Mkuu wa Idara ya Huduma za Sheria wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi Emmanuel Kawishe akifafanua hoja katika mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi.
Mkuu wa Idara ya Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
Irene Kadushi, akifafanua jambo wakati wa mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi.
Afisa Uchaguzi Meshack Mgovano, akieleza jambo kwenye mafunzo
kwa wasimamizi wa uchaguzi.
Picha zote na NEC
Na Margareth Chambiri
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
imewaonya Wasimamizi wa Uchaguzi ambao ama kwa kujua au kwa makusudi wataharibu
au kukiuka taratibu za Uchaguzi kutokana na kutofuata sheria na taratibu za
Uchaguzi.
Onyo hilo limetolewa na
Makamu Mwenyekiti wa Tume Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Mbarouk Salum Mbarouk wakati akifungua
mafunzo kwa Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi jijini Dodoma.
Mheshimiwa Mbarouk ambaye
amewataka Wasimamizi hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea amesema Sheria ya Taifa
ya Uchaguzi na ile ya Serikali za Mitaa zinaunda kosa la jinai na kutoa
masharti ya adhabu kwa Afisa yeyote wa Uchaguzi ambaye atasababisha kuharibu
uchaguzi.
Makamu Mwenyekiti huyo wa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
amesema madhara ya
kutozingatiwa kwa taratibu za Uchaguzi ni kusababisha kesi nyingi za Uchaguzi
na kuitumbukiza Serikali katika gharama ambazo zingeweza kutumika katika
shughuli nyingine za maendeleo.
Amewataka Wasimamizi na
Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kuyaelewa vyema maeneo wanayofanyia kazi na
kujiamini ambapo pia amewakumbusha jukumu walilo nalo la kuimarisha imani ya
wananchi na wadau wengine wa Uchaguzi kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi
Dkt Athumani Kihamia amewataka washiriki wa mafunzo hayo kutoa ushirikiano kwa
vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Mdogo ikiwa ni pamoja na
kuvishirikisha katika kila hatua muhimu wakati wa mchakato wa Uchaguzi.
Dkt. Kihamia amesema Watendaji
wote wa Tume wanapaswa kuwapo katika maeneo yao ya kazi wakati wote hususan
kipindi cha Uteuzi, kufungua ofisi hadi muda wa kisheria na Vyama vyote ambavyo
vimefuata taratibu vipewe fomu za Uteuzi na Wagombea wao wateuliwe kama
wamekidhi vigezo.
Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi
ameongeza kusema kuwa kutozingatiwa kwa mambo hayo husababisha kuharibu imani
ya Wadau na kusababisha malalamiko ya kutoridhishwa na mchakato wa Uchaguzi na
hatimaye mashauri ya Uchaguzi kufikishwa mahakamani.
Kadhalika Dkt Kihamia
amewataka Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi hao wa Uchaguzi kutojihusisha na
migogoro ya ndani ya Vyama na iwapo Vyama vitakuwa na malalamiko vielekezwe
kuwasilisha malalamiko yao kwenye Kamati za Maadili na si mahali pengine
popote.
Kwa mujibu wa Dkt. Kihamia
chaguzi zote duniani ni kielelezo cha demokrasia na kwamba Uchaguzi huru na wa
haki hutokana na Wasimamizi wa Uchaguzi wanaozingatia Sheria, Kanuni na
Taratibu zinazosimamia Uchaguzi husika.
Jumla ya Wasimamizi na
Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi 210 kutoka katika Majimbo manne ya Serengeti,
Simanjiro, Ukerewe na Babati Mjini pamoja na Kata 47 zinazotarajiwa kufanya
Uchaguzi Mdogo Desemba 3, mwaka huu wanashiriki katika mafunzo hayo
yatakayodumu kwa siku tatu jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment