Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Azungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania.

 Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya  Nguvu za Atomiki Tanzania {TAEC} Profesa Lazaro Busagala Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi SDeif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar alipofika kujitambulisha baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya  Nguvu za Atomiki Tanzania {TAEC} Profesa Lazaro Busagala wa Nnne kutoka Kulia akifafanua majukumu ya Tume yake mbele ya Balozi Seif alipofika kujitambulisha.
Profesa Lazaro Busagala Kulia akimkabidhi Balozi Seif baadhi ya Vitabu vyenye maelezo ya Majukumu ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania { TAEC .
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya  Nguvu za Atomiki Tanzania {TAEC} Profesa Lazaro Busagala wa Nnne kutoka Kulia akifafanua majukumu ya Tume yake mbele ya Balozi Seif alipofika kujitambulisha.Na.Othman Khamis.OMPR. 
Watanzania lazima waendelee kubakia salama na Afya chini ya matumizi sahihi ya Mionzi inayotokana na Teknolijia ya Nyuklia Duniani ambapo kwa Tanzania yanaratibiwa na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania {TAEC}.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Profesa Lazaro Busagala alisema hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar alipofika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kuiongoza Taasisi hiyo ya Teknolojia.
Profesa Lazaro Busagala alisema Tume hiyo iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Nambari 7 ya Mwaka 2003 kulingana na kifungu nambari 6{1} cha Saheria ya Atomiki imepewa jukumu la kudhibiti matumizi salama ya Mionzi, kuhamasisha na kupanua matumizi salama ya Teknolojia ya Nyuklia pamoja na kutoa ushauri na taarifa tofauti za Kisayansi na Teknolojia ya Nyuklia.
Alisema udhibiti huo una lengo la kulinda Umma, Wafanyakazi pamoja na mazingira dhidi ya madhara ya Mionzi jukumu linalowapa mamlaka ya kufanya ukaguzi wa Vituo vitoavyo huduma ya mionzi Nchini ili kujiridhisha na hali ya usalama.
Profesa Lazaro alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba zipo Hospitali 72 Nchini Tanzania zilizofungiwa kutoa huduma za Mionzi baada ya kubainika matatizo yanayopelekea kuathiri kwa Wagonjwa wasiopungua Laki 262,000 kwa Mwaka.
Alifahamisha kuwa Ugonjwa wa Saratani unaoibuka kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo zile za Mionzi umeongezeka kwa asilimia 30% hadi 40% katika kipindi cha Miaka Mitatu iliyopita hali inayowafanya Wataalamu wa Tume hiyo kuwa makini katika utekelezaji wa majukumu yao katika kusimamia udhitibi mzuri wa matumizi ya Mionzi.
Profesa Lazaro alisema matumizi ya Teknolojia ya Mionzi Nchini hivi sasa tayari yameibua vianzio zaidi ya 700 vinavyotokana na huduma za Hospitali, Viwanda pamoja na vifaa ya Utengenezaji wa Bara bara.
Akizungumzia masuala ya Ufundi wa vifaa vinavyotokana na Mionzi Mkurugenzi Mkuu huyo wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Profesa Lazaro alieleza kwamba Tume ina maabara Maalum inayofanya kazi ya kuratibu, kutoa huduma ya kudhibiti ubora wa Vifaa vya Nyuklia pamoja na mafunzo ya Ufundi.
Alisema wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imesharidhia kuipatia Tume hiyo eneo la Ujenzi wa Maabara kwa upande wa Zanzibar ili iendelee kutekeleza majukumu yake ya ufanisi mzuri zaidi lengo la Maabara hizo ni kuimarisha  uwezo wa Taifa katika ufundi wa Vifaa vya Nyuklia.
Profesa Larazo alieleza kuwa baadhi ya huduma zinazotolewa na Maabara kufuatia maombi ya wadau mbali mbali ni pamoja na matengenezo ya mashine za Hospitali za X – ray, Vifaa vya kisayansi vinavyotumika katika utafiti, Viwanda na Hospitali.
Kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya Kilimo kwa matumizi bora ya Mionzi Mkurugenzi Mkuu huyo wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania alisema lipo ongezeko kubwa la uzalishaji katika kilimo cha Mpunga, Migomba, Mahindi na Shairi hatua iliyowapa matumaini makubwa Wakulima hasa upande wa Zanzibar.
Profesa Lazaro alisema mafanikio hayo yalikwenda sambamba na udhibiti wa maradhi mbali mbali kwenye mimea na Matunda yaliyokuwa yakisababishwa na wadudu Mbuno ambapo Zanzbar ilifanikiwa kupiga vita maradhi hayo mnamo Mwaka 1998 baada ya upandishaji mbegu za kuzuia ongezeko la Wadudu hao chini ya Utaalamu wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani {IAEA}.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliueleza Ujumbe wa Viongozi wa Tume hiyo ya Nguvu za Atomiki Tanzania kwamba Jamii bado ina uelewa mdogo juu ya tafrisi sahihi ya masuala ya Nguvu za Atomiki.
Balozi Seif alisema Watu wengi wana ufahamu wa Atomiki na masuala yanayotokana na nguvu za Kijeshi wanazofikiria zinaweza kuleta athari ya maangamizi wakati wowote iwapo wasimamizi wake watatumia visivyo stahiki.
Alisema ipo haja ya Wataalamu wa Tume hiyo kuendelea kutoa Taaluma kwa Jamii ili iondoe shaka sambamba na kujilinda na masuala ya Mionzi katika misingi halali inayokubalika Kitaaluma.
Akielezea faraja yake kutokana na uelewa na majukumu ya Tume hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba Uongozi wa juu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania {TAEC} kuandaa Mafunzo kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaowakilisha Wananchi katika Majimbo yao ili kwa hatua za awali Taaluma ya Teknolojia ya Nuklia isambae kwa Jamii nzima.
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania yenye Makao Makuu yake Mjini Arusha iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Nambari 7 ya Mwaka 2003, awali ilikuwa ikijuilikana kama Tume ya Taifa ya Mionzi iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Nambari 5 ya Mwaka 1983.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.