanzibar.
Katika maelezo yake,
Shaikh Al Qasimi alisifu juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Kampuni ya RAK GAS ya Ras al Khaimah
katika kutekeleza mipango iliyopo ya utafutaji wa nishati hiyo.
Katika mazungumzo hayo,
Mtawala huyo alieleza kuvutiwa kwake na mipango inayoendelezwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta ya mafuta na gesi hasa kwa maamuzi
yaliyofikiwa ya kutaka kujenga bandari maalum ya mafuta na gesi katika eneo la
Mangapwani.
Aidha, Mtawala huyo
alisema kwamba Serikali ya Ras al Khaimah itatekeleza ahadi iliyoitoa mwezi
Januari mwaka huu wakati Rais Dk. Shein alipotembelea nchi hiyo ya kushirikiana
na Zanzibar kinyenzo na kitaalamu katika kujitayarisha kuingia katika uchumi wa
mafuta na gesi asilia.
Shaikh Saud Bin Saqr Al
Qasimi ambaye hapo jana aliungana na Rais Dk. Shein katika viwanja vya Ikulu
mjni Zanzibar kushuhudia utiaji saini Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa
Mafuta na Gesi Asilia, alisema kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa kuzingatia kwamba
nchi kadhaa duniani zinapata changamoto kwa kushindwa kujitayarisha vizuri
katika kuipokea sekta hiyo.
Kadhalika kiongozi huyo alisifu
juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza
sekta ya utalii na kuahidi kwamba Serikali yake itaendelea kutoa ushirikiano
unaohitajika ili Zanzibar iweze kufikia malengo yake iliyojiwekea katika
kuendeleza sekta hiyo.
Kiongozi huyo
alimuhakikishia Rais Dk. Shein kwamba Ras al Khaimah inatumia uzoefu wake
ulionao kwa kushirikiana na Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha sekta ya
utalii nchini.
Kuhusu sekta ya elimu,
Kiongozi huyo aliipongeza Serikali ya Mpinduzi ya Zanzibar chini yauongozi wa
Rais Dk. Shein kwa juhudi inazoendelea kuzichukua katika kuendeleza sekta ya
elimu ili kuweza kukidhi mahitaji ya wataalamu wanaohitajika nchini katika
sekta mbali mbali pamoja na kuweza kwenda sambamba na mahitaji ya karne ya 21.
Kiongozi huyo alieleza
kuwa ili kuhakikisha Zanzibar inafikia azma ya kuwa na wataalamu wa kutosha
aliahidi kwamba pande zote mbili zitashirikiana kuimarisha sekta ya elimu kwa
nchi hiyo kutoa nafasi za masomo kwa wananchi wa Zanzibar pamoja na
kubadilishana wanafunzi baina ya pande mbili hizo.
Alieleza kwamba
wananachi wan chi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wanahistoria kubwa
inayoonesha kuwa wamekuwa na ushirikiano wa kidugu na ndugu zao wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na kwamba ziara hiyo itazidi kuimarisha uhusiano na
ushirikiano uliopo.
Alisema kwamba ziara
yake hiyo inatoa fursa nzuri ya kuharakisha utekelezaji wa mambo mbali mbali
yaliyokubaliwa katika ziara aliyoifanya Rais Dk. Shein mwezi Januari mwaka huu
katika nchi za Falme za Kiarabu.
Nae Dk. Shein kwa upande
wake alitumia fursa hiyo kwa kueleza juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na
Serikali katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ili kuimarisha ustawi wa
wananchi.
Rais Dk. Shein alieleza
kuwa mafanikio yanayoendelea kupatikana katika sekta ya utalii ambayo ni muhimili
mkuu wa uchumi wa Zanzibar hivi sasa na kueleza azma na mikakati iliyowekwa ili
kuongeza idadi ya watalii ifikapo mwaka 2020.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza mipango ya Zanzibar ya kujenga bandari maalum ya kusafirisha mafuta na
gesi asilia kwa azma ya kurahisisha usafiri wa nishati hiyo ili kuondoa
changamoto zilizopo hivi sasa za usafirishaji wa bidhaa pamoja na kujitayarisha
na mipango ya hapo baadae.
Rais Dk. Shein alitoa
shukurani kwa Mtawala huyo kwa kukubali kushirikiana na Zanzibar katika juhudi
zake za kuimarisha sekta ya elimu, kwa kukubali kutoa nafasi maalum za masomo
kwa wanafunzi wa Zanzibar katika nyanja mbali mbali zinazofundishwa katika vyuo
vya Ras al Khaimah.
Alitoa shukurani maalum
kwa Serikali ya nchi hiyo kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi
zake za kukuza uchumi na kuimarisha utoaji huduma mbali mbali za kijamii ikiwa
ni pamoja na kusaidia kuimarisha sekta ya maji safi na salama hapa Zanzibar.
Alieleza haja kwa Ras al
Khaimah kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii hasa
ikizingatiwa kuwa nchi hiyo tayari imeshapata mafanikio makubwa katika sekta
hiyo huku akieleza umhimu wa pande mbili hizo kushirikiana katika sekta ya
usafri wa anga hatua ambayo itasaidia shughuli za utalii, biashara na shughuli
nyenginezo za kijamii.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein amemueleza kiongozi huyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imejidhatiti kuyatekeleza makubaliano yote yaliyokubaliwa katika ziara zote
zilizofanyika nchini humo pamoja na yale yote yaliyokuwemo katika Mkataba wa
Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia.
Shaikh Saud Bin Saqr Al
Qasimi ameondoka nchini leo kurejea Ras al Khaimah ambapo katika uwanja wa
ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume aliagwa kwa heshima zote za Kitaifa pamoja
na kuagwa na viongozi mbali mbali wa Serikali wakiongozwa na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment